Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Habari Kuu

Mhubiri akutwa na hatia ya kuua wafuasi wake 191

Ama kweli imani ni kitu cha ajabu. Kuna wakati inakufanya ushindwe kufikiri. Ona sasa, mtu aliyejipachika uhubiri amelazimisha waumini wake 191, wengi wakiwa watoto, kufunga kula hadi kufa ili waende mbinguni.

Jumanne, 20 Oktoba 2026 · 06:01Dakika 1 kusoma
Mackenzie
Mackenzie — Picha ya mtandaoni

MHUBIRI mwenye utata nchini Kenya, Paul Nthenge Mackenzie, aliyewashawishi wafuasi wake kufunga kula hadi kufa kwa madai kwamba wangekwenda mbinguni kukutana na Yesu Kristo, amepatikana na hatia ya mauaji ya watu 191, wakiwamo watoto 190.

Mahakama Kuu ya Kenya imemtia hatiani Mackenzie pamoja na washitakiwa wengine 28, baada ya kubaini kwamba walitumia mafundisho ya dini kuendesha mfumo wa kuwanyima chakula waumini wa Kanisa la Good News International, hatua iliyosababisha vifo vyao.

Hukumu hiyo ilitolewa jana - Jumatatu, Oktoba 19, 2026, na Jaji Diana Kavedza Mochache, aliyesema ushahidi uliowasilishwa mahakamani umethibitisha kuwa washitakiwa walihusika katika mpango wa kuwalazimisha waumini kufunga hadi kufa.

Mackenzie, aliyekuwa akijitangaza kuwa mtumishi wa Mungu, alidai kwamba kufunga kwa muda mrefu hadi kufa kungewafanya wafuasi wake kuingia mbinguni kabla ya mwisho wa dunia.

Katika mazingira ya kutisha, watoto walikuwa miongoni mwa waathirika wakubwa, huku baadhi yao wakinyimwa chakula na kutengwa chini ya usimamizi wa wazazi wao na viongozi wa kundi hilo.

Mauaji hayo yalifichuka mwaka 2023, baada ya polisi kugundua makaburi ya pamoja katika Msitu wa Shakahola, Kaunti ya Kilifi, ambako zaidi ya miili 400 imefukuliwa.

Ingawa Mackenzie alikanusha kuwalazimisha wafuasi wake kufunga hadi kufa, mahakama imeyatupilia mbali maelezo yake baada ya kupitia ushahidi wa mashahidi mbalimbali.

Mahakama imepanga kutoa adhabu Novemba 6, 2026, huku Mackenzie akikabiliwa na uwezekano wa kupewa adhabu kali kwa makosa hayo.

Tukio hilo limeacha simanzi kubwa nchini Kenya na kuibua mjadala kuhusu matumizi mabaya ya imani za kidini, udanganyifu na wajibu wa mamlaka kuwalinda wananchi dhidi ya viongozi wanaotumia jina la Mungu kuhatarisha maisha ya watu.

Umebakiwa na makala 2 za bure mwezi huu. Jiunge ili kusoma bila kikomo.

  • Mackenzie. Shakahola
  • Kenya
  • Imani

Soma Pia