Uhusiano
Usifungue kinywa kila muda, jidhibiti
HABARI za leo msomaji wangu wa safu ya uhusiano, karibu kwenye uwanja huu tuweze kushiriki mafunzo na elimu kuhusu masuala mbalimbali ya maisha.
Leo nitazungumza namna udhibiti wa kinywa chako utakavyoweza kukusaidia kukuepusha na mambo yasiyofaa na kukulindia heshima.
Kinywa ni lango la tabia yako, hivyo ni vyema ukawa makini unapotaka kuzungumza jambo hasa wakati unapokuwa na hasira.
Fahamu kuwa maneno mengi uharibu kuliko vitendo. Neno moja lisilofikiriwa vyema linaweza kuvunja ndoa ya miaka 10, kukufukuzisha kazi, au kuwasha ugomvi usiopoa.
Unapokuwa na hasira au unapokasirika akili hushindwa kuchuja mambo na mara nyingi kinywa hushindwa kujizuia kuzungumza jambo lolote kwani na hii inawexza kukusababishia kuropoka jambo baya kisha baadaye ukajuta.
Wakati mwingine unaweza kuudhiwa na mtu ambaye hapo awali mlikuwa mkishirikishana mambo ya siri ndani yake, lakini kutokana na kuudhika dhidi yake ukajikuta unatoa kwa watu siri mlizokuwa mkipeana!
Kwa kuvujisha siri hiyo utaonyesha kwamba wewe si wa kuaminika tena kwa watu.
Ni ukweli usiopingika kwamba katika dunia kila muda, jidhibiti ya leo marafiki, ndugu na jamaa wamekosana na kuvunja uhusiano wao kutokana na kushindwa kuhifadhi au kushindwa kujizuia wanapohitilafiana kwa mmoja wao kuamua kuweka ‘hadharani’ yale yote waliyokuwa wakifichiana.
Mume na mke pia wanapovurugana kwa mambo yahusuyo ndoa yao mara nyingi mwanamke hushindwa kuzuia hasira aliyonayo na kujikuta akiropoka kuhusu madhaifu ya ndoa na kusahau kwamba kuvuka huko mipaka kutamgharimu.
Kutodhibiti vinywa kunaweza pia kufarakanisha familia kwa familia kutokana na kutoleana maneno magumu pale wanapohitilafiana.
Kudhibiti kinywa hakumaanishi kunyamaza milele bali kutumia kanuni ya kufikiri kabla ya kusema; jiulize kabla neno unalotaka kulitamka linajenga au linabomoa? Na kama umelipima kuwa halina maana, nyamaza. Kukaa kimya siyo ujinga, ni hekima.
Mtu anayedhibiti kinywa chake, anadhibiti hatma yake.
Tukutane wiki ijayo.
- Uhusiano
- Mawasiliano
- Tabia