Habari
OMO ahimiza ushirikiano serikali, sekta binafsi
Ustawi wa Tanzania unachochewa zaidi kwa kuwepo ushirikiano wa serikali na sekta binafsi kama anavyohimiza OMO uimarishwe na kupewa kipaumbele zaidi.

MAKAMU wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman (OMO), ameitaka serikali na sekta binafsi kuimarisha ushirikiano katika kukuza biashara na uchumi.
OMO amesisitiza kuwa uhusiano huo si hisani bali ni wajibu wa pamoja unaohitaji sera bora, miundombinu imara na uwekezaji wenye tija.
Amesema serikali ina jukumu la kuweka mazingira rafiki ya biashara kupitia sera, sheria na miundombinu inayofanya kazi kwa ufanisi, huku sekta binafsi ikiwajibika kuwekeza, kulipa kodi kwa uadilifu na kutoa ajira kwa Watanzania.
Othman aliyasema hayo jijini Dar es Salaam wakati akifungua Tuzo za SML (2026), zinazotambua mchango wa wadau katika huduma za ugavi, usafirishaji, uhifadhi na masoko ya bidhaa kutoka Tanzania na nchi nyingine za Afrika.
Tuzo hizo zinazotambua na kutoa zawadi kwa taasisi katika sekta za ugavi, usafirishaji na lojistiki, zinatambua ubora, ubunifu na mchango wa kampuni na watu binafsi katika maeneo kama usafirishaji wa mizigo, bandari, usimamizi wa minyororo ya ugavi, usafirishaji wa barabara na reli, maghala na huduma zinazowezesha biashara.
Katika hotuba yake, OMO alisisitiza kuwa Tanzania ina faida kubwa ya kijiografia kutokana na bandari, bahari, maziwa, mito na rasilimali nyingine, lakini rasilimali hizo pekee haziwezi kuifanya nchi kuwa kitovu cha biashara bila mikakati madhubuti ya kupunguza gharama za usafirishaji na kuongeza thamani ya bidhaa zinazozalishwa nchini.
“Lazima tuhakikishe tunakuwa kitovu cha kweli cha biashara Afrika Mashariki badala ya kuwa lango la kupitisha mizigo pekee,” alisema.
Mizigo bandarini kupunguza muda
Katika hatua ya kuimarisha ushindani wa Tanzania, Othman amezitaka Wizara za Uchukuzi na Ujenzi za Tanzania Bara na Zanzibar kuandaa mpango kazi wa kuondoa vikwazo visivyo vya lazima katika bandari na mipakani.
Lengo, alisema, ni kupunguza kwa angalau asilimia 30 muda ambao mizigo hukaa bandarini, hatua inayoweza kusaidia kupunguza gharama zinazobebwa na wafanyabiashara na kuongeza ufanisi wa minyororo ya ugavi.
Kwa wafanyabiashara, muda wa mizigo kukaa bandarini huathiri gharama za uhifadhi, upatikanaji wa bidhaa na uwezo wa kutimiza mikataba kwa wakati. Hivyo, kupunguza ucheleweshaji kunaweza kusaidia kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na nje.
Aidha, amezitaka wizara zinazohusika na utalii kuandaa mikutano ya kimataifa itakayofungua fursa zaidi kwa hoteli za ndani na kukuza huduma zinazohusiana na viwanja vya ndege.
Mitaji nafuu kwa biashara
Makamu huyo wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar amezitaka taasisi za fedha nazo kubuni huduma za kifedha zinazozingatia mahitaji ya biashara za ugavi, usafirishaji na uhifadhi wa bidhaa.
Amesema wafanyabiashara wanahitaji mitaji yenye gharama nafuu ili waweze kusafirisha na kuhifadhi bidhaa zao kwa ufanisi na kupata faida.
Pia ametaka Mamlaka ya Uwekezaji na Maeneo Maalum ya Kiuchumi Tanzania (Tiseza) na Mamlaka ya Kukuza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) kushirikiana kuwasilisha fursa za uwekezaji kwa mabalozi wa Tanzania walioko nje ya nchi ili kuvutia mitaji mipya.
Miundombinu na viwanda
Naibu Waziri wa Uchukuzi, David Kihenzile, akimwakilisha Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa, alisema serikali inaendelea kukamilisha miradi ya kimkakati ya reli na barabara ili kuimarisha miundombinu ya usafirishaji, kukuza uchumi na kuongeza ajira.
Aliitaka sekta binafsi kutumia fursa zinazotokana na uwekezaji huo kwa kuwekeza katika shughuli za usafirishaji na kusaidia juhudi za Serikali za kukuza uchumi.
Naibu Waziri wa Biashara na Maendeleo ya Viwanda Zanzibar, Salum Suoud Hemed, alisema maendeleo ya viwanda yanategemea mfumo bora wa usafirishaji unaowezesha bidhaa kufika sokoni kwa wakati na kwa gharama zinazokubalika.
Waziri wa Utalii na Mambo ya Kale Zanzibar, Nasra Nasro Omar, alisema mfumo imara wa ugavi na usafirishaji ni muhimu katika kukuza utalii kwa kuwa unawezesha wageni kufikia vivutio na kuimarisha shughuli zinazounda mnyororo wa thamani wa sekta hiyo.
Tuzo za SML ziliwakutanisha wataalamu wa ugavi na ununuzi, wawekezaji, wafanyabiashara na wadau wengine kutoka Tanzania, Kenya, Uganda, Rwanda, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Zambia, Malawi na Msumbiji. Zaidi ya tuzo 50 zilitolewa kwa washindi kutoka nchi hizo.
Umebakiwa na makala 2 za bure mwezi huu. Jiunge ili kusoma bila kikomo.
- Makamu Zanzibar
- OMO
- Sekta binafsi