Bustani ya Sheria
Ukitaka kununua ardhi, zingatia haya
UNUNUZI wa ardhi ya kijiji siyo jambo la kukabidhiana fedha na kusainiana mkataba wa kawaida.
Ardhi ya kijiji inasimamiwa kwa utaratibu maalumu chini ya Sheria ya Ardhi ya Vijiji, Sura ya 114, na kutofuata utaratibu huo kunaweza kusababisha mgogoro au kuathiri uhalali wa haki inayodaiwa kupatikana.
Kwa mtu anayetaka kupata ardhi ya kijiji, hatua ya kwanza ni kuhakikisha maombi yanafanywa kwa utaratibu unaotambuliwa na sheria.
Maombi ya haki ya kimila ya kumiliki ardhi (Customary Right of Occupancy) hufanywa kwa fomu iliyowekwa na sheria na kusainiwa na mwombaji au wawakilishi wanaotambulika, kutegemea kama ni mtu binafsi, familia, kikundi au taasisi.
Kwa mtu au kikundi ambacho siyo wakazi wa kawaida wa kijiji husika, sheria inaweka pia masharti maalumu ya utambulisho na wadhamini kutoka kijijini.
Hivyo, siyo salama kununua ardhi kwa makubaliano ya mtu binafsi bila kuthibitisha kwanza hadhi ya ardhi na mamlaka ya anayeiuza.
Hatua nyingine muhimu ni kuhusisha Halmashauri ya Kijiji na, pale sheria inapohitaji, Mkutano wa Kijiji.
Sheria inaweka madaraka na muda tofauti kulingana na aina na ukubwa wa haki inayotafutwa. Kwa mfano, maombi ya baadhi ya lease yanayozidi hekta tano lakini chini ya thelathini yanahitaji uthibitisho wa Mkutano wa Kijiji, huku yanayozidi hekta thelathini au yenye muda mrefu zaidi yakihitaji taratibu za ziada pamoja na ushauri wa Kamishna wa Ardhi.
Kwa hiyo, mnunuzi anatakiwa kufanya uhakiki wa ardhi kabla ya kulipa fedha: kuthibitisha mipaka ya eneo, aina ya haki iliyopo, matumizi yaliyopangwa, kumbukumbu za kijiji na mamlaka ya muuzaji.
Pia ni muhimu kuhakikisha kama kuna watu wengine wenye maslahi au madai juu ya eneo hilo.
Kwa wawekezaji wanaohitaji kupata ardhi ya kijiji kwa miradi mikubwa, utaratibu unaweza kuwa tofauti zaidi na kuhusisha mamlaka za wilaya, Wizara ya Ardhi na taratibu za uwekezaji.
Somo: Usinunue ardhi ya kijiji kwa kuamini mkataba wa kawaida pekee. Hakikisha kwanza ardhi hiyo imetambuliwa, muuzaji ana haki ya kuhamisha au kuuza anachodai kumiliki, na taratibu zote zinazotakiwa na sheria zimefuatwa.
Katika masuala ya ardhi, utaratibu ni sehemu ya ulinzi wa haki yako.
Mwandishi ni Mwanasheria na Mchambuzi wa Sheria kutoka KGM Attorneys.
- Ardhi
- Sheria
- Vijiji
- Uwekezaji