Mazingira
Ujenzi wa ukuta wa kilomita mbili Msitu wa Ngezi wakera
UKUTA kuzunguka mradi wa ujenzi wa hoteli ya nyota tano ndani ya Msitu wa Ngezi, Pemba unakera wananchi.
Katika mradi huo wenye uwekezaji wa Shilingi bilioni 17.4 wa hoteli ya kitalii inayomilikiwa na Kampuni ya WIPI Group kutoka China, unalalamikiwa na wananchi kwamba unazinga ustawi wao, ikiwamo kuwanyima njia walizozoea kupita kwa miaka mingi.
Ukuta huo wa kilomita mbili, unajengwa kuzunguka mradi wa hoteli hiyo.
Wakazi wa Jimbo la Konde, maofisa wa idara ya misitu, watafiti na wanaharakati wa mazingira kisiwani Pemba wameiomba Serikali ya Mapinduzi Zanzibar kupitia Mamlaka ya Kuendeleza Uwekezaji Zanzibar (ZIPA) kusitisha ujenzi huo kwani unaharibu mazingira na kutishia shughuli za utalii na kiuchumi miongoni mwa wananchi.
Katika taarifa yake wiki iliyopita, kiongozi wa watafiti wa mazingira kutoka Chuo Kikuu cha Bristol nchini Uingereza, Profesa Tim Caro amesema ujenzi wa ukuta huo ambao ni uzio katika eneo ambalo Hoteli ya Mantuli Eco-Resort inajengwa, pia unazuia shughuli za doria za maofisa misitu katika msitu huo na shamba la mpira la Vumawimbi.
“Ukuta huo pia ni pingamizi katika shughuli za kiuchumi za wananchi kama vile uvuvi, kuongoza watalii katika hifadhi, lakini pia unazuia wananchi kufika katika fukwe za Bahari ya Hindi kwa ajili ya mapumziko,” Prof Caro amesema katika taarifa yake.
Ujenzi wa ukuta huo kwa kutumia matofali yaliyofyatuliwa kijiji cha jirani cha Makangale ulianza mwishoni mwa mwaka jana na kuzua taharuki miongoni mwa wananchi na wanaharakati wa mazingira.
“Malori na mitambo ya ujenzi vimeondoka, lakini bado kuna kibao kirefu chenye maandishi ya Mantuli Eco-Resort na ramani ikionyesha mipaka ya eneo la mradi ambalo asilimia 23 ni eneo la Msitu wa Hifadhi wa Ngezi,” ilisema taarifa hiyo ya Prof Caro.
Taarifa hiyo ilifafanua kwamba pamoja na maelezo ya maofisa wa ZIPA kwamba ujenzi huo utafanyika zaidi kwenye shamba la mpira la Vumawimbi, hakuna ramani wala maandishi yoyote yanayothibitisha jambo hilo zaidi ya maelezo ya mwekezaji.
Katika taarifa hiyo, Prof Caro ameonya kwamba ujenzi huo utaathiri mazingira ya viumbehai wakiwemo wadudu, mimea, wanyama na ndege ambao hawapatikani sehemu yoyote duniani jambo ambalo litapunguza utalii wa mazingira.
“Kwanza, hifadhi ya msitu huu ina aina nane za mimea ambayo ni ya kipekee katika sayansi ya utafiti na mpaka sasa haipatikani popote Afrika isipokuwa Ngezi,” ilisema ripoti hiyo.
Pamoja na mimea hiyo ya pekee, Msitu wa Hifadhi wa Ngezi una miti mirefu yenye umri wa miaka zaidi ya 100 pamoja na mnyama mdogo aina ya mbalawa wa blu ambaye hayupo popote hapa Afrika.
Wakati shughuli za kusafisha eneo la ujenzi zinaanza mwezi Septemba mwaka jana, wanaharakati wa mazingira, watafiti na wananchi walipinga mradi huo wakisema utaathiri shughuli zao za maendeleo.
“Ujenzi huu ndani ya Hifadhi ya Msitu wa Ngezi unatishia kuharibu mazingira na kuathiri viumbehai ambayo ndiyo kivutio kikuu cha watalii na chanzo cha mapato ya wananchi wengi hapa Konde,” alisema Abdurahman Mbaruk, katibu wa taasisi ya wanaharakati ya Ngezi Natural Resources Conservation Organization.
Mbaruk anasema ujenzi wa hoteli hiyo tayari unaathiri shughuli za uhifadhi na utalii katika msitu huo ambao watafiti wanasema una upekee katika Afrika.
Ameomba uongozi wa ZIPA kuwashirikisha wakazi wa eneo hilo katika uwekezaji huo ili kupata maoni yao namna ya kuboresha mradi huo kwa manufaa ya jamii ya eneo hilo ambayo baadhi yao ni waongoza watalii.
Mjumbe wa bodi ya Tanzania Forest Conservation Group, Thabit Masoud aliunga mkono hoja hiyo akisema mradi huo wa hoteli ya kitalii utazorotesha shughuli za uhifadhi na kuathiri maisha ya watu wa Konde ambao wengi wao ni wakulima na wavuvi.
“Tangu miaka ya tisini ujenzi wa hoteli za kitalii ndani ya msitu umepamba moto na manufaa yake kwa wananchi bado kuonekana, ni vyema sasa kuwepo kwa mazungumzo ambayo yataleta amani na maendeleo kwa wahusika wote,” alisema Masoud huku akishauri ZIPA kuhamishia mradi huo kwende eneo jingine.
“Mradi kama huu unahitaji kushirikisha wananchi ili kuleta manufaa kwani wawekezaji wakishajenga hoteli hawashirikiani na wananchi kama wanavoahidi kabla,” alisisitiza huku sha mradi huo ambao umekuwa kimya siku za karibuni baada ya wanaharakati kushinikiza uondoke eneo hilo.
Idara ya Misitu Kisiwani Pemba ilisema katika ripoti yake mwishoni mwa mwaka jana kwamba ujenzi wa ukuta huo umezuia shughuli za doria kwani umeziba njia za kupita askari wa idara hiyo na pia maafisa utalii.
Katika ripoti yake ya Desemba 18, 2025 ambayo ilipelekwa kwa Mkurugenzi wa Misitu - Wizara ya Kilimo, Umwagiliaji, Maliasili na Mifugo na nakala kwa Katibu Mtendaji wa ZIPA, idara hiyo ilisema kwamba mradi huo ulikiuka baadhi ya taratibu za uwekezaji za wizara.
“Hatupingi mradi huu kwani serikali inayo nia njema ya kukuza utalii ila ni vyema taratibu za wizara za uwekezaji katika eneo la hifadhi zifuatwe,” ilisema ripoti hiyo ambayo Katibu Mtendaji wa ZIPA, Saleh Saad Mohamed aliwahi kuikana.
“Mie sijaona ripoti hiyo ila naweza kusema kwamba hakuna tofauti kati yetu na Idara ya Misitu kuhusu mradi huo ambao ni mpango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kuendeleza utalii kisiwani Pemba,” alisema Mohamed.
Alisisitiza kwamba mradi huo una manufaa makubwa kwa uchumi wa Pemba na Zanzibar kwa ujumla kwani unaboresha miundombinu ya utalii ili kuongeza idadi ya watalii wanatembelea kisiwa hicho cha pili kwa ukubwa visiwani Zanzibar.
Hoja yake iliungwa mkono na mwakilishi wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar, Zawadi Amour Nassor ambaye alisema wakati Unguja inapokea watalii zaidi ya laki tano, Pemba inapata wasiozidi laki moja kwa mwaka.
“Moja ya tatizo kubwa ni ukosefu wa hoteli za kitalii kwa hiyo mradi huu unalenga kutatua changamoto hiyo,” alisema Nassor ambaye alipinga madai ya wananchi wa jimbo lake kwamba hawakushirikishwa katika kupitishia mradi huo.
“Wanaotoa madai hayo ni wale ambao hawaji kwenye mikutano tukiitisha kwani jambo hili tulijadili kwenye mikutano ya hadhara,” alisema mwakilishi huyo huku akiwataka wakazi hao kuunga mkono jitihada hizo za serikali.
Umebakiwa na makala 2 za bure mwezi huu. Jiunge ili kusoma bila kikomo.
- Msitu wa Ngezi
- Pemba
- Mazingira
- Utalii