Habari Kuu
Mizizi historia ya Ndejembi
DEOGRATIUS John Pancras Ndejembi, aliyeapishwa Agosti 29, 2026 kuwa Makamu wa Rais wa Tanzania, amefika katika nafasi ya pili kwa mamlaka nchini akiwa na miaka 43.

Baada ya kuapishwa, mmoja wa wanafamilia yake alisikika akitamka; “Masonrnyii Deo,” – neno la Kigogo lenye maana ya “hongera.”
Kupanda ngazi katika utumishi na hata kazini, kumekuwa kwa kasi; kutoka sekta binafsi, miundo ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), ukuu wa wilaya, ubunge na uwaziri hadi Ikulu.
Wasifu unaorejelewa na Bunge unataja Julai 12, 1983 kuwa tarehe yake ya kuzaliwa, huko Moshi, Kilimanjaro.
Kinachothibitika zaidi ni kuwa ukoo wa Ndejembi, upande wa baba yake, una mizizi eneo la Mkonze, Dodoma, ambako mwanasiasa mkongwe Pancras Mtemi Ndejembi alizikwa Januari 2019.
Baba yake makamu wa rais ni John, huku Pancras akiwa babu yake upande wa baba.
Pancras ndiye kiungo kikubwa kinachoeleza mazingira ya kisiasa aliyokulia Deogratius.
Aliiongoza CCM Mkoa wa Dodoma kwa miaka 25, kuanzia 1982 hadi 2007, na pia akawa mwenyekiti wa wenyeviti wa CCM wa mikoa. Alifariki Desemba 29, 2018 katika Hospitali ya Rufaa ya Dodoma.
Taarifa za mazishi zilisema aliacha mjane, watoto 13 na wajukuu 24, ishara ya ukoo mkubwa uliokuwa na mizizi na ushawishi mkoani Dodoma.
Tofauti na Pancras, historia ya kazi na maisha ya John, ambaye ni baba yake makamu wa rais, haijaandikwa kwa kina katika kumbukumbu zilizopo.
Hata hivyo, Pambazuko linaweza kueleza pasina shaka kwamba baba yake Deogratius, aliishi Moshi kwa muda na ndiko alipokutana na Amina na kuanza uhusiano na hatimaye kupatikana kwa mtoto ambaye sasa ni makamu wa rais.
Baadaye, John alirejea Dar es Salaam akiendelea na maisha na shughuli zake, na kuishi nyumba za Msajili, eneo la Fire, Dar es Salaam.
Deogratius aliishi na baba yake kwa muda kabla ya kupelekwa Dodoma kwa babu yake ambapo alikulia, kusoma elimu ya awali nyumbani, msingi na sekondari kabla ya kwenda Uingereza kwa elimu ya juu.
Ukoo wa mama yake
Mama yake Deogratius, anaitwa Amina Shariff Mudhari, ambaye alizaliwa Moshi na kukulia huko kabla ya kwenda Uingereza kwa ajili ya masomo na kuanza kazi.
Babu yake Deogratius alikuwa mmoja wa waanzilishi wa Uislam mkoani Kilimanjaro na alikuwa miongoni mwa wafanyabiashara na mwalimu wa elimu ya Kiislam kwa miaka mingi. Alifariki na kuzikwa Moshi kwenye makaburi ya Mbuyuni. Bibi yake aliitwa Khadija Mudhari.
Familia ya Deogratius hukutana mara kwa mara kwa ajili ya ibada na kuzulu makaburi ya ndugu zao ambao wengi wamezikwa alikozikwa babu yao.
Kuitafuta elimu
Safari ya elimu ya Ndejembi ilianza Cannon Andrea, iliyoko Dodoma - Mwaka Primary School kati ya 1988 na 1995.
Aliendelea Sekondari ya Jamhuri na Kigurunyembe, kisha Merton College kwa elimu ya juu ya sekondari kati ya 2002 na 2004.
Kuanzia 2006 hadi 2009 alisoma Shahada ya Uhusiano wa Kimataifa katika Chuo Kikuu cha Lincoln, Uingereza.
Baadaye alipata Stashahada ya Juu ya Usimamizi kutoka Institute of Administrative Management. Wasifu wa Bunge pia unaorodhesha masomo ya uzamili katika Chuo Kikuu cha Cumbria kuanzia 2019.
Kusaka maisha
Kabla ya kuingia katika uongozi wa siasa, Deogratius alijenga uzoefu wa biashara na mawasiliano. Mwaka 2012 alikuwa meneja wa Kampuni ya matangazo ya A1 Outdoor; baadaye Mkuu wa Mauzo wa Smile Communications kati ya 2012 na 2014, Meneja wa Kanda wa Kampuni ya Tigo mwaka 2014 hadi 2015, na Mkuu wa Masoko wa GSM Group mwaka 2016.
Kuingia siasa
Kama ilivyokuwa kwa Pancras Ndejembi - babu yake, Deogratius alipenda siasa kutoka kwake na inaelezwa babu yake alipenda kumuita “Mbunge” akimtania kwa kuwa alipenda kuhoji maswali mengi.
Julai 2016, Rais John Magufuli alimteua kuwa Mkuu wa Wilaya ya Kongwa, akahudumu hadi 2020. Mwaka huo alichaguliwa kuwa Mbunge wa Chamwino kupitia CCM.
Baadaye aliteuliwa Naibu Waziri katika Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, kisha akahamishiwa Tamisemi.
Machi 2024 alipandishwa kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, akisimamia kazi, vijana, ajira na watu wenye ulemavu. Julai mwaka huo akateuliwa Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi.
Baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2025, Rais Samia Suluhu Hassan alimteua kuwa Waziri wa Nishati, nafasi iliyomweka katikati ya miradi mikubwa ya uzalishaji na usafirishaji umeme.
Agosti 26, 2026, CCM ilimpendekeza kujaza nafasi iliyoachwa na Dkt. Emmanuel Nchimbi. Siku mbili baadaye, wabunge wote 324 waliopiga kura walimthibitisha; Agosti 29 akaapishwa Ikulu ya Chamwino, Dodoma, kuwa Makamu wa Rais wa 13 wa Tanzania.
Historia yake, kwa hiyo, ina sura mbili. Ni mrithi wa ukoo wenye alama nzito katika siasa za CCM Dodoma, lakini pia ni mtu aliyejenga uzoefu wake katika biashara, utawala na wizara tofauti. Babu yake alimwachia jina na mazingira ya kisiasa; nafasi ya Makamu wa Rais sasa itapima uwezo wa Ndejembi kujenga urithi wake mwenyewe.
- Deogratius Ndejembi
- Makamu wa Rais
- CCM
- Dodoma