Bustani ya Sheria
Ardhi yako imevamiwa? Usifanye kosa hili la kusubiri
IKIWA una mgogoro wa ardhi na ukaendelea kulalamika kwa viongozi wa kijiji kwa miaka mingi, hatua hiyo pekee haisimamishi ukomo wa muda wa kisheria (limitation period).
Katika hukumu hii, mrufani (appellant) alieleza kuwa aligundua madai ya mjibu rufaa (respondent) dhidi ya ardhi yake mwaka 2011.
Baada ya hapo, aliwasilisha malalamiko kadhaa kwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Mang’onyi, lakini mashauri rasmi ya kisheria yalianza mwaka 2025.
Mahakama Kuu ilibaini kuwa kipindi hicho kilikuwa takriban miaka 14, wakati sheria ya kudai au kurejesha ardhi (recovery of land) ikiekeza ukomo wa muda wa miaka 12.
Katika kesi ya Elisha Kyang’u Sungi v. Israel Joseph (Land Appeal No. 7723/2026, High Court Dodoma), Jaji: Mheshimiwa Hassan, J.
Elisha Kyang’u Sungi alidai kuwa alipata eneo la ardhi lenye ukubwa wa ekari 25 mwaka 1982 baada ya kulifyeka na kuanza kulitumia. Mwaka 1990, aliondoka eneo hilo na kumuachia baba yake, Kyangu Khome, aliyefanya shughuli za kilimo na ufugaji hadi alipofariki dunia mwaka 2008.
Hata hivyo, mnamo mwaka 2011, Elisha alitaarifiwa na mtu aitwaye Apolinary kuwa kuna mtu mwingine aliyekuwa anadai umiliki wa ardhi hiyo.
Hapo ndipo msingi wa mgogoro ulipoanzia.
Sasa badala ya kufungua mashauri rasmi ya kisheria au ya kimahakama mara moja, aliendelea kuripoti mgogoro huo kwa Mwenyekiti wa Kijiji cha Mang’onyi kwa nyakati tofauti. Pamoja na malalamiko hayo, mgogoro haukupata usuluhishi.
Hatimaye, mnamo mwaka 2025, ndipo alipoanzisha mashauri rasmi kwanza katika Baraza la Ardhi la Kata (Ward Tribunal) na baadaye katika Baraza la Ardhi na Nyumba la Wilaya (District Land and Housing Tribunal).
Hapa ndipo suala kuu la kisheria lilipoibuka, je, muda wa kufungua kesi ulikuwa umekwisha kisheria?
Mahakama ilirejelea Sheria ya Ukomo wa Muda, Sura ya 89 (R.E. 2023) (Law of Limitation Act, Cap.
89 R.E. 2023) Kifungu cha 4 kinaeleza kuwa hesabu za muda wa ukomo huanza pale tu haki ya kuchukua hatua za kisheria inapojitokeza (right of action accrues).
Kipengele cha 22, Sehemu ya I ya Jedwali kinaweka ukomo wa miaka 12 kwa mashauri ya kurejesha au kudai ardhi (suit for recovery of land).
Kutokana na msingi huo, suala kuu halikuwa tu kujua kama Elisha alikuwa mmiliki halali, bali alijua lini kwa mara ya kwanza kuwa kuna mtu mwingine anayedai haki juu ya ardhi yake?
Majibu yalipatikana kutoka kwenye ushahidi wa mrufani mwenyewe. Alikiri kuwa alifahamu uwepo wa madai hayo yanayokinzana na umiliki wake (adverse claim) mwaka 2011, na ndipo alipoanza kuwasilisha malalamiko kwa serikali ya kijiji.
Mahakama ilifafanua kuwa, mara tu alipogundua kuwa kuna mtu anayepinga umiliki wake, mazingira yaliyotoa haki ya kufungua shauri (cause of action) yalikuwa yameshajitokeza tayari.
Kwa hiyo, saa ya ukomo wa muda (limitation clock) ilianza kuhesabu kuanzia mwaka 2011.
Wakati sheria inataka shauri lifunguliwe ndani ya miaka 12, mrufani alifungua shauri lake baada ya miaka 14 kupita. Kwa hiyo, hata kwa kuzingatia maelezo yake mwenyewe, alikuwa ameshapitiliza muda uliowekwa na sheria.
Je, malalamiko katika serikali ya kijiji yalisimamisha saa ya sheria?
Jibu ni Hapana na hili ndilo somo kuu la kisheria katika kesi hii.
Mahakama ilibaini kuwa kufanya jitihada za kisera au kiutawala (administrative settlement) kupitia viongozi wa kijiji hakuondoi wala kuzuia haki ya msingi ya kufungua shauri iliyokwisha kujitokeza (cause of action), na wala haisimamishi saa ya kisheria (statutory clock).
Kwa maneno mengine, kutoa taarifa au kulalamika kwa viongozi wa kijiji hakumaanishi kuwa muda wa ukomo wa kisheria unaanza upya kila unapolalamika.
Mwandishi ni Mwanasheria na Mchambuzi wa Sheria kutoka KGM Attorneys).
- Ardhi
- Sheria
- Mahakama