Habari
TBS yawekeza mabilioni kupanua huduma za viwango
Miundombinu mipya, maabara za kisasa na maelfu ya vyeti vya ubora vilivyotolewa na TBS vyalenga kuongeza ushindani wa bidhaa za ndani, kulinda walaji na kurahisisha biashara.
Sahihisho · Jumanne, 27 Oktoba 2026
positioning of the story

SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limepanua uwekezaji katika miundombinu, teknolojia na huduma za uthibitishaji ubora katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita, hatua inayolenga kuimarisha usalama wa bidhaa sokoni na kuongeza uwezo wa wazalishaji wa ndani kushindana katika masoko ya ndani na nje ya nchi.
Mafanikio hayo yaliwasilishwa na Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dkt. Ashura Katunzi, katika mkutano na wahariri na waandishi wa habari ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina jijini Dar es Salaam.
Kwa mujibu wa Dkt. Katunzi, uwekezaji wa shirika katika kipindi cha mwaka 2021 hadi 2026 umejikita katika kupanua huduma za viwango, kuongeza uwezo wa maabara, kuboresha mifumo ya kidijitali na kuimarisha udhibiti wa bidhaa zinazoingia nchini.
“Hatua hizo zina umuhimu wa kiuchumi kwa sababu viwango vya ubora ni sehemu muhimu ya mazingira ya biashara. Vinasaidia kupunguza hatari za bidhaa zisizokidhi matakwa ya usalama, kuongeza imani ya walaji na kuwapa wazalishaji fursa ya kufikia masoko yanayohitaji bidhaa zenye ubora unaothibitishwa,” anasema Dkt. katunzi.
Katika juhudi za kupanua huduma nje ya Dar es Salaam, Dkt. Katunzi amewaambia wahariri hao kuwa TBS inaelekea kukamilisha na kukabidhi mradi wa Viwango House Dodoma wenye thamani ya Sh bilioni 24.7.
Maabara za kituo hicho zinatarajiwa kuhudumia pia mikoa ya Singida na Tabora, hivyo kuongeza upatikanaji wa huduma za upimaji na uthibitishaji ubora kwa wazalishaji na wafanyabiashara wa maeneo hayo.
Wakati huohuo, ujenzi wa Viwango House Mwanza, eneo la Kiseke wilayani Ilemela, unaendelea kwa gharama ya Sh bilioni 12.1. Kituo hicho kinalenga kuhudumia mikoa sita ya Kanda ya Ziwa, huku maandalizi ya awali ya ujenzi wa kituo kingine Arusha yakiwa yameanza.
“KKusogezwa kwa huduma hizi karibu na wazalishaji kumepunguza muda na gharama zinazohusiana na upimaji wa bidhaa, hasa kwa kampuni ambazo hapo awali zililazimika kusafiri umbali mrefu kupata huduma hizo,” anasema.
TBS pia imetumia zaidi ya Sh bilioni 9.8 kuimarisha ofisi tisa za kanda na vituo vya mipakani kwa kuongeza watumishi na vitendea kazi vinavyohitajika katika udhibiti wa bidhaa.
Uwekezaji huo una umuhimu zaidi katika soko linalopokea bidhaa kutoka nchi mbalimbali, ambako udhibiti madhubuti ni muhimu ili kuhakikisha bidhaa zinazoingia zinakidhi matakwa ya viwango vinavyotumika nchini.
Viwango 3,901 kuongeza ushindani
Dkt. Katunzi amesema katika eneo la uandaaji wa viwango, TBS imeandaa viwango 3,901 kupitia kamati 117 za kitaalamu zinazoshirikisha wadau mbalimbali.
“Viwango hivyo vinaweka vigezo vinavyoweza kutumiwa kutathmini ubora, usalama na sifa za bidhaa katika sekta mbalimbali za uchumi,” anasema.
Katika kipindi hicho, shirika lilitoa vyeti na leseni 3,940 za ubora kwa wazalishaji, zikiwamo 1,683 zilizotolewa kwa wajasiriamali wadogo wanaohudumiwa bila malipo.
Dkt. Katunzi anasema TBS imesema hutenga zaidi ya Sh milioni 300 kila mwaka kusaidia huduma hizo kwa wajasiriamali wadogo.
Mpango huo ni muhimu kwa sababu gharama za upimaji, uthibitishaji na kupata alama za ubora zinaweza kuwa kikwazo kwa biashara ndogo zenye mitaji finyu.
Udhibiti wa bidhaa na ulinzi wa walaji
Katika kulinda afya na usalama wa walaji, TBS ilisajili bidhaa 9,731 za chakula na vipodozi pamoja na maeneo 80,836 ya biashara.
Kwa upande wa bidhaa zinazoingia nchini, shirika lilikagua shehena 183,186 kabla ya kuingia Tanzania kupitia mfumo wa uthibitishaji wa bidhaa kabla ya kusafirishwa kwenda nchini (Pre-shipment Verification of Conformity — PVoC).
Aidha, shehena 426,842 zilikaguliwa baada ya kuwasili nchini kupitia ukaguzi wa bidhaa zinapofika (Destination Inspection), huku magari 249,386 yakikaguliwa.
Takwimu hizo zinaonesha ukubwa wa jukumu la TBS katika kusimamia ubora wa bidhaa zinazotumika na wananchi na zinazouzwa katika soko la Tanzania.
Udhibiti wenye ufanisi unaweza kupunguza uwezekano wa bidhaa zisizokidhi viwango kuingia sokoni, kulinda walaji dhidi ya bidhaa hatarishi na kusaidia ushindani wa haki kwa wazalishaji wanaowekeza katika ubora.
Kwa upande mwingine, mifumo ya ukaguzi inahitaji kuwa na uwazi, ufanisi na utabirika ili kuepusha ucheleweshaji usio wa lazima unaoweza kuongeza gharama kwa waagizaji na watumiaji wa bidhaa.
Bilioni 12.9/- za vifaa vya maabara
Dkt. Katunzi anasema uwezo wa kupima na kuthibitisha ubora wa bidhaa ni sehemu nyingine muhimu ya uwekezaji wa TBS.
“Shirika lina maabara 14 zenye ithibati ya umahiri wa kimataifa, ambazo zilipima sampuli 188,952 na kufanya ugezi wa vifaa 54,396 katika kipindi kilichoripotiwa,” anasedma.
Aidha, Serikali imewekeza zaidi ya Sh bilioni 12.9 katika vifaa vya kisasa vya maabara.
Miongoni mwa vifaa vilivyotajwa ni mashine ya kupima uwezo wa mabomba ya maji kuhimili shinikizo (hydrostatic pressure test), ambayo kwa mujibu wa taarifa ya TBS inapatikana katika nchi tano pekee barani Afrika.
Vifaa vingine ni mashine ya kidijitali ya kupima ukinzani wa umeme katika nyaya (automatic conductor resistance tester) na mashine ya kupima utendaji wa paneli za sola (solar simulator), ambayo TBS imesema ndiyo pekee ya aina yake katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.
Mifumo ya kidijitali kurahisisha huduma
Katika kuboresha utoaji wa huduma, TBS imeunganisha mfumo wake wa maombi mtandaoni (OAS) na Mfumo wa Dirisha Moja la Huduma za Biashara Tanzania (TeSWS).
Lengo ni kurahisisha upatikanaji wa huduma kwa wafanyabiashara na kupunguza usumbufu unaoweza kujitokeza katika taratibu za maombi.
Kwa mazingira ya sasa ya biashara, mifumo ya kidijitali inaweza kuongeza uwazi, kurahisisha ufuatiliaji wa maombi na kupunguza muda unaotumika kukamilisha taratibu za kiutawala.
Tuzo na ithibati za kimataifa
Dkt Katunzi amewaambia wahariri kuwa TBS imetambuliwa katika ngazi ya kitaifa na kimataifa kutokana na utendaji wake na kutunukiwa tuzo kadhaa.
Kwa mujibu wa taarifa ya Dkt. Katunzi, shirika lilitambuliwa kama Taasisi Bora ya Udhibiti Barani Afrika mwaka 2023, pamoja na kupata utambuzi kutoka Shirika la Afya Duniani (WHO) na Shirika la Kimataifa la Viwango (ISO).
Aidha, Ofisi ya Msajili wa Hazina ililitambua kama taasisi ya tatu bora ya Serikali iliyofanya mabadiliko makubwa ya utendaji na kuongeza gawio katika mwaka wa fedha 2025/2026.
TBS pia imepata ithibati zinazohusishwa na taasisi za kimataifa na kikanda, zikiwamo SADCAS, BIPM na ARSO.
TBS muhimili utekelezaji wa Dira ya 2050
Akizungumza kwa niaba ya Msajili wa Hazina, Sabato Kosuri alisema Shirika la Viwango Tanzania (TBS) lina nafasi ya kimkakati katika juhudi za Tanzania za kutekeleza Dira ya Maendeleo ya 2050, hususan katika kujenga uchumi shindani unaoendeshwa na sekta binafsi imara.
Alisema jukumu la TBS la kusimamia viwango vya ubora wa bidhaa na huduma linaifanya kuwa taasisi muhimu katika kuhakikisha kuwa malengo ya kiuchumi ya nchi yanatafsiriwa katika matokeo halisi ya maendeleo kwa wafanyabiashara na wananchi kwa ujumla.
Kosuri alisema kufikia mwaka 2050, Tanzania inapaswa kujenga uchumi shindani kwa kuimarisha minyororo ya thamani inayowaunganisha wazalishaji na wafanyabiashara nchini kote, katika ukanda wa Afrika Mashariki na katika masoko ya kimataifa.
Alisisitiza kuwa uwepo wa viwango vinavyolingana na miundombinu imara ya uhakiki wa ubora ni muhimu katika kufanikisha azma hiyo, kwa kuwa tofauti katika matakwa ya bidhaa na vigezo vya ubora zinaweza kuzuia biashara na kupunguza uwezo wa wafanyabiashara wa Tanzania kushindana katika masoko ya nje ya nchi.
Alisisitiza kuwa TBS haipaswi kuonekana kama taasisi ya udhibiti pekee, bali pia kama mshirika wa kimkakati katika mageuzi ya uchumi wa nchi. Alisema miundombinu imara ya viwango inaweza kusaidia wafanyabiashara kuboresha ubora wa uzalishaji, kuimarisha imani ya walaji na kuhakikisha bidhaa zao zinakidhi matakwa ya masoko ya kikanda na kimataifa.
Kwa msingi huo, alisema, uwekezaji wa TBS katika maabara, mifumo ya uthibitishaji wa ubora na huduma kwa wafanyabiashara una umuhimu mkubwa wakati Tanzania ikijitahidi kupanua uzalishaji wa viwandani na kuongeza ushindani wa bidhaa zinazozalishwa nchini.
Kosuri alisema mkutano kati ya TBS na wahariri wa vyombo vya habari, ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina, ni sehemu ya juhudi pana za kuimarisha uwajibikaji, utawala bora na ushirikiano kati ya taasisi za umma na wananchi kupitia vyombo vya habari.
Umebakiwa na makala 2 za bure mwezi huu. Jiunge ili kusoma bila kikomo.
- TBS
- Viwango Tanzania
- Dkt. Ashura Katunzi
- ubora wa bidhaa
- biashara Tanzania
- wajasiriamali
- maabara za kisasa
- udhibiti wa bidhaa
- ushindani wa biashara
- uchumi Tanzania