Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Habari Kuu

RC kukumbuka waliouawa Oktoba 29. Wachukua ushauri wa Tume ya Chande haraka

Kanisa Katoliki limewahi kuchukua mapendekezo ya kuchochea amani, haki na ustawi wa Tanzania kwa kukumbuka madhila yaliyotokea Oktoba 29, 2025 na siku kadhaa baada, Pambazuko linaeleza zaidi.

Ijumaa, 23 Oktoba 2026 · 17:22Dakika 1 kusoma
Askofu Pisa akiwa na Jaji Chande kwenye picha ya kuunganisha.
Askofu Pisa akiwa na Jaji Chande kwenye picha ya kuunganisha. — Picha kutoka Maktaba ya Pambazuko

KANISA Katoliki (RC) limeamua kuwahi kufanyia kazi moja ya mapendekezo ya Jaji Mkuu (mstaafu) Mohamed Chande Othman ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Tume ya Rais ya Kuchunguza Matukio ya Ghasia na Uvunjifu wa Amani yaliyotokea wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa Oktoba 2025.

Tume hiyo iliwasilisha mapendekezo yake Aprili 23, 2026 Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Katika kuwasilisha mapendekezo yake kwa Rais Samia Suluhu Hassan, Tume ya Chande ilipendekeza kuwepo kwa siku maalum ya kitaifa kuwakumbuka wote waliopata madhila wakati na baada ya uchaguzi huo.

Tume hiyo ilitaja idadi ya watu waliouawa katika kadhia hiyo ni 518.

Sasa Kanisa Katoliki limetangaza kuwa Oktoba 29, 2026 ni siku ya ibada maalumu kuwaombea waliouawa, kujeruhiwa na kupotea wakati wa  ghasia za Uchaguzi Mkuu mwaka jana, Oktoba 29, 2025.

Katika tangazo lake lililotolewa leo Oktoba 23, 2026 kupitia barua iliyosainiwa na Rais wa Baraza la Maaskofu wa RC (TEC), Wolfgang Pisa  kwenda kwa waumini wake, lilieleza umuhimu wa kufanya hivyo kuwa njia ya kuombea wote waliokumbwa na madhila.

 "Kwa moyo wa kiuchungaji na kwa kutambua wajibu wetu wa kuliongoza Taifa la Mungu, katika ukweli, haki, upendo na mwanga wa Injili, kwa barua hii nawaalika kuadhimisha Misa Takatifu kwa ajili ya kuliombea taifa letu Tanzania na sisi wenyewe, katika kutimiza mwaka mmoja tangu uchaguzi wa mwaka jana,” imesema sehemu barua hiyo.

Barua hiyo iliendelea kueleza kuwa wanawakumbuka baadhi ya watu kuumizwa, kupotea na hata kuuawa na kwamba hali hiyo ya maumivu na msiba bado ipo.

 “Katika mazingira hayo tunaitwa kusimama pamoja kama jumuiya ya waumini tukimkabidhi Mungu mwenye huruma na taifa letu, tukiomba umoja, upendo, ukweli mshikamano ambavyo ni matunda ya haki," ilisema barua hiyo.

 Barua hiyo imeeleza kuwa misa hiyo ifanyike siku ya Alhamisi Oktoba 29,2026 kwenye parokia, vituo vya sala na taasisi za kanisa kadri iwezekanavyo.

Umebakiwa na makala 2 za bure mwezi huu. Jiunge ili kusoma bila kikomo.

  • Chande
  • Askofu Pisa
  • RC
  • Uchaguzi 2025
  • Tanzania

Soma Pia