Kilinge cha Mawasiliano
Sifa ya kampuni haipaswi kuachiwa idara moja
KAMPUNI kubwa duniani hazianguki kwa kukosa bidhaa nzuri, zinaanguka kwa kukosa sifa njema.
Hilo halibishaniwi.
Tatizo linakuja pale wakuu wa vitengo vya Uhusiano na Umma ya Kampuni wanapoendelea kuzungumza lugha ya vyombo vya habari wakati bodi inataka kusikia lugha ya faida, hasara na hatari. Huko ndiko tofauti inapoanzia.
Takwimu za Taasisi ya Kimataifa ya Wakurugenzi (IoD) na Chama cha Wataalamu wa Uhusiano na Umma nchini Uingereza (CIPR), katika ripoti yao ya mwaka 2022 kuhusu upangaji mkakati na maandalizi ya majanga, zinaonyesha jambo zito.
Kwa miaka minne kati ya mitano iliyopita, ukosefu wa uwakilishi wa wataalamu wa Uhusiano na Umma kwenye ngazi ya bodi umeendelea kuwa miongoni mwa changamoto tano kubwa zinazoikabili taaluma hii.
Hii siyo bahati mbaya, ni matokeo ya jinsi taaluma hii inavyojieleza mbele ya wakurugenzi.
Ripoti ya “PR in the Boardroom” ya Jampuni ya Ambitious PR, ikinukuu Jukwaa la Kiuchumi Duniani (WEF), inasema robo ya thamani ya soko la kampuni inahusiana moja kwa moja na sifa yake.
Hizo siyo takwimu za kupuuza katika chumba cha bodi, hatari ya kutokuwa makini nayo ipo.
Benki ya HSBC ilitozwa faini Uingereza baada ya matangazo yake kuonekana yanapotosha kuhusu mchango wake dhidi ya mabadiliko ya tabianchi, huku yakificha taarifa nyingine muhimu kuhusu uwekezaji wake.
Hiyo ndiyo hatari ya kujipamba kwa lugha nzuri bila vitendo vinavyolingana. Bodi haitaki kusikia lugha nzuri, inataka ushahidi.
Kuhusu vipimo, mfumo unaoitwa Integrated Evaluation Framework, unatoa lugha ambayo bodi tayari inaifahamu kutoka idara nyingine za biashara; pembejeo, matokeo ya kazi, mtazamo uliobadilika, matokeo halisi na mchango wa mwisho kwa biashara (impact).
Bodi haitaki kusikia idadi ya magazeti yaliyoandika habari, inataka kujua tabia ya hadhira imebadilikaje na hilo limeigusaje biashara.
Maandalizi ya majanga
Ripoti ya Taasisi ya Ambitious PR inasisitiza mpango wa dharura lazima uwe sehemu ya mpango wa hatari wa bodi tangu mwanzo, siyo taarifa inayoletwa baada ya moto kuwaka.
Kuna somo jingine, ijapokuwa halitoki kwenye tasnia ya PR moja kwa moja. Kiongozi mmoja wa muundo (design) nchini Marekani, Leonardo De La Rocha, kila Jumatatu huandika upya taarifa ya mkurugenzi mtendaji kwa lugha inayoeleweka na timu yake ya watu thelathini.
Anasema pengo kati ya kile bodi inachokijua na kile timu inachohisi ndicho kinachozalisha uvumi na wasiwasi kazini.
Ndicho hasa kinachotakiwa kufanywa na wakuu wa vitengo wa Uhusiano na Umma kutafsiri, kwa pande zote mbili, kutoka bodi kwenda chini na kutoka chini kwenda kwenye bodi.
Shirley Chisholm, mwanamke mweusi wa kwanza kuchaguliwa Bunge la Marekani, aliwahi kusema kama hawakupi kiti mezani, leta kiti chako mwenyewe.
Ndicho hasa wakuu wa Uhusiano na Umma wanapaswa kufanya, siyo kusubiri mwaliko, bali kujenga thamani inayothibitishwa na namba mpaka kiti kiwe cha kwao kihalali.
Kupanga ni kuchagua; wale watakaobaki kwenye lugha ya zamani ya Uhusiano na Umma watabaki nje ya chumba cha uamuzi.
Mwandishi wa safu hii ni mtaalamu wa Uhusiano na Umma (PR). Anapatikana kwa namba: na kupitia email; projects@ lothmakuza.co.tz.
- Uhusiano na Umma
- Uongozi