Habari
Serikali yajenga ghala Nzega kuhifadhi tani 10,000
Nchi kuwa na uhakika wa chakula ni jambo muhimu katika ustawi wa wananchi wake na ndivyo Tanzania imejizatiti kuwa na hifadhi ya kutosha kama mikakati inavyothibitika kwa ujenzi wa ghala kubwa huko Nzega.

WAKALA wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Kanda ya Shinyanga, unaendelea na ujenzi wa ghala kubwa la kisasa la kuhifadhi nafaka katika Kijiji cha Itilo, Wilaya ya Nzega, Tabora.
Hatua hii ni sehemu ya mkakati wa kuongeza uwezo wa kuhifadhi chakula na kupunguza gharama ambazo zimekuwa kubwa kwa kukodi sehemu za kutunzia.
Ghala hilo litakapokamilika mwezi ujao; Desemba, 2026 litakuwa na uwezo wa kuhifadhi tani 10,000 za nafaka, hatua inayotarajiwa kuongeza nafasi ya kuhifadhi mazao yanayonunuliwa kutoka kwa wakulima, hasa katika Mkoa wa Tabora ambao ni miongoni mwa maeneo muhimu yanayozalisha mpunga nchini.
Meneja wa NFRA Kanda ya Shinyanga, Dickson Nyika, amesema uamuzi wa kujenga ghala hilo umetokana na uhitaji wa kuongeza uwezo wa kuhifadhi nafaka katika mkoa huo, kutokana na uwezo mdogo wa maghala yaliyokuwepo awali ikilinganishwa na mahitaji ya wakala.
Akizungumza kuhusu maendeleo ya mradi huo, Nyika amesema NFRA imeona umuhimu wa kuwekeza katika miundombinu yake yenyewe ili kupunguza gharama zinazotumika kukodisha maghala kutoka kwa watu binafsi na taasisi nyingine, hususan katika maeneo ya Igunga na Bukene.
Amesema kukamilika kwa ghala hilo kutakuwa na manufaa makubwa kwa wakala na wananchi kwa ujumla, kwa kuwa kutasaidia kuongeza nafasi ya kuhifadhi nafaka zinazozalishwa na kununuliwa katika maeneo hayo, huku kukirahisisha usimamizi na usambazaji wa chakula pale kinapohitajika.
Nyika amesema NFRA - Kanda ya Shinyanga inasimamia mikoa minane; Shinyanga, Tabora, Simiyu, Mara, Kagera, Geita, Mwanza na Kigoma, huku makao makuu ya kanda hiyo yakiwa katika Shinyanga.
Amefafanua kuwa katika mikoa hiyo wakala una miundombinu ya kuhifadhi nafaka, ambapo mazao makuu yanayohifadhiwa ni mahindi na mpunga, huku sehemu kubwa ya mpunga unaopatikana katika hifadhi hizo ukitoka Mkoa wa Tabora.
Amesema katika Mkoa wa Shinyanga, ambako ndiko yalipo makao makuu ya kanda hiyo, kuna ghala moja lenye uwezo wa kuhifadhi tani 10,000 za nafaka na ghala jingine maalumu kwa ajili ya kuhifadhi mpunga lenye uwezo wa tani 3,500.
Kwa upande wa Mkoa wa Simiyu, alisema kuna ghala moja lenye uwezo wa kuhifadhi tani 1,500, huku Mkoa wa Kigoma ukiwa na maghala mawili yaliyopo katika Wilaya za Kibondo na Kasulu, ambayo kila moja lina uwezo wa kuhifadhi tani 1,500.
Mkoa wa Mara una ghala lenye uwezo wa kuhifadhi tani 3,500, huku Mkoa wa Tabora, licha ya kuwa miongoni mwa maeneo muhimu ya uzalishaji wa mpunga, ulikuwa na ghala moja pekee lenye uwezo wa kuhifadhi tani 1,500 lililopo Wilaya ya Nzega.
Nyika amesema hali hiyo imekuwa ikisababisha changamoto ya nafasi ya kuhifadhi nafaka katika Mkoa wa Tabora, jambo lililofanya NFRA kutumia gharama zaidi kukodisha maghala ili kukidhi mahitaji ya uhifadhi.
Amefafanua kuwa kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo, NFRA imepata eneo lenye ukubwa wa ekari 22, ambalo litatoa nafasi ya kutosha kwa shughuli za sasa na mipango mingine ya kuongeza miundombinu ya kuhifadhi nafaka baadaye.
Katika hatua nyingine, Nyika amesema eneo hilo lenye ukubwa wa ekari 22 lina nafasi ya kutosha kwa ajili ya mipango ya baadaye ya kuongeza miundombinu ya kuhifadhi nafaka, ikiwamo ujenzi wa vihenge maalumu vitakavyosaidia kuhifadhi mazao kwa muda mrefu.
Amesema mpango wa kuongeza vihenge ni muhimu kwa kuwa utasaidia kuhifadhi nafaka kwa kipindi cha hadi miaka mitano bila kupoteza ubora wake, endapo zitahifadhiwa kwa kuzingatia taratibu na viwango vinavyotakiwa.
Nyika amefafanua kuwa uwepo wa miundombinu hiyo utaongeza uwezo wa NFRA kuhifadhi akiba kubwa ya chakula, kupunguza upotevu wa mazao na kuhakikisha nafaka zinazokusanywa kutoka kwa wakulima zinabaki katika hali nzuri kwa matumizi ya baadaye.
Amesema kwa mujibu wa ratiba ya utekelezaji, ujenzi wa ghala hilo unatarajiwa kukamilika Desemba 2026 na kuanza kutumika Januari 2027.
Nyika ameeleza kuwa uwepo wa ghala hilo pia utasaidia kurahisisha upatikanaji wa chakula kwa wananchi wa Tabora na maeneo jirani wakati wa mahitaji, badala ya kutegemea kwa kiwango kikubwa nafaka zinazosafirishwa kutoka katika mikoa mingine.
Amebainisha kuwa endapo kutatokea uhaba wa chakula katika Mkoa wa Tabora, itakuwa rahisi kwa NFRA kutumia akiba iliyohifadhiwa katika ghala la Itilo kuwahudumia wananchi, bila kulazimika kusafirisha chakula kutoka maeneo ya mbali kama Shinyanga au Musoma.
Amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza muda na gharama za usafirishaji, huku ikiongeza ufanisi wa utoaji wa chakula kwa wananchi wanaokihitaji.
Nyika amesisitiza kuwa uwekezaji katika maghala ya kuhifadhi nafaka ni muhimu katika kuhakikisha mazao yanayozalishwa na wakulima yanapata sehemu salama ya kuhifadhiwa na kuwa sehemu ya akiba ya taifa inayoweza kutumika wakati wa dharura.
Amesema NFRA itaendelea kuimarisha miundombinu yake katika maeneo mbalimbali nchini ili kuongeza uwezo wa kuhifadhi chakula na kutekeleza jukumu lake la kuhakikisha taifa linakuwa na akiba ya kutosha kukabiliana na changamoto zinazoweza kujitokeza katika sekta ya chakula.
Ujenzi wa ghala ukiendelea.
- NFRA
- Nzega
- Hifadhi
- Chakula