Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Bustani ya Sheria

Sakata la Wakili Fatma Karume – IV

KATIKA sehemu ya tatu tuliona jinsi Kamati ya Maadili ya Mawakili ilivyomkuta Wakili Fatma Karume na hatia ya utovu mkubwa wa nidhamu na kuamuru afutwe kabisa kwenye Daftari la Mawakili.

Jumatatu, 17 Agosti 2026 · 15:15Dakika 3 kusomaToleo 178, uk. 26

Kwa wengi, huo ulionekana kuwa mwisho wa safari yake ya uwakili, lakini kwa Fatma Karume Ilikuwa mwanzo wa vita vipya vya kisheria.

Fatma alikata rufaa Mahakama Kuu baada ya kuvuliwa uwakili kwani hakukubaliana na uamuzi wa kamati.

Kupitia wakili wake, Peter Kibatala, mbele ya Jopo la Majaji watatu (Full Bench), hata hivyo kabla hata rufaa haijaanza kusikilizwa, serikali iliweka mapingamizi ya awali.

Upande wa Mwanasheria Mkuu uliiambia Mahakama kwamba rufaa ya Fatma ilikuwa mbovu kisheria. Walidai kwamba hakufuata utaratibu wa kutoa Notice of Appeal na kwamba alitumia hati isiyo sahihi kwa kuwasilisha Petition badala ya Memorandum, au kinyume na utaratibu uliowekwa kwenye Kanuni za Nidhamu za Mawakili na zaidi kuwa hakufuata njia sahihi ya kuwasilisha rufaa kupitia Katibu wa Kamati kama sheria ilivyotaka.

Kwa kifupi, serikali ilitaka Mahakama isisikilize kabisa hoja za Fatma na hapo jopo la majaji likachambua hoja hizo moja baada ya nyingine.

Baada ya kufanya hivyo likasema kuwa mapingamizi yote hayana msingi wa kuizuia rufaa kusikilizwa. Mahakama ikaamua kwamba kasoro zilizodaiwa hazikuwa za kiwango cha kuua rufaa.

Kwa hiyo, rufaa ya Fatma ikaendelea kusikilizwa kwa hoja zake za msingi na hii ikawa ushindi wake wa kwanza tangu avuliwe uwakili, ingawa ushindi mkubwa ulikuwa bado mbele.

Hoja iliyoitikisa kesi nzima ya Fatma ni kuwa hakujikita kujitetea kuhusu kama maneno aliyotumia yalikuwa sahihi au la, badala yake aliuliza swali moja muhimu sana. Je, Kamati ya Maadili ilikuwa na mamlaka ya kusikiliza shauri lililofikishwa mbele yake kwa namna lilivyofikishwa?

Hii ndiyo hoja iliyogeuza kabisa mwelekeo wa kesi. Kupitia Wakili Peter Kibatala, Fatma aliieleza Mahakama ya Tanzania kuwa katika kesi ya Ado Shaibu, Jaji Feleshi alikuwa tayari ametoa maelekezo maalumu. Maelekezo hayo yalikuwa wazi kabisa.

Sakata la Wakili Fatma Karume – IV Na Wakili Karim Gabriel Mussa Kwamba Msajili wa Mahakama Kuu ndiye alitakiwa kupeleka suala la nidhamu la Fatma kwenye Kamati ya Maadili.

Lakini kilichotokea baadaye kilikuwa tofauti.

Badala ya kusubiri Msajili atekeleze amri ya Mahakama, Mwanasheria Mkuu wa Serikali akaenda mwenyewe kufungua shauri jipya mbele ya Kamati ya Maadili. Kwa hiyo Fatma akasema, Kamati ilisimamia shauri ambalo halikuletwa mbele yake kwa utaratibu ulioagizwa na Mahakama.

Na kama msingi wa kuifikisha kesi ulikuwa batili, basi hata uamuzi wote uliotolewa ulikuwa batili.

Serikali haikukubalia na ilisema kuwa Mahakama ilikuwa imetoa maelekezo kwa Msajili, lakini maelekezo hayo hayakumzuia Mwanasheria Mkuu kufungua malalamiko mengine mapya.

Zaidi ya hayo malalamiko yaliyowasilishwa mbele ya Kamati hayakuhusu maneno yaliyotamkwa Mahakamani pekee, yalijumuisha pia machapisho ya Twitter na matukio mengine yaliyotokea baadaye.

Kwa hiyo, kwa mtazamo wa serikali, Kamati ilikuwa na mamlaka kamili ya kuyasikiliza.

Uamuzi wa Mahakama

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote mbili, jopo la majaji likafikia hitimisho ambalo halikutarajiwa na wengi. Majaji wakasema; ni kweli Mahakama ya kwanza ilikuwa tayari imetoa agizo mahsusi kwamba Msajili wa Mahakama ndiye angepeleka suala hilo kwenye Kamati.

Agizo hilo lilikuwa bado halijawahi kufutwa wala kubadilishwa.

Kwa hiyo, Mwanasheria Mkuu hakuwa na mamlaka ya kulipuuza agizo hilo na kufungua shauri jipya lililochanganya malalamiko yaleyale yaliyokuwa tayari yameguswa na Mahakama.

Majaji wakasema hatua hiyo ilikuwa imeenda kinyume na agizo la Mahakama. Na pale ambapo msingi wa kuanzisha shauri ni batili, na kwamba hata uamuzi unaotolewa juu yake hauwezi kusimama.

Itaendelea… Mwandishi ni Mwanasheria na Mchambuzi wa Sheria kutoka KGM Attorneys). Anapatikana kwa namba: au Email: karimbinmussa@ gmail.com.

  • Fatma Karume
  • Sheria
  • Mahakama

Soma Pia