Tahariri
Tanesco iwezeshwe kukamilisha furaha ya JNHPP
UZINDUZI rasmi wa Bwawa na Kituo cha Kuzalisha Umeme cha Julius Nyerere (JNHPP), uliofanywa na Rais Samia Suluhu Hassan Agosti 22, 2026, ni hatua ya kihistoria inayostahili pongezi kutoka kwa kila anayeitakia mema Tanzania.
Kimsingi, huu siyo ushindi wa serikali pekee, bali mafanikio ya taifa lililothubutu kutumia rasilimali zake kujenga msingi wa uchumi wa kisasa.
Kwa uwezo wa kuzalisha megawati 2,115 kupitia mitambo tisa, kila mmoja ukiwa na uwezo wa megawati 235, JNHPP ni mradi mkubwa kuliko yote ya uzalishaji umeme nchini na miongoni mwa miradi mikubwa ya kuzalisha umeme Afrika.
Umegharimu takribani Shilingi trilioni 7.452, fedha zilizotolewa na Serikali ya Tanzania, na umeongeza uwezo wa mitambo ya taifa kuzalisha umeme kufikia karibu megawati 4,075. Zaidi ya nusu ya uwezo huo sasa inatokana na JNHPP pekee.
Hata kabla ya kuzinduliwa rasmi na Rais Samia, matokeo yake tayari yanaonekana. Katika kipindi hadi Mei 31, 2026, kituo hiki kilichangia asilimia 44.9 ya umeme wote uliozalishwa na kuingizwa katika Gridi ya Taifa.
Hiyo ni hatua kubwa katika kuondoa historia ya mgao, kuipa sekta ya viwanda uhakika wa uzalishaji, kuvutia uwekezaji na kuwezesha huduma za afya, elimu, maji, mawasiliano pamoja na biashara ndogo zinazotegemewa na mamilioni ya Watanzania.
Sisi Pambazuko tunahimiza kuwa shangwe za uzinduzi zisifanye tusahau ukweli mmoja; kuzalisha umeme mwingi ni nusu tu ya kazi. Umeme hauna faida ukiishia kwenye mitambo ya Rufiji, unapotea njiani au hauwafikii wananchi na wawekezaji kwa ubora unaotakiwa.
Sasa ni wakati wa kuhamisha nguvu ya kitaifa kutoka kwenye uzalishaji kwenda kwenye usafirishaji na usambazaji.
Takwimu za Mamlaka ya Udhibii wa Nishati (Ewura) zinaonyesha kuwa hadi Juni 2025, Tanzania ilikuwa na kilomita 8,303.87 za njia za kusafirisha umeme na vituo 72 vya Gridi ya Taifa.
Mtandao wa usambazaji unaomilikiwa na Tanesco ulikuwa na zaidi ya kilomita 213,278, lakini katika mwaka wa fedha 2024/25, shirika hilo la kusambaza umeme lilipoteza asilimia 13.86 ya nishati katika mifumo ya usafirishaji na usambazaji.
Hata kama baadhi ya viwango hivyo vilikuwa ndani ya malengo ya udhibiti, kupoteza sehemu hiyo ya umeme unaozalishwa kwa gharama kubwa siyo jambo la kupuuzwa.
Tunaitaka serikali kuiwezesha Tanesco kifedha na kitaalamu kubadilisha transfoma zilizochakaa, kuongeza njia za msongo mkubwa, kujenga vituo vipya, kuweka mifumo janja ya kupima na kufuatilia umeme, na kufanya matengenezo kabla ya hitilafu.
Uwekezaji huo uende sambamba na uwazi katika ununuzi, usimamizi wa kitaalamu, uwajibikaji wa watendaji na huduma bora kwa wateja.
Pia, umeme huu utumike kuchochea viwanda, kilimo cha umwagiliaji, uchakataji wa mazao, uchimbaji madini na uchumi wa kidijitali.
Wananchi wa vijijini na pembezoni wasiishie kusikia idadi ya megawati; waone umeme wa uhakika majumbani, shuleni, vituo vya afya na kwenye shughuli za uzalishaji.
Aidha, Tanesco ipewe uwezo wa kusawazisha uzalishaji na mahitaji, kujenga hifadhi za nishati na kuunganisha vyanzo vingine vya gesi, jua na upepo.
Pambazuko tunaamini kuwa JNHPP ni nguzo kuu, lakini usalama wa nishati unahitaji mfumo unaohimili ukame, mafuriko na hitilafu kubwa.
JNHPP ni fahari ya Tanzania, lakini kipimo chake cha mwisho hakitakuwa ukubwa wa bwawa wala gharama ya ujenzi, bali kitakuwa viwanda vinavyofunguliwa, ajira zinazozaliwa, biashara zinazokua, Ankara ambazo wananchi wanazimudu na kukoma kwa kukatika umeme.
Baada ya uzinduzi, kazi kubwa sasa ni kuhakikisha kila megawati inafika inapohitajika na kubadilisha maisha ya Watanzania na wawekezaji.
- JNHPP
- Tanesco
- Nishati