Habari
Wasira ahimiza vikao CCM, kujitambua
MAKAMU Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Bara, Stephen Wasira, amewataka wanachama wa chama hicho kukutana mara kwa mara katika vikao rasmi.

Amehimiza vikao vya chama chao ili kujadili masuala muhimu na kuepuka kupotoswa na taarifa zisizo na ukweli zinazosambazwa kwenye mitandao ya kijamii.
Akizungumza wiki iliyopita katika ziara yake wilayani Ikungi, Singida Wasira alisema vikao hivyo vinawapa wanachama fursa ya kupata taarifa sahihi na kuambizana ukweli.
“Wanachama wetu nchi nzima, kwa mujibu wa Katiba mna vikao vya wanachama. Mkutane muambizane. Siku hizi kwenye mitandao kuna uongo mwingi sana. Usipoangalia unaweza hata wewe kushirikishwa kusema uongo,” alisema.
Alisisitiza kuwa ni muhimu wanachama kukutana na kujadili madai yanayosambaa, kisha kumtafuta mtu mwenye ujuzi awasaidie kuyafafanua na kuujua ukweli.
Makamu Mwenyekiti huyo alibainisha kuwa mikutano ya wanachama ni fursa muhimu ya kujadili masuala yanayoendelea nchini ili waweze kukitetea chama ipasavyo.
Kuhusu uhuru na umoja wa nchi, Wasira amesema CCM itaendelea kulinda urithi huo uliopatikana kwa kazi kubwa.
Aliongeza kuwa wapo wanaodai CCM haijatekeleza chochote tangu uhuru, jambo ambalo amesema ni kinyume na ukweli.
Wasira aliwataka wanachama wenye nia ya kugombea nafasi za uongozi kujitokeza bila kuogopa kuwa hawana fedha, akisema kiongozi anapaswa kuchaguliwa kwa uwezo, sifa na uadilifu, siyo kwa kutumia fedha kushawishi wapiga kura.
Akiwa Iramba, Wasira aliwakumbusha wana-CCM wenzake kuwa chama hakipaswi kuruhusu viongozi wanaopatikana kwa rushwa, vitisho au ujanja, akisisitiza kuwa viongozi wanapaswa kuchaguliwa kwa misingi ya haki na uwezo.
Kuhusu uimara wa viongozi, Wasira alisema viongozi hawapaswi kuyumba katika masuala ya msingi au kubadilisha misimamo kutokana na mazingira au maslahi binafsi.
Alisema utajiri siyo kipimo cha uwezo wa kuongoza. Kauli yake ilikuwa kwamba mtu hawezi kudai uwezo wake wa uongozi umeongezeka kwa sababu fedha zake zimeongezeka; kwa mtazamo wake, fedha haziwezi kuongeza uwezo wa mtu kuongoza.
Alisema uwezo wa kuongoza si jambo la kudumu maisha yote na kiongozi anapaswa kuwa tayari kumpisha mwingine pale anapoona uwezo wake hauendani tena na mahitaji ya wakati.
Aliwataka wanachama kutumia vikao rasmi badala ya kutegemea taarifa za mitandao ya kijamii.
Wasira alionya kuwa kuna taarifa nyingi zisizo za kweli kwenye mitandao na akashauri wanachama wakutane, wajadili madai yanayosambaa na watafute ufafanuzi kutoka kwa wenye ujuzi.
Katika ziara hiyo Wasira alitembelea Manyoni, Ikungi na Iramba, ikiwa na lengo la kuimarisha uhai wa chama na maandalizi ya uchaguzi wa ndani wa CCM unaotarajiwa mwaka 2027.
- CCM
- Stephen Wasira