Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Habari Kuu

Madalali ‘wapiga fedha kibao’ hifadhi za barabara Dar

Ama kweli mjini mambo ni mengi na kila mwanya una fursa zake. Hapa Dar es Salaam, madalali wanapata fedha nyingi kwa kurahisisha mchakato wa kupata maeneo ya kuwekeza kwenye hifadhi za barabara kama Pambazuko linavyodadavua hapa.

Jumatatu, 26 Oktoba 2026 · 02:21Dakika 7 kusoma
Malori yakiwa yameegeshwa kwenye eneo la Hifadhi ya Barabara ya Morogoro, Mbezi kwa Msuguli, Dar es Salaam jana.(
Malori yakiwa yameegeshwa kwenye eneo la Hifadhi ya Barabara ya Morogoro, Mbezi kwa Msuguli, Dar es Salaam jana.( — Na Mpigapicha Wetu

HATUA ya Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) - Mkoa wa Dar es Salaam kuanza kupangisha eneo la hifadhi ya barabara kuanzia Kimara hadi Kiluvya wilayani Ubungo, imeibua wimbi la madalali wanaotumia fursa hiyo kujipatia fedha.

 Madalali hao hupata fedha kwa kuwa “daraja la kuunganisha” wawekezaji na mamlaka zinazohusika kupangisha maeneo ya hifadhi hiyo ya barabara, Pambazuko linaweza kueleza.

Hivi sasa hifadhi ya barabara katika maeneo hayo yamegeuka ‘dili’ na yanapangishwa kwa kasi na kuendelezwa kwa ajili ya uwekezaji wa miradi mbalimbali ya watu binafsi, ikiwamo ujenzi wa vituo vya mafuta, maegesho ya malori, gereji, yadi za kuuza magari, baa na biashara nyingine.

Uchunguzi uliofanywa na Gazeti la Pambazuko kwa wiki kadhaa sasa, umebaini kuwapo kwa kila dalili za ukaribu na uhusiano wenye shaka kati ya madalali na baadhi ya wafanyakazi wa Tanroads ili kuwezesha michakato ya upangishaji kwa haraka zaidi, jambo ambalo linatoa upenyo kwa wajanja kujipatia fedha nyingi kutokana na mradi huo.

Mwandishi wa Pambazuko ametembelea eneo hilo na kuchukua nafasi ya mteja anayetafuta eneo la kukodi na kukutana na dalali aliyemhakikishia kuwa atamuunganisha na baadhi ya maofisa wa Tanroads ili kurahisisha upatikanaji wa kibali cha kukodi eneo kwa ajili ya ujenzi wa kituo cha mafuta.

 Ingawa utaratibu wa Tanroads upo wazi kwa mtu anayetaka kuomba eneo kwa ajili ya uwekezaji na biashara zinazoruhusiwa kisheria, madalali hao wanatumia udhaifu na mazoea ya Watanzania kutafuta urahisi na njia za mkato, jambo ambalo wanalitumia kama fursa kwao kujipatia mamlioni ya fedha.

 Kaimu Msimamizi wa Kitengo cha Matengenezo wa Tanroads Mkoa wa Dar es Salaam, Deogratius Lyatuu, amezungumza na Pambazuko ofisini kwake ambapo amesisitiza wanaohitaji kuwekeza kwenye maeneo hayo kufuata taratibu, kanuni na kisheria.

 Ofisa huyo wa Tanroads anaeleza kuwa kwa sasa matumizi yoyote ya maeneo ya hifadhi ya barabara hiyo yako ndani ya mfumo ambapo yeyote anayetaka kufanya hivyo anaingia, anajisajili, akitimiza masharti anapewa namba ya malipo ya serikali (control number) na akipata majibu ya kukubaliwa, anafanya malipo kisha anapewa kibali.

 “Vibali vinavyotolewa ni vya mwaka mmoja mmoja, na wahusika hutakiwa kuhuisha vibali hivyo kila baada ya mwaka mmoja, hasa kwa wale wanaojenga vituo vya mafuta, ambavyo ni huduma muhimu kwa watumiaji wa barabara,” anasema Lyatuu.

 Licha ya msisitizo huo, baadhi ya waombaji hawana uelewa wa kutosha kutumia mifumo hiyo ya teknolojia ya kisasa, na hivyo kutoa mwanya kwa baadhi ya madalali ambao wanaweza kuwasaidia kukamilisha michakato hiyo haraka.

 Makundi ya madalali

 Katika uchunguzi huo, Pambazuko iliyopiga kambi katika eneo hilo kwa zaidi ya wiki mbili, umebaini kuwepo makundi mawili ya madalali.

 Kundi la kwanza ni madalali wasomi. Hawa ni vijana waliomaliza vyuo vikuu na wana ujuzi wa kutumia kompyuta, mitandao na teknolojia ya kisasa kuingia kwenye mifumo ya Tanroads na kuwajazia fomu wanaoomba vibali vya kuwekeza kwenye eneo hilo kwa gharama ya Shilingi 100,000 kwa kila ombi.

 Mmoja wa vijana hao ambaye ni mtaalam wa teknolojia ya mawasiliano (IT) amesema aligundua kuna ugumu kwenye kuingia na kujaza fomu za maombi kwenye mifumo ya Tanroads, ambapo ilimfanya kutoa fedha kwa mmoja wa wafanyakazi wa taasisi hiyo ili amfundishe namna ya kuingia baada ya kukwama mara kadhaa.

“Nililazimika kutoa fedha kufundishwa namna ya kuingia kwenye mifumo kukamilisha maombi yangu ya kuomba eneo kwa ajili ya biashara. Niliambiwa nitoe Shilingi 100,000. Kuanzia hapo nikagundua hiyo ni fursa nyingine ya kujiingizia kipato...”

 “Unaweza kuingia kwenye mfumo, lakini kutokana na ugumu wa mfumo huo, huwezi kukamilisha taratibu zao, na ugumu unakuja zaidi mtu akitumia simu ya mkononi hawezi kukamilisha maombi yake kwani kuna mahala baadhi ya alama hazionekani mpaka utumie kompyuta au kishikwabi (tablet)...”

 “Na hiyo ni siri ambayo waombaji wengi hawaijui. Na mtu akishaona huo usumbufu analazimika kutafuta msaada, nasi tupo hapa kuwasaidia kwa gharama nafuu kabisa,” anasema kijana huyo ambaye anafanya kazi kwenye moja ya ofisi zilizo karibu na hifadhi ya barabara eneo la Kiluvya, amesema kijana huyo aliyejitambulisha kwa jina moja, Muddy.

 Dalali mwingine ameeleza namna wanavyopata fedha kwa kazi yao ya ukodishaji maeneo licha kwamba kuna mifumo ya Tanroads.

 “Kama unataka eneo kwa ajili ya ujenzi wa ‘sheli’ (kituo cha mafuta) maana yake utahitaji kuanzia mita za mraba si chini ya 1,000, tutakuonyesha eneo zuri ambalo bado halijaguswa,” amesema.

 Kuhusu gharama, dalali huyo ambaye anaonekana kuwa mtulivu na makini, anasema malipo ya kuonyeshwa eneo la kuwekeza kituo cha mafuta maarufu ‘hela ya miguu’ ni Shilingi 50,000.

 Baada ya kuridhika, mteja atatakiwa kulipia kati ya Shilingi 4,000 hadi 5,000 kwa kila mita moja ya mraba nje ya gharama halisi kulingana na kibali atakachopewa.

 Anasema ili kufanikisha mchakato huo lazima uwe na mtu wa Tanroads ambaye anajua maeneo yote yaliyo wazi.

 “Sisi tukipata mteja tunawasiliana nao, na fedha yetu hulipwa kabla mteja hajalipa ela ya serikali kupitia namba maalum (control number),” anasema, huku akitaja jina lake kuwa ni Christopher Massinga.

 Kwa uwekezaji wa yadi ya magari (showroom), maegesho ya maroli na biashara nyingine, madalali wanatoza wastani wa kati ya Shilingi 3,000 mpaka 3,500 kwa kila mita moja ya mraba.

 “Unajua haya maeneo kuna baadhi yapo chini ya Halmashauri ya Ubungo, kwa mfano eneo la Luguruni, kuna eneo la wazi, kwa ajili ya mikutano na shughuli nyingine za kijamii, lakini pia kuna eneo la makaburi...”

 “Haya yote wao ndiyo wanajua matumizi yao, lakini kwa mtu asiyefahamu anaweza kutamani kuwekeza hapo, kumbe haparuhusiwi,” anaeleza.

 Aidha, sehemu ya taarifa kwa umma iliyotolewa na Tanroads Oktoba 21, mwaka huu, 2026, inasema kuwasilisha maombi pekee hakumaanishi kuwa kibali kitatolewa. Kwamba uamuzi hutegemea matokeo ya tathmini iwapo ombi linakidhi masharti yanayotumika.

 Gharama za ukodishaji

 Tovuti ya Tanroads inaeleza kuwa gharama za kukodisha sehemu ya hifadhi ya barabara hiyo katika eneo la Kimara hadi Kiluvya, zinasimamiwa na sheria mpya ya Kanuni za Usimamizi wa Barabara za mwaka 2025, huku eneo hilo likiangukia chini ya kundi la kwanza la ushuru wa kijiografia (Dar es Salaam) ambalo lina gharama kubwa zaidi ikilinganishwa na mikoa au wilaya nyingine.

 Tanroads imeeleza kuwa gharama hizo zimegawanyika katika sehemu kuu mbili; Ada ya Awali ya Usimamizi (kilemba) inayolipwa mara moja wakati wa kuomba kibali, na kodi ya pango ya mwaka inayolipwa kwa kila mita ya mraba, kulingana na aina ya biashara au shughuli kwa eneo la Dar es Salaam.

 Tovuti hiyo inataja kuwa; kwa vituo vya mafuta ada ya awali ya usimamizi ni Shilingi milioni tatu na kodi ya mwaka kwa mita ya mraba ni Shilingi 30,000, yadi ya makontena - gharama ya awali ya usimamizi ni Shilingi 5,000,000 na kodi ya mwaka kwa mita ya mraba ni Shilingi 20,000, yadi ya kuuzia magari ada ya awali ni Shilingi 500,000 na kodi ya mwaka kwa mita ya mraba ni Shilingi 30,000.

 Aidha, eneo la mapumziko/burudani, ada ya awali ya usimamizi ni Shilingi 500,000 kwa mita ya mraba na ada ya mwaka ni Shilingi 20,000 huku migahawa ada ya awali ya usimamizi ikiwa ni Shilingi 300,000 na kodi ya mwaka kwa mita ya mraba ni Shilingi 20,000.

Vyoo vya umma ada yake ya awali ya usimamizi ni Shilingi 300,000 na ada ya mwaka kwa mita ya mraba ni Shilingi 20,000. Kwa biashara ya samani ada ya awali ya usimamizi ni Shilingi 500,000 na kodi ya mwaka kwa mita ya mraba ni Shilingi 10,000.

 Tanroad imeainisha pia kuwa, kwa ajili ya eneo la kuoshea magari, ada ya awali ya usimamizi ni shilingi 500,000, na kodi ya mwaka kwa mita ya mraba ni Shilingi 10,000, maegesho ya malori  ada ya awali ni Shilingi 1,000,000 na kodi ya Shilingi 10,000 kwa mita ya mraba.

 Orodha hiyo imeainisha zaidi kuwa maegesho ya magari madogo, bajaji na pikipiki ada ya awali ni Shilingi 500,000 na kodi ya Shilingi 8,000 kwa mita ya mraba, huku wanaotaka kufungua vibanda vya biashara wakitakiwa kulipia ada ya awali Shilingi 40,000 na Shilingi 15,000 kwa mita ya mraba kwa mwaka.

 Kwa upande wa mamalishe; ada ya awali ni Shilingi 50,000 na ada ya mwaka Shilingi 5,000 kwa mita ya mraba, wauzaji wa matunda na mbogamboga ada ya awali Shilingi 50,000 na kodi ya mwaka  kwa mita ya mraba ni Shilingi 5,000 huku bustani na maeneo ya kilimo soko ada yake ya awali ikiwa ni Shilingi 100,000 na ada ya mwaka kwa mita ya mraba ni Shilingi 3,000.

 Eneo la hifadhi

 Kwa mujibu wa taarifa za Tanroads zinazopatikana katika tovuti yake, Barabara ya Morogoro, katika eneo la Ubungo hadi Kibaha linalindwa na Sheria ya Hifadhi ya Barabara ya Mwaka 1932 na mipango ya Serikali.

 Sheria hiyo inataja umbali tofauti wa hifadhi ya barabara katika baadhi ya maeneo na imeendelea kuwa mwongozo kwa Barabara ya Morogoro.

Tanroads wameainisha kuwa upana wa hifadhi ya Barabara ya Morogoro unatofautiana kulingana na maeneo na umbali kutoka Sanamu ya Askari jijini Dar es Salaam, ukiwa kati ya mita 60 hadi 120 kwa jumla (kutoka katikati ya barabara kwenda kila upande).

Katika kuzingatia sheria, ndiyo maana kulitekelezwa ubomoaji wa nyumba mwaka 2017 ili kupisha ujenzi wa barabara ya njia nane kuanzia Kimara/Ubungo hadi Kibaha.

Umebakiwa na makala 2 za bure mwezi huu. Jiunge ili kusoma bila kikomo.

  • Tanroads
  • Dar
  • Hifadhi ya barabara
  • madalali

Soma Pia