Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Habari

Tanzania yataka mfumo mpya migogoro uwekezaji

Wakati Tanzania ikifanya mageuzi makubwa kuvutia mitaji ya ndani na nje, serikali imeibua mjadala kuhusu upande mwingine wa uwekezaji ambao hauzungumzwi sana; mashauri ya wawekezaji dhidi ya serikali, gharama zake na hatari ya nchi kulipa fidia kubwa zinazotokana hata na makadirio ya faida ambazo mwekezaji alitarajia kupata miaka ijayo.

Jumatatu, 21 Septemba 2026 · 06:00Dakika 2 kusomaToleo 183, uk. 28

TANZANIA imeungana na nchi nyingine zinazoendelea kushinikiza mageuzi ya mfumo wa kimataifa wa kutatua migogoro baina ya wawekezaji na serikali.

Inataja baadhi ya mambo ya kufanyiwa marekebisho makubwa kuwa ni pamoja na fidia kubwa, gharama za mashauri na madai yanayojengwa juu ya makadirio ya faida za baadaye kuwa miongoni mwa maeneo yanayohitaji kuangaliwa upya.

Msimamo huo umejitokeza wakati Tanzania ikiwa katika hatua ya kupitia upya sheria, sera na mifumo yake ya uwekezaji ili kuvutia mitaji zaidi, lakini wakati huohuo kuhakikisha uwekezaji unaingia nchini unazalisha ajira, ujuzi na ongezeko la thamani ndani ya uchumi.

Kaimu Mkurugenzi Msaidizi katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Felista Lelo, alisema nchi zinazoendelea zinakabiliwa na changamoto mbalimbali chini ya mfumo wa Investor-State Dispute Settlement (ISDS), unaowezesha wawekezaji wa kigeni katika mazingira yanayoruhusiwa na mikataba husika kuwasilisha madai dhidi ya serikali.

Akiwasilisha mada katika Mkutano wa 17 wa Sera za Uwekezaji (Investment Policy Forum—IPF) uliofanyika Dar es Salaam kuanzia Septemba 16 hadi 18, Lelo alitaja miongoni mwa changamoto hizo kuwa ni ukubwa wa baadhi ya fidia zinazotolewa na mabaraza ya usuluhishi, gharama na muda wa mashauri pamoja na ufadhili wa kesi na watu wengine wasio wahusika wa moja kwa moja katika mgogoro.

Hoja nyingine ni matumizi ya makadirio ya faida ambazo mwekezaji anadai angezipata katika siku zijazo katika kukokotoa baadhi ya madai ya fidia.

Kwa mtazamo wa Tanzania, hoja hizo zinaweka mezani swali pana zaidi; nchi inaweza kulinda vipi wawekezaji bila kujifunga mikono inapohitaji kubadili sheria au sera kwa maslahi ya wananchi?

Lelo alisisitiza umuhimu wa kuwa na mfumo wa utatuzi wa migogoro unaozingatia mazingira ya kisheria na kisera ya nchi husika.

Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali iliwakilishwa katika mkutano huo na Lelo pamoja na Wakili wa Serikali, Mwita Chacha.

Mjadala mkubwa kuliko Tanzania Mkutano wa Dar es Salaam ulikuwa na umuhimu wa pekee, kwani kwa mujibu wa Taasisi ya Kimataifa ya Maendeleo Endelevu (IISD), uliwakutanisha takribani watunga sera 100 kutoka zaidi ya nchi na mashirika 40 kutoka Afrika, Asia, Amerika Kusini na Caribbean.

Jukwaa hilo lilianzishwa mwaka 2007 na limekuwa likitumika na nchi zinazoendelea kubadilishana uzoefu kuhusu mikataba ya uwekezaji, sheria, migogoro na namna ya kuhakikisha uwekezaji wa kimataifa unaendana na malengo ya maendeleo endelevu.

IISD inalielezea kama jukwaa pekee la aina yake linalowakutanisha watunga sera na wajadiliano wa masuala ya uwekezaji kutoka nchi zinazoendelea na uchumi unaoibukia.

  • Uwekezaji
  • Sheria
  • ISDS
  • Biashara

Soma Pia

Tanzania yataka mfumo mpya migogoro uwekezaji | Pambazuko