Kilinge cha Mawasiliano
Mlanguzi wa binadamu hununua maneno sio silaha
VITA dhidi ya usafirishaji haramu wa binadamu haitashinda kwa sauti kubwa, bali itashinda kwa akili ya kimawasiliano.
Wapo vijana kutoka Pwani, Singida, Arusha, Mwanza, Tanga na Dodoma waliahidiwa mafunzo na kazi nzuri ya mauzo mkoani Morogoro.
Walipofika, waliwekwa katika mzunguko; walilazimishwa kununua bidhaa za bei mbaya, kisha wakafundishwa jinsi ya kuwashawishi wengine wafanye hivyo hivyo.
Wengi walifundishwa hata jinsi ya kuwadanganya familia zao kwamba wanapata pesa, hakuna aliyewafunga minyororo.
Hawa wote walishikwa kwa maneno, ahadi, mafunzo, mfumo wa “mafanikio” uliopangwa vizuri kiasi cha kuwafanya wawe sehemu ya udanganyifu wenyewe, hii siyo hadithi ya kubuni ni kesi halisi iliyoainishwa katika Ripoti ya Mwaka 2024/2025 ya Tanahut, ambao ni Mtandao wa Kitaifa wa Kupinga Usafirishaji Haramu wa Binadamu, iliyozinduliwa rasmi Agosti 20, 2026 jijini Dar es Salaam.
Ripoti hiyo mpya ya Tanahut, inaonyesha zaidi ya kesi 2,400 zilizoripotiwa Tanzania Bara katika kipindi kilichopita, nyingi zikitoka Ukanda wa Mashariki, hasa Morogoro, ambako pekee kunachangia takriban kesi 1,700.
Ukanda wa Ziwa Victoria; ikiwamo mikoa ya Kagera, Mwanza, Mara, Geita na Simiyu, unafuata kwa kesi 400, kutokana na ukaribu na Ukanda wa Maziwa Makuu, kazi za kilimo cha tumbaku na uchimbaji mdogo wa madini unaowavuta hata raia wa Uganda na Burundi.
Kwa aina ya unyonyaji, “uhalifu wa kulazimishwa” (forced criminality) ndio unaoongoza, zaidi ya matukio 1,000, ukifuatiwa na unyonyaji wa nguvu kazi na unyonyaji wa kingono.
Wavulana wanaonekana zaidi kwenye unyonyaji wa nguvu kazi; wasichana kwenye utumwa wa nyumbani na unyonyaji wa kingono. Hizi siyo namba tu, ni ramani ya jinsi walanguzi wanavyoongea na kila kundi kwa lugha yake.
Ni kujenga simulizi zinazopambana na ahadi za walanguzi bila kutengeneza hofu isiyo na tija, ni kufanya kazi na waandishi wa habari bila kumfichua muathirika mara ya pili kwa jina la habari kali.
Ni kuunganisha serikali, mashirika kama Tanahut ambao ni muungano wa taasisi 105 nchini, vyombo vya habari na sekta binafsi chini ya sauti moja.
Na hapa ndipo tunapaswa kujiuliza swali ngumu; je, tunawasiliana ili kulinda watu au tunawasiliana ili kuonyesha shirika letu linafanya kitu?
Kampeni yenye “views” milioni moja inaweza kuwa sahihi kiuandishi lakini mbaya kimaadili, hasa pale muathirika anapogeuzwa kuwa kielelezo cha kutengeneza huruma badala ya binadamu mwenye heshima na faragha yake.
Sekta binafsi nayo haiwezi kujitoa, kampuni za ajira, uchimbaji madini, kilimo na usafirishaji ndio yanayokutana na waathirika kabla ya mtu mwingine yeyote.
Sera nzuri ya ajira ya haki, ikiwasilishwa vizuri, ni kinga.
Walanguzi wa binadamu hawapigani kwa nguvu tu, bali kwa maneno yaliyopangwa vizuri na kumlenga mtu sahihi na wakati sahihi.
Hadi tutakapoelewa hilo, tutaendelea kuchapisha mabango wakati wao wanajenga mifumo mizima ya “mafunzo” inayogeuza waathirika kuwa mawakala wapya wa udanganyifu.
Vita hii haitashinda kwa sauti kubwa zaidi, itashinda kwa mawasiliano ya karibu zaidi, ya mapema zaidi na yenye akili zaidi kuliko ya adui.
Mwandishi wa safu hii ni mtaalamu wa Uhusiano na Umma (PR). Anapatikana kwa namba: na kupitia email; projects@ lothmakuza.co.tz.
Chanzo: Ripoti ya Mwaka 2024/2025 ya Tanahut, iliyozinduliwa Agosti 20, 2026, Dar es Salaam.
Mwandishi wa safu hii ni mtaalamu wa Uhusiano na Umma (PR). Anapatikana kwa namba: na kupitia email; projects@ lothmakuza.co.tz
- Usafirishaji haramu wa binadamu
- Mawasiliano