Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Habari

Muafaka Z’Bar waendelea kukamilishwa

MCHAKATO wa maridhiano ya kisiasa kati ya ACT Wazalendo na Chama Cha Mapinduzi (CCM) -Zanzibar, umeingia katika hatua mpya.

Jumatatu, 24 Agosti 2026 · 06:00Dakika 2 kusomaToleo 179, uk. 21

Hatua hizo ni kila upande wa vyama hivyo kukabidhi mapendekezo ya mfumo wa utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa baada ya mvutano wa kisiasa uliofuatia Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana - 2025, Pambazuko linaweza kudokeza.

Mwenyekiti wa ACT Wazalendo, Othman Masoud Othman, amewataka viongozi wa dini, masheikh, maimamu na Wazanzibari kwa ujumla kuunga mkono mchakato huo, akisema wakati umefika wa kuachana na tofauti za kisiasa na kuelekeza nguvu katika utekelezaji wa makubaliano yaliyofikiwa.

Othman, ambaye pia ni Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar mstaafu, amesema pande hizo tayari zimepeana rasimu ya mapendekezo ya namna makubaliano hayo yatakavyotekelezwa. “Tumeshakabidhiana rasimu ya mapendekezo ya mchoro wa kuandaa utaratibu wa utekelezaji ili masuala haya yaweze kutekelezwa.

Baada ya hapo itakuja tume itakayofanya kazi ya kutekeleza jambo moja baada ya jingine,” alisema.

Alitoa kauli hiyo wiki iliyopita kisiwani Pemba wakati wa mkutano maalumu na viongozi wa dini ya Kiislamu, wakiwemo maimamu, masheikh na walimu wa vyuo vya Qur’an.

Makubaliano hayo yalifikiwa baada ya kutokuelewana kisiasa baada ya ACT Wazalendo kutoyakubali matokeo ya uchaguzi mkuu wa mwaka jana.

Hata hivyo, vyama hivyo vilikaa pamoja, kujadiliana na baadaye kutangazwa rasmi kwa maridhiano kupitia tamko la pamoja lililotolewa Ikulu ya Zanzibar Julai 9, mwaka huu.

Othman amesema kufikiwa kwa makubaliano hayo hakukuwa jambo rahisi, kutokana na tofauti kubwa za kisiasa zilizokuwepo na hitaji la pande mbalimbali kujenga uaminifu na maridhiano.

Othman amewataka viongozi hao kutumia nafasi na ushawishi wao katika jamii kuwaunganisha Wazanzibari na kujenga uelewa mpana kuhusu umuhimu wa mchakato wa maridhiano.

Amesema sasa ni wakati wa kuondoa mifarakano na kujenga umoja wa kweli wa Wazanzibari katika kutafuta suluhu ya kudumu ya changamoto za kisiasa.

Maridhiano na uchumi Kwa Othman, lengo la maridhiano siyo kumaliza tofauti za kisiasa pekee, bali pia kuweka mazingira yatakayoiwezesha Zanzibar kusonga mbele kiuchumi na kimaendeleo.

Amesema miongoni mwa vipaumbele vya makubaliano hayo ni kulinda maisha ya watu, mali zao na heshima yao.

Amesema mazingira ya amani na utulivu wa kisiasa ni muhimu katika kuwezesha Zanzibar kufikia maendeleo ya kiuchumi yanayostahili, akitoa mfano wa nchi nyingine zenye mazingira yanayofanana na Zanzibar ambazo zimepiga hatua kubwa kiuchumi.

Othman anatarajiwa kuendelea na ziara kama hiyo ya kukutana na viongozi wa dini na kwamba mikutano hiyo inatarajiwa kuwa sehemu muhimu ya juhudi za kujenga uelewa na kuhamasisha uungwaji mkono wa wananchi wakati Serikali ya Umoja wa Kitaifa ikielezea kwenye hatua ya kuanza kazi.

  • Zanzibar
  • ACT Wazalendo
  • CCM

Soma Pia