Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Hoja Yangu

Faida za JNHPP zipige hodi majumbani

KUKAMILIKA kwa Mradi wa Kufua Umeme wa Julius Nyerere (JNHPP), unaofahamika pia kama Stiegler’s Gorge, ni hatua kubwa katika historia ya nishati Tanzania.

Jumatatu, 24 Agosti 2026 · 06:00Dakika 2 kusomaToleo 179, uk. 27
Faida za JNHPP
Faida za JNHPP — Picha na Maktaba

Mradi huo wenye uwezo wa kuzalisha megawati 2,115 umejengwa kwa gharama ya takribani Shilingi trilioni 7.45, ukiwa miongoni mwa uwekezaji mkubwa zaidi wa miundombinu nchini.

Lakini baada ya miaka ya ujenzi na matumizi makubwa ya fedha za umma, swali la msingi sasa siyo tena kama mradi umejengwa. Swali ni utaleta faida gani katika maisha ya Mtanzania?

Kwa uwezo wa megawati 2,115 na makadirio ya kuzalisha takribani gigawati-saa 5,920 kwa mwaka, JNHPP ina uwezo wa kubadilisha sura ya sekta ya umeme na uchumi kwa ujumla.

Mradi ulianza kuingiza umeme kwenye gridi kwa awamu mwaka 2024, ukiwemo mchango wa awali wa megawati 235.

Hii ni nafasi ambayo Tanzania haipaswi kuiacha ipite. Umeme mwingi na wa uhakika unatakiwa kuwa kichocheo cha viwanda, kilimo cha umwagiliaji, biashara, huduma za kidijitali na ajira.

Hoja Yangu hapa ni serikali inapaswa kuhakikisha kwamba umeme huu hauishii kwenye takwimu za mafanikio, bali unaonekana kwenye uzalishaji wa bidhaa na huduma.

Takwimu za Benki ya Dunia zinaonyesha kuwa mwaka 2023 ni asilimia 48.3 tu ya Watanzania waliokuwa na upatikanaji wa umeme.

Hii ina maana kuwa, licha ya uwekezaji mkubwa katika uzalishaji, bado kuna kazi kubwa ya kupeleka umeme kwa wananchi.

Kwa maana hiyo, hatua inayofuata inapaswa kuwa kuongeza kasi ya usambazaji.

Umeme wa JNHPP ukifika vijijini, unaweza kubadilisha maisha kwa kuwezesha mashine za kusaga na kukoboa, viwanda vidogo, vituo vya kuhifadhi mazao, visima vya maji saloon za vijana na huduma za afya na elimu.

Benki ya Dunia tayari imeonesha mifano ya maeneo ambako upatikanaji wa umeme umewezesha biashara ndogo na viwanda kukua, huku uzalishaji wa mpunga na mafuta ya alizeti ukiongezeka na gharama za usafirishaji kupungua.

Ndiyo maana Serikali inapaswa kuwa na mpango mahsusi wa kuhakikisha umeme huu unazalisha thamani ya kiuchumi.

Viwanda vipya vinapaswa kuvutiwa, vilivyopo viwezeshwe kupanua uzalishaji, na wawekezaji wa ndani wahamasishwe kutumia fursa ya nishati ya uhakika.

Vilevile, wananchi wanahitaji kuona uwazi kuhusu gharama za mradi, mapato yanayotarajiwa na namna uwekezaji huo utakavyorejesha thamani kwa Taifa.

Kwa hiyo, mafanikio ya Stiegler’s Gorge hayatapimwa kwa ukubwa wa bwawa wala idadi ya megawati pekee.

Yatapimwa kwa viwanda vingapi vitaongezeka, ajira ngapi zitazalishwa, uzalishaji utakua kwa kiasi gani na maisha ya wananchi yatabadilika kwa kiwango gani.

Sasa ni wakati wa kugeuza megawati kuwa maendeleo. Hapo ndipo Stiegler’s Gorge itakapothibitisha kuwa siyo tu mradi mkubwa wa umeme, bali ni uwekezaji mkubwa katika maisha ya Mtanzania.

Rashid Mtagaluka ni mwandishi wa habari na anapatikana kwa simu nambari na email; mtagaluka@gmail.com

  • JNHPP
  • Nishati

Soma Pia