Bustani ya Sheria
Sakata la Wakili Fatma Karume – V
KATIKA sehemu ya nne tuliona jinsi Mahakama Kuu ilivyotengua uamuzi wa Kamati ya Maadili ya Mawakili uliokuwa umemfuta Wakili Fatma Karume kwenye Daftari la Mawakili.
Sababu haikuwa kwamba Mahakama ilisema Fatma hakufanya kosa. La hasha, bali ilisema utaratibu uliotumika kuifikisha kesi mbele ya Kamati haukufuata agizo la awali la Mahakama, kwani aliyepaswa kuipeleka ilikuwa ni Msajili wa Mahakama Kuu, siyo Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Kwa wengi, huo ulikuwa ushindi mkubwa kwa Fatma Karume, lakini serikali haikuwa tayari kukubali kushindwa.
Baada ya Mahakama Kuu kutengua uamuzi wa Kamati ya Maadili, Mwanasheria Mkuu wa Serikali pamoja na Kamati ya Maadili walitaka kupeleka shauri hilo Mahakama ya Rufani, lakini kulikuwa na kikwazo kimoja muhimu.
Kwa mujibu wa sheria, hawangeweza kukata rufaa moja kwa moja kwani walipaswa kwanza kupata ruhusa (leave) kutoka Mahakama Kuu.
Hivyo wakafungua maombi wakiiomba Mahakama Kuu iwape ruhusa ya kukata rufaa.
Upande wa Fatma Karume, ukiwakilishwa na Wakili Peter Kibatala pamoja na Dkt. Rugemeleza Nshala, uliipinga hoja ya serikali.
Kwa kifupi, waliieleza Mahakama kwamba haikuwa imeonyesha hoja mpya nzito zinazostahili kujadiliwa Mahakama ya Rufani.
Uamuzi wa Mahakama Kuu ulikuwa umejengwa kwenye misingi sahihi ya sheria.
Hakukuwa na sababu ya kuiruhusu Serikali kuendelea na rufaa nyingine.
Kwa hiyo, waliomba maombi hayo yatupiliwe mbali.
Mahakama ya Tanzania (Kuu) ikaamua baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, Mahakama Kuu ilifikia uamuzi wake na kutamka kuwa serikali haikuonyesha hoja za msingi (arguable points of law) zinazohitaji kuamuliwa na Mahakama ya Rufani.
Kwa sababu hiyo, Mahakama ikakataa kutoa ruhusa (leave) ya kukata rufaa na kwa lugha rahisi serikali ilishindwa hatua ya kwanza kabisa.
Haikuruhusiwa kwenda Mahakama ya Rufani kupitia njia hiyo, je, hapo ndipo kesi iliisha?
Wengi walidhani ndiyo, lakini serikali haikukata tamaa.
Badala ya kuishia hapo, serikali Iliamua kujaribu tena na safari hii haikurudi Mahakama Kuu.
Iligonga moja kwa moja mlango wa Mahakama ya Rufani, ikiomba ruhusa hiyo hiyo ambayo ilikuwa imekataliwa na Mahakama Kuu.
Katika taaluma ya sheria, hatua hiyo mara nyingi huitwa “second bite” yaani kujaribu tena kupata ruhusa baada ya kunyimwa katika mahakama ya chini.
Lakini hata safari hiyo haikuwa rahisi, kwani kulikuwa na pingamizi jingine la kiufundi lililowakabili kabla hata Mahakama ya Rufani haijafikiria kama wapewe ruhusa au la.
Je, pingamizi hilo lilikuwa nini? Na Mahakama ya Rufani ililiamuaje?
Hapo ndipo simulizi hili linaingia katika hatua ya sita.
Itaendelea...
Mwandishi ni Mwanasheria na Mchambuzi wa Sheria kutoka KGM Attorneys). Anapatikana kwa namba: au Email: karimbinmussa@gmail.com
- Fatma Karume
- Sheria
- Mahakama