Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Habari Kuu

Museveni akubali mazungumzo kufuta kesi ya uhaini ya Dkt Besigye

Hatimaye Rais wa Uganda Yoweri Museveni ameridhia kuanza kwa mazungumzo na mpinzani wake mkubwa wa kisiasa, Dkt. Kiiza Besigye ili kuachiwa huru kutoka gerezani anakoshikiliwa kwa tuhuma za uhaini.

Alhamisi, 22 Oktoba 2026 · 19:03Dakika 1 kusoma
Rais Museveni (kushoto) akiwa na Dkt. Besigye kwenye picha ya kuunganishwa.
Rais Museveni (kushoto) akiwa na Dkt. Besigye kwenye picha ya kuunganishwa. — Picha kutoka Maktaba ya Pambazuko

SERIKALI ya Rais Yoweri Museveni imeanza mchakato wa mazungumzo yanayolenga kupata suluhu ya kisiasa juu ya hatma ya mwanasiasa mkongwe wa upinzani nchini Uganda, Dkt. Kizza Besigye, na wakili wake, Erias Lukwago, ambao wanashikiliwa gerezani wakikabiliwa na mashtaka ya uhaini.

Waziri wa Sheria na Masuala ya Katiba, Norbert Mao, amesema mazungumzo hayo yanafanyika kwa maelekezo ya Rais Museveni, yakiongozwa na Jenerali Salim Saleh, ambaye ni ndugu wa rais huyo.

Mao amesema majadiliano yanahusisha wawakilishi wa serikali, familia na baadhi ya viongozi wa kisiasa, yakilenga kuleta maridhiano na kuhakikisha haki za washitakiwa hao zinalindwa, huku lengo kubwa ikiwa kuachiwa huru.

Waziri Mao ameeleza kuwa mazungumzo hayo hayaondoi mamlaka ya mahakama kuendelea kusikiliza kesi zinazowakabili wanasiasa hao.

Hata hivyo, taarifa hizo zimepingwa na mke wa Besigye, Winnie Byanyima, ambaye amesisitiza kuwa mumewe hashiriki mazungumzo yoyote ya kutafuta kuachiwa huru.

Byanyima amesema kipaumbele chake ni kuhakikisha Besigye anapata matibabu yanayostahili na haki ya dhamana, badala ya uhuru wake kutegemea makubaliano ya kisiasa.

Besigye, aliyewahi kugombea urais wa Uganda mara nne, amekuwa kizuizini tangu Novemba 2024, baada ya kukamatwa Nairobi, Kenya, na kurejeshwa Uganda.

Anakabiliwa na mashtaka ya uhaini pamoja na msaidizi wake, Obeid Lutale na mwanajeshi Denis Oola. Wote wamekanusha mashtaka hayo.

Kwa upande wake, Lukwago, aliyewahi kuwa Meya wa Kampala na wakili wa Dkt. Besigye, alikamatwa Juni 2026 na kushtakiwa kwa kosa la kutotoa taarifa kuhusu mipango inayodaiwa kuwa ya uhaini. Naye amekanusha tuhuma hizo na anaendelea kushikiliwa katika Gereza la Luzira.

Hali ya afya ya Besigye na Lukwago imeongeza shinikizo la kutafutiwa ufumbuzi, huku familia na wafuasi wao wakitaka wapatiwe matibabu na haki zao ziheshimiwe.

Hata hivyo, haijafahamika lini mazungumzo hayo yatakamilika, na je, yatazaa makubaliano yatakayowezesha wawili hao kuachiwa huru?

Umebakiwa na makala 2 za bure mwezi huu. Jiunge ili kusoma bila kikomo.

  • Museveni
  • Dkt. Besigye
  • Uganda
  • Uhaini

Soma Pia