Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Habari

Mkosoaji wa Kagame auawa, mwili wakutwa bila kichwa

Wakati Rais Paul Kagame wa Rwanda, akiendelea kukanusha kuhusika katika mauaji ya wapinzani wake, mkoaji mwingine wa utawala wake amekutwa ameuawa huko Uganda. Soma zaidi Pambazuko kujua nini hasa kimetokea.

Jumanne, 20 Oktoba 2026 · 06:10Dakika 1 kusoma
Kabera
Kabera — Picha ya Maktaba ya Pambazuko

MWANAHARAKATI wa kisiasa na mkosoaji mkubwa wa Rais Paul Kagame wa Rwanda, Robert Kabera, ameuawa kikatili nchini Uganda, huku mwili wake ukikutwa bila kichwa katika eneo la Mpigi, pembezoni mwa Jiji la Kampala.

Kabera (50), aliyewahi kuwa mwanajeshi katika Jeshi la Ulinzi la Rwanda (RDF), alikutwa ameuawa Jumamosi, Oktoba 17, 2026, katika Kijiji cha Luwala, eneo la Kamengo, wilayani Mpigi.

Polisi Uganda wamesema uchunguzi umeanzishwa kubaini mazingira ya mauaji hayo, huku kichwa cha marehemu kikiwa bado hakijapatikana na hakuna mtuhumiwa aliyekuwa amekamatwa hadi Jumatatu, Oktoba 19.

Msemaji wa Polisi Uganda, Kituuma Rusoke, amesema mwili huo ulitambuliwa na ndugu wa marehemu, ingawa polisi wanaendelea na taratibu za kisayansi kuthibitisha utambulisho wake.

Kabera, aliyekuwa na cheo cha Sajini Meja, alikimbilia Uganda mwaka 2020 baada ya kudai kuwa maisha yake yalikuwa hatarini kutokana na mazingira ya kisiasa nchini Rwanda.

Akiwa uhamishoni, aligeuka mkosoaji mkubwa wa serikali ya Kagame, akitumia mitandao ya kijamii, hususan kituo chake cha YouTube kilichojulikana kama Major Robert TV, kufikisha maoni yake kwa maelfu ya wafuasi.

Mauaji yake yameibua wasiwasi miongoni mwa baadhi ya Wanyarwanda wanaoishi uhamishoni, wakikumbuka matukio mengine ya kuuawa kwa wakosoaji wa serikali ya Kigali katika mataifa mbalimbali.

Miongoni mwao ni Patrick Karegeya, aliyewahi kuwa mkuu wa ujasusi wa Rwanda, aliyekutwa ameuawa jijini Johannersburg, Afrika Kusini mwaka 2014.

Serikali ya Rwanda imekuwa ikikanusha madai ya kuhusika na mashambulizi dhidi ya wapinzani wake.

Umebakiwa na makala 2 za bure mwezi huu. Jiunge ili kusoma bila kikomo.

  • Kabera
  • Rwanda
  • Kagame
  • kifo

Soma Pia