Kilinge cha Mawasiliano
Mabadiliko na kazi ya timu ya mawasiliano
OFISA mmoja wa mawasiliano alinipigia simu asubuhi baada ya kusambaa kwa taarifa kwamba Dkt. Emmanuel Nchimbi amefukuzwa ndani ya chama chake; CCM.

Hakutaka somo la historia kutoka kwangu. Alitaka kujua tu la kusema. “Tuwaambie nini watu?”
Baada ya zaidi ya muongo mmoja kwenye tasnia hii, naweza kukuambia hilo ndilo swali gumu kuliko yote niliyoyapata.
Kwa sababu mabadiliko ya uongozi kamwe siyo mabadiliko tu. Kiongozi wa juu anapoondolewa, kazi yetu sisi watu wa mawasiliano na umma hubadilika.
Watu wasipojua kilichotokea, huanza kubuni. Na kubuni hugeuka uvumi haraka, kwamba chama kinasambaratika, kwamba fulani ni mgonjwa, kwamba sera kubwa zinakaribia kubadilika. Uvumi hautulii.
Hivyo kazi ya kwanza ni kuzungumza mapema na kwa uwazi; ujumbe mmoja uliokubaliwa na wote, unaotolewa kabla habari potofu haijaenea. Hatuachi watu wauone kama ni “mgogoro.”
Tunaueleza kwa maneno ya utulivu, serikali inajipanga upya ili ifanye kazi vizuri zaidi na kuwahudumia watu kwa haraka. Kunyamaza hakusaidii. Ukimya hutoa tu nafasi kwa uvumi kukua.
Lakini ujumbe mmoja hautoshi, kwa sababu mabadiliko ya uongozi hugusa makundi mengi kwa wakati mmoja, na kila kundi lina wasiwasi wa jambo tofauti.
Watumishi wa serikali wanataka kujua kama kazi zao ziko salama na kama maagizo yao bado yanasimama.
Viongozi wa chama wanahitaji kusema jambo lilelile, ili wasiwepo wawili wanaosema tofauti hadharani.
Wafanyabiashara na wawekezaji, ambao wanaweza kuyumbisha thamani ya fedha na bei kwa uvumi mmoja tu, wanahitaji kusikia kwamba mambo yako imara.
Washirika wa nje na balozi, ambao wamekuwa wakiifuatilia nchi hii kwa karibu tangu Oktoba iliyopita, husoma kila ishara.
Na umma, kundi kubwa na lisilo na subira kuliko yote, unahitaji ukweli ulio wazi kabla hadithi za kutunga hazijawafikia. Hivyo hatuwaambii wote kwa mara moja.
Tunawaambia watu wa ndani kwanza, ili taarifa ya hadhara inapotoka, asiwepo anayeshtukizwa.
Katikati ya haya yote, ni lazima pia tuonyeshe kisichobadilika. Nyuso ni mpya, lakini malengo, ahadi na mwelekeo havijabadilika. Na ni lazima tuseme haya kama binadamu wa kweli, siyo kama mashine, kwa maneno ya wazi na ya upole. Katika wakati wa wasiwasi, watu huamini ujoto wa moyo, si maneno makubwa. Watu wanaweza kukubali mabadiliko. Wasichoweza kukubali ni kuzungumzwa nao kana kwamba ni wapumbavu.
Kisha huja sehemu ambayo wengi husahau; mabadiliko ya uongozi si mwisho wa hadithi. Ni mwanzo wa hadithi nyingine. Siku thelathini za kwanza huamua kama watu watamkubali kiongozi mpya au watamvumilia tu.
Hivyo tunamtambulisha kwa uangalifu, siyo kwa kelele, ziara za mapema, mikutano ambayo yeye husikiliza zaidi kuliko kuongea, na jitihada za kweli za kujenga imani badala ya kuitegemea.
Pia tunaacha kuongea kutoka juu kwenda chini pekee. Tunawaruhusu watu wajibu, kupitia majukwaa ya wazi na maswali ya ukweli, na tunaendelea kufuatilia habari na hisia za watu, ili tuweze kujibu uvumi mdogo kabla haujakua moto.
Mwandishi wa safu hii ni mtaalamu wa Uhusiano na Umma (PR).
- Mawasiliano
- Uhusiano na Umma
- Uongozi