Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Habari

Wakulima wa mahindi wagomea bei ya serikali

WAKULIMA wa mahindi katika maeneo mbalimbali nchini wamekataa kuuza zao hilo kwa bei elekezi iliyotangazwa na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) ya Shilingi 450 kwa kilo.

Jumatatu, 21 Septemba 2026 · 06:00Dakika 2 kusomaToleo 183, uk. 17

Wakizungumza na Pambazuko kwa nyakati tofauti, wakulima hao wamesema ni heri wakae na mahindi yao nyumbani kuliko kuyauza kwa bei hiyo wakisema ni ndogo mno na inawaumiza na kuwapatia hasara kubwa.

Septemba 9, 2026 NFRA ilitangaza rasmi kununua mahindi kwa bei ya Shilingi 450 kwa kilo moja kwa ajili ya msimu wa ununuzi wa 2026/2027.

Tangazo hilo lilitolewa na Meneja wa NFRA Kanda ya Makambako, Revocatus Bisama, wakati wa vikao na viongozi na wakulima katika Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe.

Wakulima wengi katika mikoa inayozalisha mahindi kwa wingi ikiwamo Songwe, Ruvuma na Njombe wamegoma kuuza mahindi yao kwa NFRA kwa bei hiyo ya Shilingi 450 kwa kilo, sawa na Shilingi 45,000 kwa gunia la kilo 100.

Wakulima hao wanalalamika kuwa bei hiyo ni ndogo mno na kwamba haiendani na gharama kubwa za uzalishaji wanazozitumia kuzalisha zao hilo.

Hali hiyo inajitokeza pamoja na kwamba wafanyabiashara binafsi wananunua zao hilo kwa bei ya chini zaidi. Katika baadhi ya maeneo wafanyabiashara hao wananunua mahindi kwa kati ya Shilingi 250 na 300 kwa kilo.

Pambazuko limebaini kushuka zaidi kwa bei ya zao hili katika maeneo ya Kiteto na Songea, ambapo yanauzwa hadi Shilingi 32,000 kwa gunia, huku Songwe, Katavi, Rukwa, Dodoma na Arusha bei zikiwa chini ya Shilingi 45,000 kwa gunia.

Mkulima kutoka Katavi, Elias Mwasyoka, ameliambia Pambazuko kuwa kuuza kilo moja kwa Shilingi 450 ni hasara kubwa kwao.

“Hapana, hii si sawa, ni unyonyaji. Acha tukae na mahindi yetu kuliko kuuza kwa bei hiyo ya hasara.

Tunajiuliza ni kwa nini katika nchi hii wakuma tumekuwa tukionewa hivi,” amelalamika.

Mkulima mwingine kutoka Mbeya ambaye hakutaka jina lake kutajwa gazetini, amesema kuuza gunia moja kwa kati ya Shilingi 36,000 na Shilingi 38,000 ni hasara kutokana na gharama kubwa za uzalishaji ikiwemo mbolea ya kupandia iliyogharimu Shilingi 95,000, mbolea ya kukuzia Shilingi 80,000 na mbegu bora hadi Shilingi 100,000.

Gharama za pembejeo kama mbolea ya kupandia (DAP) inayofikia kati ya Shilingi 95,000 na 96,000 kwa mfuko na gharama za mbegu zinamfanya mkulima kupata hasara kubwa akiuza mahindi yake kwa bei elekezi ya NFRA.

Serikali kupitia Mkurugenzi Mkuu wa NFRA, Dkt. Andrew Komba, imekiri kuwepo kwa upinzani huo kutoka kwa wakulima wa baadhi ya maeneo ya vijijini.

Aidha, Dkt. Komba alisisitiza kuwa NFRA inafanya ununuzi huo kama afueni kwani wafanyabiashara binafsi (walanguzi) kwa sasa wananunua mahindi kwa bei ya chini zaidi, kati ya Shilingi 250 hadi 300 kwa kilo katika maeneo mengi.

Amesema NFRA inaendelea kununua mahindi kwenye maeneo ambayo tayari wamekubaliana na bei hiyo.

Amesema NFRA inalenga kununua jumla ya tani milioni 1.2 za nafaka nchi nzima kwa msimu huu kutokana na mavuno makubwa.

Kwa mwaka wa fedha 2025/26, NFRA ilinunua mahindi kwa wakulima kwa bei ya Shilingi 700 kwa kilo.

Baadaye ukaibuka mjadala bungeni ambapo wabunge walipendekeza bei ya mahindi kuwa Shilingi 800.

Baada ya mjadala huo, Wizara ya Kilimo iliripoti kuwa bei elekezi ya mahindi ilikuwa Shilingi 800 kwa kilo katika kipindi hicho.

  • Kilimo
  • Mahindi
  • NFRA
  • Bei
  • Wakulima

Soma Pia

Wakulima wa mahindi wagomea bei ya serikali | Pambazuko