Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Kilinge cha Mawasiliano

Kuonekana siyo sawa na kuaminika

KUNA jaribio dogo ninalotumia kila ninapokutana na mteja mpya. Namuuliza ataje jambo moja ambalo taasisi yake imewahi kukubali hadharani kuwa ilikosea katika miaka miwili iliyopita.

Jumatatu, 17 Agosti 2026 · 13:15Dakika 2 kusomaToleo 178, uk. 24
Loth Makuza
Loth Makuza — Kutoka Maktaba ya Pambazuko

Wengi hukaa kimya na wengine hucheka kwa woga na wapo wanaosisitiza kuwa hakuna kitu chochote.

Ukimya huo unaniambia zaidi kuhusu hali halisi ya taasisi mbele ya jamii kuliko ripoti yoyote ya takwimu za mitandao inavyoweza kuniambia, kwa sababu taasisi ambayo haijawahi kukosea hadharani kwa kawaida ni ile ambayo haijawahi kuwa ya kweli hadharani pia.

Jaribio hilo dogo linaashiria jambo kubwa zaidi. Taasisi inaweza kuonekana kila mahali, lakini bado ikatiliwa shaka, inaweza kutawala kila jukwaa la mitandao lakini ikapoteza heshima chumbani.

Kuonekana na kuaminika siyo ndugu. Kimoja ni kuhusu kuonekana. Kingine ni kuhusu kuaminiwa.

Kwa zaidi ya muongo mmoja nikifanya kazi katika Uhusiano na Umma na Mawasiliano ya kimkakati, nimeshuhudia taasisi zikimwaga fedha nyingi katika kampeni, mabadiliko ya chapa, na ‘kelele za kidijitali, ’ kisha zikashuhudia uaminifu ukitoweka polepole mlangoni wa nyuma bila wao kutambua.

Mazingira ya kidijitali yanasonga mbele kwa kasi kuliko uwezo wa kuthibitisha ukweli. Watu hawasubiri tena uthibitisho kabla ya kuunda maoni yao, huunda maoni kwanza, kisha hutafuta uthibitisho baadaye.

Kwa hiyo swali la msingi linalowakabili viongozi leo siyo “tufanyeje ili tuonekane zaidi?”

bali ni; “tunawezeje kuendelea kuaminika wakati kila mtu mwingine anazidi kupaza sauti?”

Mambo matano yanatofautisha taasisi zinazoweza kufanikisha hili na zile zisizoweza.

Kwanza, mawasiliano lazima yasikike kibinadamu, jamii imejenga uwezo wa kutambua lugha za kishirika zinazolenga kumkinga msemaji badala ya kumjulisha msikilizaji.

Na Loth MAKUZA Pili, kile taasisi inachosema na kile inachofanya lazima viwiane. Wataalamu wa mawasiliano huita pengo kati ya hivyo viwili “pengo la kusema na kutenda,” na katika enzi hii ya kidijitali pengo hilo hujifunga lenyewe hata kama viongozi hawataki.

Utafiti maarufu wa kimataifa wa Edelman Trust Barometer, unaohusisha karibu watu 34,000 katika nchi 28 kila mwaka, unaonyesha kwamba watu wanamwamini mwajiri wao zaidi kuliko wanavyoiamini biashara kwa ujumla au serikali.

Tatu, kasi si hiari tena, zamani ukimya ulinunua muda, sasa unanunua mashaka.

Wachambuzi wanaofuatilia majibu ya migogoro wamegundua kwamba taasisi zinazojibu ndani ya saa moja ya kwanza huhifadhi uaminifu mkubwa zaidi wa umma kuliko zile zinazosubiri hata siku moja tu, na migogoro isiyoshughulikiwa vizuri inaweza kuathiri thamani ya soko karibu papo hapo.

Taasisi zinazopita salama katika wakati mgumu si zile zenye kauli za akili sana, ni zile zilizojitokeza kwanza, kabla mtu mwingine hajaandika hadithi kwa niaba yao.

Nne, mawasiliano yanahitaji nafasi mezani, si kiti karibu na mlango. Kuchukulia Uhusiano na Umma kama pambo badala ya mkakati ni miongoni mwa makosa ya gharama kubwa zaidi ambayo timu ya uongozi inaweza kufanya.

Tano, teknolojia inapaswa kuhudumia uaminifu, si kuubadilisha. Otomatiki na akili bandia ni muhimu kweli katika kufuatilia mazungumzo na kubaini matatizo mapema.

Taasisi ambazo zitaendelea kusimama, na kuaminiwa, miaka mitano ijayo hazitakuwa lazima zile zenye sauti kubwa zaidi chumbani.

Zitakuwa zile zilizogundua mapema kwamba kuonekana ni rahisi, lakini kuaminiwa lazima kupatikane upya kila siku.

Mwandishi wa safu hii ni mtaalamu wa Uhusiano na Umma (PR). Anapatikana kwa namba: na kupitia email; projects@ lothmakuza.co.tz.

  • Uhusiano na Umma
  • Uaminifu

Soma Pia