Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Habari

Profesa Saffari asifu sheria kuandikwa Kiswahili

Hatua ya Tanzania kuamua sheria na hukumu zote kutolewa kwa Kiswahili kunatajwa kuwa njia bora ya kufikia mfumo wa haki wenye kuthaminiwa zaidi.

Alhamisi, 17 Septemba 2026 · 12:07Dakika 2 kusomaToleo 182, uk. 13
Mwanasheria nguli na mtunzi wa vitabu, Profesa Abdallah Saffari, akizungumza katika mahojiano maalum na mhariri wa habari wa gazeti hili, Arodia Peter ofisini kwake jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.
Mwanasheria nguli na mtunzi wa vitabu, Profesa Abdallah Saffari, akizungumza katika mahojiano maalum na mhariri wa habari wa gazeti hili, Arodia Peter ofisini kwake jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. — Na Mpigapicha Wetu

NGULI wa sheria nchini, Profesa Abdallah Saffari amesifu hatua ya serikali kukubali kuandika sheria zote kwa Kiswahili, akisema kuwa ni moja ya mapinduzi makubwa ya mfumo wa haki nchini.

Mbali na hilo, ameshauri Tanzania iwe na mahakama ya juu zaidi – ya upeo (suprime court) badala ya mashauri kuishia kwenye ngazi ya mahakama ya rufani pekee.

Akizungumza na Pambazuko mwishoni mwa wiki, Profesa Saffari amesema mahakama ya upeo inatoa haki zaidi, kwani mtu akitiwa hatiani katika mahakama za chini ana uwezo wa kuendelea kutafuta haki yake mpaka kwenye mahakama hiyo.

“Tanzania ni pekee Afrika ambayo haina supreme court (mahakama ya upeo), nafikiri ni serikali kuamua suala hilo muhimu linaloongeza wigo wa utoaji haki nchini,” amesema Profesa Saffari.

Kuhusu umuhimu wa matumizi ya Kiswahili katika sheria za Tanzania, amesema yeye ni miongoni mwa wajumbe wa kikosi kilichofanya kazi za kubadilisha sheria kutoka kwenye Kiingereza kwenda Kiswahili na kwamba huenda mwakani kazi hiyo itakuwa imekamilika rasmi.

Profesa Saffari ambaye ni mtaalam na mtunzi wa vitabu vya Kiswahili, amesema moja ya maandiko yake ya kisheria aliwahi kushauri Kiswahili kitumike rasmi kuwa lugha ya mahakama, jambo ambalo anasema linakwenda kutimia hivi karibuni.

Amesema ndoto yake ni kuona wigo wa haki unaongezeka na kwamba matumizi ya Kiswahili yatafanya wengi kufuatilia na kuelewa mwenendo mzima wa haki.

Mwanasheria nguli na mtunzi wa vitabu, Profesa Abdallah Saffari, akizungumza katika mahojiano maalum na mhariri wa habari wa gazeti hili, Arodia Peter ofisini kwake jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki. (Picha na Mpigapicha Wetu).

Baadhi ya vitabu vyake vinaendelea kutumiwa kwenye shule za sekondari, sheria na vyuo vikuu mbalimbali hususani kwenye rejea ya fasihi. Vitabu hivyo ni pamoja na harusi, joka la mdimu, mashtaka ya jinai na utetezi na vingine kikiwamo haja ya kuwa na tume huru ya Taifa ya uchaguzi Tanzania alichokiandika mwaka 2010.

Aidha, Profesa Saffari ameshauri matumizi ya Kiswahili yawekwe rasmi kwenye Katiba ya nchi kama walivyofanya Kenya ingawa kwao siyo lugha rasmi inayotumika kila mahali kama ilivyo Tanzania.

“Kwa nini Kenya inaonekana wako mbele kwenye Kiswahili wakati wao vyombo vya habari zikiwamo televisheni, karibu vyote, bungeni na kila mahali wanatumia Kiingereza, ingawa kisheria kwa maana ya Katiba yao inaonyesha Kiswahili kimetambuliwa rasmi.

“Kuna mtu mmoja amewahi kuniuliza swali kwamba kati ya sheria na Kiswahili unapenda zaidi nini, sikusita, nilimjibu moja kwa moja mimi napenda sana lugha ya Kiswahili, ninapokaa na magwiji tunafanya uchambuzi wa hili na lile kuhusu Kiswahili, naona raha sana na nikiwa na magwiji kama akina Andanenga, watunzi wa mashairi, mimi najifunza zaidi na kupata mambo ya ziada kuhusu lugha hiyo adhimu,”

amesema.

  • sheria
  • haki
  • kiswahili
  • tanzania

Soma Pia