Habari
Padre aadhimisha misa juu ya Mlima K'njaro
MLIMA Kilimanjaro umezoeleka kwa shughuli za utalii pekee, lakini tukio la hivi karibuni limeupa mlima huo mrefu kuliko yote Afrika taswira mpya katika ramani ya utalii wa Tanzania.

Tukio hilo linaonyesha kuwa Mlima Kilimanjaro siyo tena eneo linalovutia wanaopanda milima na wapenda mazingira pekee, bali eneo hilo linaweza pia kuwa jukwaa la utalii wa kiimani - mchanganyiko unaoweza kuongeza thamani ya moja ya vivutio vikubwa zaidi vya nchi.
Jambo hilo limejirudia mwaka huu kupitia hija ya Padre João Silveira, Mmisionari Mkatoliki kutoka Ureno, aliyeshiriki safari ya siku nane kuupanda mlima huo kupitia njia ya Lemosho na kuadhimisha Misa ya Jadi ya Kilatini katika safari hiyo, ikiwamo katika kilele cha Uhuru Peak, mita 5,895 juu ya usawa wa bahari.
Taarifa za waandaaji wa hija zinaonyesha kuwa safari hiyo iliyofanyika mwezi uliopita – Agosti, ilihusisha sala, Misa ya Kilatini na kupanda mlima, huku waumini wakitumia safari hiyo kama hija ya kiroho na pia kuunga mkono kazi za kimisionari Tanzania.
Padre kuadhimisha misa akiwa madhabahuni ni tukio la kawaida, lakini misa hii ilioyoadhimishwa katika kilele cha mlima unaonyesha utafauti mkubwa ukitoa picha ya padre akiwa madhabahuni juu ya mlima wa kitalii.
Kilimanjaro ni moja ya maeneo ya Urithi wa Dunia yanayotambuliwa na Unesco. Ni mlima mrefu kuliko yote Afrika.
Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (Tanapa) inautaja pia kuwa mlima mrefu zaidi duniani usiosimama peke yake (usiokuwa katika safu ya milima).
Takwimu kutoka Wizara ya Maliasili na Utalii zinaonyesha kuwa Mlima Kilimanjaro ulipokea zaidi ya wageni 58,000 wa kimataifa mwaka 2024.
Wakati huohuo, ukanda wa utalii wa kaskazini, unaojumuisha Mlima Kilimanjaro, hifadhi za Serengeti na Ngorongoro, uliendelea kuwa kitovu kikubwa cha mapato ya utalii nchini.
Hivyo, hija kama ya Padre Silveira inaweza kutazamwa kama sehemu ya mabadiliko mapana ya namna Tanzania inavyoweza kukuza sifa za utalii za Mlima huu, kwani tukio hili linaweza kuanzisha safari ya kuufanya mlima huu kuwa eneo la hija (hata kama halitatambuliwa rasmi) kwa waumini wa Kikatoliki kutoka maeneo mengi duniani.
Muhimu zaidi, tukio hili linaonyesha kuwa utalii wa kiimani unaweza kuunganishwa na bidhaa nyingine za utalii badala ya kutazamwa kama shughuli inayojitegemea.
Hija inaweza kuhusisha malazi, usafiri, wapagazi, waongoza watalii, chakula, huduma za afya na shughuli za kitamaduni kabla na baada ya kupanda mlima.
Historia yenyewe inalifanya tukio hili kuwa zito zaidi tangu Johannes Rebmann, mmisionari Mjerumani, alipouona na kuripoti uwepo wa Kilimanjaro mwaka 1848.
Zipo taarifa kuwa Rebmann aliadhimisha Misa kileleni wakati huo, lakini taarifa hizo bado hazijapata uthibitisho.
Aidha, Misa zimewahi kuadhimishwa kileleni na mapadre wengine, akiwamo Fr. Corwin Low mwaka 2022 na Fr. Antony Sumich pamoja na Fr. Gregory Bartholomew mwaka 2015.
Tukio hili linathibitisha kuwa Mlima Kilimanjaro bado ina bidhaa mpya za utalii ambazo hazijatumika kikamilifu.
- Kilimanjaro
- Utalii
- Dini
- Tanapa