Habari
Samia kuzindua JNHPP Agosti 22
RAIS Samia Suluhu Hassan anatarajiwa kuzindua rasmi Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP) chenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115.
Akizungumza na waandishi habari juzi jijini Dar es Salaam, Waziri wa Nishati, Deogratius Ndejembi amesema mkuu huyo wa nchi atazindua kituo hicho Agosti 22, 2026 katika eneo la mradi lililopo Rufiji, Mkoa wa Pwani.
Pamoja na mambo Ndejembi amesema uzinduzi huo pia utahudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali, wageni kutoka ndani na nje ya nchi, wananchi na wadau wa maendeleo.
“Uzinduzi huu wa mradi wa umeme wa Julius Nyerere ni tukio la kihistoria na hatua muhimu katika safari ya Tanzania ya kujenga mfumo wa nishati ya uhakika nchini, sambamba na kuchochea shughuli za uzalishaji, uwekezaji na ukuaji wa uchumi…”
“Huu ni mradi mkubwa zaidi wa kuzalisha umeme kuwahi kutekelezwa nchini kwa kutumia fedha za ndani za Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ukiwa na uwekezaji wa takribani Shilingi trilioni 7.452,”amesema Ndejembi.
Akifafanua kuhusu mradi huo, amesema JNHPP imeendelea kuongeza kiwango cha umeme kinachoingia katika Gridi ya Taifa na hivyo kusaidia kupunguza changamoto za upungufu wa uzalishaji zilizokuwa zikichangia mgao wa umeme nchini.
Ndejembi amesema hadi Mei 31, 2026, kituo hicho kilikuwa kimezalisha takribani asilimia 44.9 ya umeme wote uliozalishwa na kuingia katika Gridi ya Taifa katika kipindi cha mwaka mmoja.
“Hivyo kituo hicho kimekuwa kikichangia takribani nusu ya umeme wote unaotumika nchini Tanzania,”amesema waziri Ndejembi.
Waziri huyo amesema kuwa kwa sasa uwezo wa mitambo yote ya kuzalisha umeme nchini umefikia takribani megawati 4,648.
“Hivyo ongezeko la megawati 2,115 itakuwa ni kiwango kikubwa wa taifa kukidhi maSamia kuzindua JNHPP Agosti 22 hitaji ya umeme na kuimarisha usalama wa nishati,”amesema.
Ndejembi amesema mbali na uzalishaji wa umeme, mradi huo una uwezo wa kuchangia katika udhibiti wa mafuriko katika Bonde la Rufiji, kilimo cha umwagiliaji, utalii na upatikanaji wa maji kwa matumizi mbalimbali.
Aidha ametaja mradi wa kusafirisha umeme wa megwati 400 kutoka Chalinze kwenda Dodoma kuwa miongoni mwa miradi inayotekelezwa kuimarisha uwezo wa kusafirisha umeme.
Ujenzi wa mradi huo ulianza Juni 2019 na kukamilika Machi 2025.
Katika kipindi cha ujenzi huo takribani wafanyakazi 12,000 waliajiriwa huku asilimia 99 wakiwa Watanzania.
Bwawa lake lina uwezo wa kuhifadhi takribani mita za ujazo bilioni 33 za maji, sawa na karibu mara 10 ya uwezo wa Bwawa la Mtera.
- JNHPP
- Nishati
- Umeme
- Rufiji