Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Tahariri

Ndejembi, kasimamie ustawi wa Tanzania, amani

TUNAMPONGEZA Deogratius John Ndejembi kwa kuaminiwa kuwa Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Jumatatu, 31 Agosti 2026 · 06:00Dakika 2 kusomaToleo 180, uk. 2

Kuapishwa kwake Ikulu ya Chamwino, Dodoma, Agosti 29, 2026, baada ya kuthibitishwa kwa kauli moja na wabunge 324, ni mwanzo wa jukumu zito linalohitaji hekima, uadilifu na uzalendo usiotetereka.

Rais Samia Suluhu Hassan alimshauri akue katika hekima, siyo umri pekee. Ushauri huo una maana kubwa. Nafasi ya Makamu wa Rais siyo ya mapambo, makofi wala kufuata upepo.

Katiba ya Tanzania inamtaja yeye ni msaidizi mkuu wa rais, anayepaswa kumshauri kwa uaminifu na kusaidia kufuatilia utekelezaji wa shughuli za serikali.

Ndejembi anaingia madarakani katika kipindi ambacho Watanzania wanataka maendeleo yanayoonekana, haki inayotendwa na usalama usiochagua.

Sisi Pambazuko tunamtaka atumie nafasi yake kumweleza rais ukweli, hata pale ukweli huo unapokuwa mchungu. Taifa halihitaji wasaidizi wanaosema “ndiyo” kwa kila jambo; linahitaji viongozi wanaotambua hatari mapema na kushauri kwa maslahi ya nchi.

Tunamtahadharisha ajilinde dhidi ya makundi ya watu wanaoweza kumzunguka kwa sifa, majungu na ushauri wenye sumu.

Wapo wanaotumia ukaribu na viongozi kujitajirisha, kuwakandamiza wenzao, kulipiza visasi na kuficha maovu. Watu hao hujivika ngozi ya uzalendo huku wakitafuna misingi ya taifa.

Ndejembi asikubali ofisi yake kuwa daraja la wala kivuli cha wanaotaka kukwepa uwajibikaji.

Zaidi, Ndejembi anapaswa kuwa sauti thabiti dhidi ya utekaji, kupotezwa kwa watu, mateso na matumizi mabaya ya mamlaka.

Aidha, atambue kuwa amani ya Tanzania haiwezi kujengwa juu ya hofu au ukimya wa familia zisizojua walipo wapendwa wao, akahimize kila madai ya kupotea kwa mtu yachunguzwe kwa uwazi, wahusika wawajibishwe na vyombo vya dola vikumbushwe kuwa wajibu wao ni kulinda maisha na haki za wananchi.

Ndejembi pia akaonyeshe kuwa rushwa bado ni adui mkubwa wa taifa, akamshauri rais kuongeza mapambano kuiomomeza.

Tunahimiza zaidi Ndejembi asaidie kusimamia matumizi ya fedha za umma, miradi ya maendeleo, zabuni na uwajibikaji wa watendaji.

Pia, aunge mkono kwa dhati ya moyo wake, taasisi za uchunguzi na kamwe asitetee mtu kwa sababu ya urafiki, chama, cheo au utajiri. Atambue kuwa kwenye rushwa ama fedha zinapoibwa, maana yake Watanzania wanaporwa.

Awe daraja kati ya serikali na wananchi, Tanzania Bara na Zanzibar, watawala na wakosoaji. Asikilize vijana, wanawake, wafanyakazi, wakulima, wafanyabiashara, viongozi wa dini, wanahabari na asasi za kiraia.

Ndejembi ajenge imani kwamba kukosolewa siyo kuchukiwa; mara nyingi ni nafasi ya serikali kuona ilipokosea kabla tatizo halijawa kubwa.

Pia, asimamie kwa karibu ajenda za mazingira na Muungano, ambazo ni miongoni mwa majukumu nyeti ya ofisi yake. Maendeleo yasiharibu vyanzo vya maji, ardhi na maisha ya wananchi, wala tofauti za Muungano zisiachwe kukua kwa ukimya mrefu.

Ndejembi ana nafasi ya kujenga urithi wa kiongozi aliyekuwa mwaminifu kwa rais bila kuisaliti dhamira ya taifa. Uaminifu wa kweli siyo kuficha makosa, bali kuyasema mapema na kusaidia kuyarekebisha.

Tunamtakia mafanikio, lakini tunamkumbusha; makundi hupita, vyeo huisha, na sifa hunyamaza, sasa akatende kazi kuwatumikia Watanzania.

  • Deogratius Ndejembi
  • Makamu wa Rais
  • Utawala bora

Soma Pia