Kilinge cha Mawasiliano
Sifa ya wakili na mtaji wake usioonekana
FIKIRIA asubuhi moja umeamka na tatizo la kisheria linalohitaji wakili. Hutafungua tu orodha ya majina na kuchagua kibahati-bahati, bali utamuuliza rafiki, utatafuta jina fulani mtandaoni na utaangalia ni nani ambaye watu wanamwamini.
Kabla hata hujakutana na wakili uso kwa uso, tayari umekwishakutana na taswira yake ambayo ndiyo taswira ya kazi ya mawasiliano, yaani Public Relations.
Katika taaluma ya sheria, ambapo uaminifu, uadilifu na heshima ni kila kitu, taswira ya kampuni siyo jambo la kupuuza.
Wateja hawachagui wakili kwa bei pekee, bali wanachagua kwa imani, wanataka kujua kama huyu ni mtu wa kuaminika, mwenye ujuzi na mwenye rekodi njema.
Ndiyo maana mawasiliano mazuri siyo anasa kwa kampuni za sheria, ni uti wa mgongo wa biashara yenyewe.
Kampuni nyingi za sheria hazitumii vyema nguvu ya mawasiliano, zinafikiri kazi yao ni kushinda kesi tu na sifa itakuja yenyewe.
Lakini dunia ya leo siyo hivyo, kwani katika soko lililojaa mawakili wanaofanana, ni taswira ndiyo inayokutofautisha.
Kampuni inayoonekana mara kwa mara katika vyombo vya habari, inayotoa maoni ya kitaalamu, na inayoshiriki katika jamii, hujenga heshima inayowavuta wateja bila hata kuwaomba.
Wakili Peter Kibatala Mawasiliano yanaisaidia kampuni kusimulia hadithi yake, thamani zake, mafanikio yake na namna inavyowajali wateja.
Hadithi hii, ikisimuliwa kwa uthabiti, hujenga daraja la imani kati ya kampuni na jamii.
Maoni mabaya mtandaoni, habari isiyo sahihi, au ujumbe uliopotoka unaweza kuharibu miaka ya kazi ngumu ndani ya siku moja.
Ndiyo maana kulinda sifa kunahitaji uangalifu wa kila siku. Ujumbe wa kampuni, kwenye tovuti, mitandao ya kijamii, na mawasiliano na wateja unapaswa kuwa mmoja na wenye mvuto.
Wataalamu wa mawasiliano husaidia kufuatilia kinachosemwa kuhusu kampuni, na kujibu kwa haraka na hekima pale panapotokea habari isiyo ya kweli. Ni bora kuzuia moto kabla haujawaka kuliko kuuzima baada ya kuteketeza nyumba.
Njia nzuri zaidi ya kampuni ya sheria kujijenga ni kuwafanya mawakili wake waonekane kama sauti za kuaminika katika fani zao.
Wakili anapoonekana akitoa uchambuzi kwenye vyombo vya habari vinavyoheshimika au akizungumza kwenye jukwaa la kitaifa, jina lake hubadilika.
Hakuonekani tena kama mtoa huduma wa kawaida, bali kama mtaalamu anayeongoza.
Mawakili hushughulikia mambo nyeti, kesi tata, tuhuma na mabishano ambayo yakiingia hadharani yanaweza kutikisa kampuni nzima. Wakati kama huu, mawasiliano ndiyo ngao.
Mkakati mzuri wa mawasiliano ya dharura huhakikisha kampuni inajibu kwa utulivu, kwa ujumbe mmoja, na kwa wakati muafaka, bila kukurupuka wala kunyamaza kimya kupita kiasi.
Zama zimebadilika, kuwa na mkakati wa mawasiliano siyo tena hiari kwa kampuni za sheria, ni hitaji la lazima.
Wateja wa leo wanachunguza kabla ya kuchagua, na taswira yako ndiyo inayozungumza kabla wewe hujazungumza.
Kampuni inayowekeza katika mawasiliano hujenga imani, huonekana na hulinda sifa yake katika kila hatua. Mwishoni, swali siyo kama kampuni yako inahitaji mawasiliano, ni kama uko tayari kuiacha taswira yako ijipange yenyewe, au utaamua kuiongoza.
Mwandishi wa safu hii ni mtaalamu wa Uhusiano na Umma (PR).
- Uhusiano na Umma
- Mawasiliano