Tahariri
Maridhiano ni mwanzo wa Zanzibar mpya
ZANZIBAR inaingia katika hatua muhimu ya kisiasa baada ya Rais wa Zanzibar, Dkt. Hussein Ali Mwinyi na Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, kuafikiana kuhusu utekelezaji wa maridhiano yaliyofikiwa kati ya CCM na ACT-Wazalendo.
Hatua hiyo inafungua ukurasa mpya wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK), huku Othman akitarajiwa kuapishwa kuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Jumanne, Septemba 22, 2026.
Ni hatua inayostahili pongezi kwa sababu, zaidi ya nafasi za kisiasa, inabeba ujumbe mpana kwamba tofauti za kisiasa zinaweza kutatuliwa kwa njia ya mazungumzo, kuvumiliana na kuheshimiana.
Rais Mwinyi na Othman wanastahili kutambuliwa kwa kuamua kuweka mbele maslahi mapana ya Zanzibar na wananchi wake.
Historia ya Zanzibar inaonyesha kuwa tofauti za kisiasa zimewahi kuwa chanzo cha mvutano mkubwa na vurugu katika jamii. Ndiyo maana maridhiano ya sasa hayapaswi kuonekana kama makubaliano ya viongozi wawili au vyama viwili pekee, bali kama fursa ya kujenga mazingira ambayo Wazanzibari wanaweza kuishi na kushirikiana bila kubebeshana mzigo wa tofauti za kisiasa.
Sisi Pambazuko tunapongeza hatua hii, tunasisitiza kwamba mafanikio ya SUK hayatapimwa kwa idadi ya viongozi watakaokuwa serikalini, bali kwa namna itakavyowahudumia wananchi.
Tunaamini kuwa Wazanzibari wanahitaji kuona matokeo chanya na yenye mashiko katika elimu, afya, ajira, uchumi, miundombinu, utalii, uvuvi na huduma nyingine muhimu.
Rais Mwinyi na Othman wana wajibu mkubwa wa kuhakikisha roho ya maridhiano inashuka kutoka kwenye ngazi ya viongozi hadi kwa wananchi wa kawaida.
Ni lazima ujumbe wa umoja ufike vijijini, mijini, kwa vijana, wanawake, wafanyabiashara na makundi yote ya jamii bila kuwepo ubaguzi wa aina yoyote.
Kwa upande mwingine, wananchi nao wana wajibu wa kutumia fursa hii kuweka pembeni chuki na uhasama unaotokana na tofauti za kisiasa.
Ushindani wa vyama ni sehemu ya demokrasia, lakini baada ya ushindani huo, Zanzibar inabaki kuwa nyumba moja inayowahusu wote.
Tunatarajia SUK itakuwa jukwaa la kujenga kuaminiana, kusikilizana na kutafuta suluhisho la changamoto zinazowakabili wananchi.
Makubaliano yaliyofikiwa kati ya CCM na ACT Wazalendo tayari yameweka msingi wa mchakato huo, huku kamati ya pamoja ikiwa sehemu ya utekelezaji wake.
Septemba 22, 2026, kwa hiyo, isiwe tu tarehe ya kuapishwa kwa viongozi, bali iwe alama ya mwanzo wa safari mpya ya Zanzibar; safari ambayo Wazanzibari wataacha tofauti za kisiasa zisitawale maisha yao na badala yake waelekeze nguvu zao katika kujenga uchumi, kulinda amani, kuimarisha demokrasia na kuhakikisha kila mwananchi ananufaika na maendeleo ya visiwa hivi.
Maridhiano ni mwanzo na utekelezaji wa Katiba kwa kuanza SUK ni muhimu kwelikweli kwa mustakabali wa Wazanzibari, huku sasa kazi kubwa ni kuyageuza makubaliano na majukumu ya sasa kuwa matokeo yanayoonekana katika maisha ya kila mwananchi.
- Zanzibar
- Maridhiano
- SUK
- Siasa