Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Habari Kuu

Lissu akosa Tuzo ya Sakharov, ICC yaibuka kidedea

Tundu Lissu ameshindwa kutwaa tuzo ya uhuru na haki inayotolewa na Bunge la Ulaya baada ya kushindwa kuipiku Mahakama ya Kimataifa Dhidi ya Uhalifu (ICC) iliyoibuka kidedea.

Alhamisi, 22 Oktoba 2026 · 20:51Dakika 1 kusoma
Tundu Lissu akiwa mahakamani Dar es Salaam ambako anakabiliwa na kesi ya uhaini.
Tundu Lissu akiwa mahakamani Dar es Salaam ambako anakabiliwa na kesi ya uhaini. — Picha kutoka Maktaba ya Pambazuko.

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kiongozi wa upinzani nchini Tanzania, Tundu Lissu, amekosa Tuzo ya Sakharov ya Uhuru wa Mawazo ya mwaka 2026, baada ya Bunge la Ulaya kuitangaza Mahakama ya Kimataifa Dhidi ya Uhalifu (ICC) pamoja na watumishi wake kuwa washindi.

 Rais wa Bunge la Ulaya, Roberta Metsola, ametangaza uamuzi huo leo, Oktoba 22, mjini Strasbourg, Ufaransa, akieleza kuwa dunia inatambua mchango wa mahakama hiyo katika kulinda sheria za kimataifa na kusimamia haki.

Lissu alikuwa miongoni mwa wagombea watatu waliofika hatua ya mwisho. Wengine walikuwa ICC na dada mapacha wa Iran, Taraneh na Romina Rahimi, wanaoshikiliwa gerezani kutokana na kushiriki maandamano dhidi ya serikali yao.

 Ushindi wa ICC umekuja wakati mahakama hiyo ikikabiliwa na vikwazo vya Marekani, hali iliyolifanya tangazo hilo kuwa ujumbe wa kuunga mkono uhuru wa vyombo vya kimataifa vya utoaji haki.

 Rais wa ICC, Jaji Tomoko Akane, ameipokea tuzo hiyo kwa kuishukuru taasisi hiyo ya Ulaya, akisema imekuja wakati mahakama na maofisa wake wanapitia changamoto kubwa.

 Ikiwa na makao yake makuu The Hague, Uholanzi, ICC hushughulikia mashitaka ya mauaji ya kimbari, uhalifu dhidi ya binadamu, uhalifu wa kivita na uhalifu wa uchokozi.

Tuzo ya Sakharov ilianzishwa mwaka 1988 kutambua watu na taasisi zinazotetea haki za binadamu na uhuru wa msingi.

Hafla ya kukabidhi tuzo hiyo imepangwa kufanyika Desemba 16, mwaka huu.

Umebakiwa na makala 2 za bure mwezi huu. Jiunge ili kusoma bila kikomo.

  • Lissu
  • Tuzo ya Sakharov
  • Uhuru
  • Haki

Soma Pia