Habari
Othman kuapishwa kesho kuingia SUK
Othman Masoud Othman MAKUBALIANO yaliyofikiwa hivi karibuni na vyama vya ACT Wazalendo na Chama Cha Mapinduzi (CCM), yakilenga kukomesha migogoro inayoibuka baada ya uchaguzi Zanzibar, yanatarajiwa kupiga hatua mpya kesho.
Ni siku atakayoapishwa Makamu wa Kwanza wa Rais mteule Othman Masoud Othman katika hafla itakayofanyika Ikulu ya Zanzibar.
Hii inafuatia hatua ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Hussein Ali Mwinyi kumteua Othman kushika wadhifa huo, Septemba 16, baada ya kupokea jina hilo kutoka Chama cha ACT Wazalendo.
Hatua hiyo ilichukuliwa siku mbili tu baada ya Rais Mwinyi akiambatana na Othman ambaye pia ni mwenyekiti wa chama hicho, kuzindua kamati itakayochambua makubaliano yaliyomo kwenye tamko lililotangazwa Julai 9, mwaka huu Ikulu ya Zanzibar, ikiwa ni tamati ya mazungumzo yaliyoanza Novemba mwaka uliopita kufuatia msimamo wa ACT kuwa hakipo tayari kujiunga na Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kwa vile hakiamini kama kulifanyika uchaguzi wa kiwango cha kuzalisha serikali hiyo ya ushirikiano.
Kikatiba, akishaapishwa makamu wa kwanza wa rais, yatakuwepo mashauriano kati ya viongozi hao wawili ya kuwezesha kuundwa serikali kwa maana ya Baraza la Mapinduzi.
Baada ya kuapishwa Dkt. Mwinyi Novemba mwaka jana, alitangaza baraza lake, lakini kwa kujua wakati ule alikosa ushirikiano wa ACT Wazalendo, alibakiza nafasi alizoahidi kuzijaza “muafaka” ukipatikana.
Rais Mwinyi alibakiza wizara za afya na biashara ambazo katika serikali ya 2020 aliteua mawaziri kutoka ACT Wazalendo, na Wizara ya Utalii aliyosema anaitenga kuwapa ACT Wazalendo uwakilishi zaidi serikalini. Nafasi nyingine ni Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais. Mpaka sasa nafasi hizo zina mawaziri wanaokaimu kutoka CCM.
ACT Wazalendo, kama ilivyokuwa mwaka 2020, ulipokuja uchaguzi mkuu wa 2025 ndio chama kilichotangazwa kupata asilimia zaidi ya kumi ya kura zote halali hivyo kikatiba kustahili kuwa mshirika katika kuundwa SUK.
Hafla ya kuapishwa makamu wa kwanza wa rais inachukuliwa na umma kuwa mwanzo wa utekelezaji wa makubaliano, lakini wakati huohuo likiibuka swali kwamba ndio serikali itakuwa imekamilika kwa kuwepo makamu wa kwanza na mawaziri watatu kutoka upinzani?
Au je, hayo ndiyo matakwa ya ACT Wazalendo kwenye makubaliano?
Swali linakuja kwa kuwa kwenye Baraza la Wawakilishi, lenyewe pia likijumuisha wajumbe waliotangazwa kushinda uchaguzi wa uwakilishi majimboni pamoja na wale wa viti maalum walioteuliwa kutokana na uwiano wa kura, wapo wajumbe wachache wa ACT Wazalendo. Ni tisa watokao majimboni na watatu viti maalum.
Hata hivyo, kutarajia jawabu ya hoja hizi kwa sasa itakuwa sawa na kuyavulia maji nguo kabla ya kuufikia mto. Kitaswira, inaonekana picha ambayo CCM itafanya itakalo barazani kwani ina udhibiti mkubwa barazani akiwemo Spika na wasaidizi wote kwenye kiti.
- Zanzibar
- SUK
- ACT Wazalendo
- CCM
- Othman Masoud