Habari
Siri kikao cha maaskofu, Rais Samia
KIKAO kilichofanywa na Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) na Rais Samia Suluhu Hassan, Ikulu jijini Dodoma kilikuwa na usiri, nyeti na mikakati, Pambazuko limeelezwa.

Katika kikao hicho kilichofanyika Jumatatu Agosti 10, 2026, maaskofu walikwenda na hoja nzito tano kwa Rais Samia, ambazo wameshauri zifanyiwe kazi katika kuongoza juhudi zozote za kuliponya taifa.
Taarifa ya Ikulu kwa umma ilisema mazungumzo hayo yalilenga kuimarisha ushirikiano kati ya serikali na TEC pamoja na masuala mengine ya kitaifa yanayogusa jamii, yakiwamo ya kisiasa, kuimarisha amani na maendeleo, mshikamano na kujenga mustakabali mwema wa Taifa.
Chanzo cha kuaminika kimeliambia Gazeti la Pambazuko kuwa, maaskofu hao wakiongozwa na Rais wa TEC, Askofu Worfgang Pisa, walipeleka hoja tano kwa Rais Samia.
Chanzo hicho kimezitaja hoja hizo kuwa ni pamoja na kumaliziwa kwa mchakato wa Katiba mpya inayojali utu na usawa kupitia maoni ya wananchi yaliyokusanywa na Tume ya Jaji Joseph Warioba, ambapo walisisitiza uanze kwa kushirikisha wadau wote.
Maaskofu pia walihimiza kulipwa fidia kwa watu wote waliopoteza ndugu zao kwenye ghasia za Oktoba 29, 2025, na kuachiwa huru kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu pamoja na watu wengine walioko mahabusu kwa sababu za kisiasa.
Hoja nyingine walizomweleza Rais Samia ni kuhusu vitendo vya utekaji na kutoweka kwa watu ambapo walitaka vikomeshwe huku hoja yao ya tano ikishauri umuhimu wa kuheshimu haki za watu na kuwasikiliza.
“Katika kikao hicho hapakuwa na sauti wala vyombo vya kurekodi, maongezi yaliishia ndani, maaskofu waliwasilisha hoja zao, huku wakinukuu vifungu vya Biblia Takatifu kwa kila kipengele cha hoja walichokiwasilisha…”
Maaskofu pia wameshauri kuwapo maisha ya uadilifu na uwazi, ukweli na uwajibikaji ili kujenga kuaminiana.
Hoja ya matamko ya TEC mara nyingi imekuwa ikihusu kukemea ukiukwaji wa haki za binadamu, kushinikiza uwajibikaji wa serikali na kutetea ustawi wa wananchi.
Hata hivyo msimamo wao mara kwa mara umekuwa ukizua mivutano ya kisiasa na mitazamo tofauti kati ya viongozi wa dini na serikali.
CCM yaibuka
Siku moja baada ya kikao cha Rais Samia na TEC, CCM kupitia jumuiya yake ya wazazi kimeiomba TEC kutumia nafasi yao ya dini kushawishi viongozi wa Chadema kuitikia mwito wa kurejea kwenye meza ya maridhiano ya kisiasa.
Mwito huo umetolewa Agosti 11, 2026 na Katibu wa Jumuiya ya Wazazi CCM Taifa, Ally Hapi, wakati akizungumza na wanachama wa chama hicho na wakazi wa Kilosa Mjini, mkoani Morogoro.
Hapi alipongeza hatua ya Rais Samia na Maaskofu wa Kanisa Katoliki kukutana na kujadili masuala ya kitaifa, na kusisitiza kuwa TEC imeonyesha mfano wa kuigwa wa ukomavu wa kidemokrasia unaopaswa kufuatwa na vyama vya upinzani.
Pamoja na ombi hilo la CCM, msimamo wa sasa wa Chadema kupitia viongozi wake wakuu umekuwa ukisisitiza kuwa hawatashiriki katika mchakato wowote wa maridhiano na serikali au CCM bila kuwepo kwa mpatanishi huru asiyefungamana na upande wowote.
- TEC
- Rais Samia
- Maridhiano
- Katiba Mpya