Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Barua za Wasomaji

Barua za Wasomaji — Toleo 177

Kero, ushauri na maoni kutoka kwa wasomaji wa Pambazuko.

Jumatatu, 10 Agosti 2026 · 17:15Dakika 3 kusomaToleo 177, uk. 30

Tutaandamana kwenda Dawasa kudai maji

Mhariri, SISI wananchi wa mitaa ya Masaki, Amani na Kilima Cheupe — Mbezi Kimara, Dar es Salaam, tumekosa maji kwa zaidi ya miezi sita.

Tumechoka kuahidiwa uongo wa mara kwa mara na mafundi wa Dawasa, ambao kila wakifika eneo hili wanadai wanashughulikia tatizo kumbe hakuna kitu.

Kwa kipindi kirefu tumeishi kwa kununua maji ambapo ndoo inauzwa shilingi 500 na kutumia maji ya mabawa ambayo siyo salama, ambayo yameleta shida kubwa kwa familia zetu kupata magonjwa ya tumbo.

Sasa tumeamua tuandamane kwenda ofisi ya Dawasa, tukakutane na uongozi watuambie suluhisho la kudumu la tatizo letu ni nini na litapatikana lini. Tumechoka, na kama tumetengwa basi waje waondoe mabomba yao tujue hatuna maji.

Tumepanga kuandamana kwenda ofisi za Dawasa Kinyerezi muda wowote kuanzia sasa.

Innocent Frank, Masaki, Mbezi

Walimu washirikiane na wazazi

NAANDIKA barua hii ili kutoa wasiwasi wangu kuhusu tatizo linaloongezeka la wanafunzi wengi kuchelewa kufika shule kila siku.

Kuchelewa kunapunguza muda wa kujifunza.

Mwanafunzi anayekosa masomo ya mwanzo hukosa misingi muhimu.

Hii inachangia kupata alama duni na hata kushindwa mitihani.

Pia tabia ya kuchelewa inaharibu nidhamu, shule inafundisha uongozi wa muda na uwajibikaji.

Mwanafunzi anayezoea kuchelewa anakuwa mtu asiyejali muda, jambo ambalo litaathiri maisha yake baadaye.

Pia usalama unakuwa hatarini, wanafunzi wengi hukimbia barabarani au kutumia njia za mkato ili kuwahi kufika shuleni, hivyo kuhatarisha maisha yao.

Tatizo hili linatokana na wazazi kutowaamsha watoto mapema au wanafunzi wenyewe kushindwa kuwajibika kwa hilo, lakini pia msongamano wa magari na baadhi ya wanafunzi kukosa nidhamu binafsi.

Napendekeza shule zishirikiane na wazazi kutoa elimu ya umuhimu wa muda na serikali iboreshe usafiri wa asubuhi.

Tujadiliane ili kizazi chetu kipate elimu kamili bila vikwazo vya ucheleweshaji.

Mwanahamisi Mwenda, Ilala, Dar es Salaam

Kwa nini sisi ni taifa la ‘machawa’?

MARA nyingi najijiuliza kwa nini tumeamua kuwa na taifa la machawa?

Inashangaza kwamba mtu anapokuwa chawa, viongozi wa serikali hutoa fursa na nafasi kwa watu wa aina hiyo, bila kutambua kuwa wanalea vijana wanaoshindwa kuwa wabunifu kulijenga taifa lao.

Inasikitisha kuona machawa wanapewa nafasi ya kuingia bungeni, na pia nasikia wapo wanaofanya uchawa ndani ya majengo makubwa na yenye heshima ya Tanzania yetu. Hii ni aibu kwa taifa.

Ninajiuliza kwamba – je, hawaoni kwa kufanya hivyo wanaua kizazi cha watu wanaojitambua?

Wapo watu wanaofanya mambo makubwa katika sekta mbalimbali, ukienda pale DIT au Costech, utakutana na vijana wanaobuni vitu kwa kutumia teknolojia, lakini hawana hata nafasi ya kukutana na wakubwa wetu ili kuwatia zaidi moyo na hata ikiwezekana fursa zaidi. Ukienda Muhimbili utakutana na madaktari bingwa wenye umri mdogo, watu kama hawa ndiyo wanapaswa kupewa kipaumbele na nafasi katika taifa linalojielewa.

Michael Elias, Mbagala, Dar es Salaam

Mamlaka iangalie Soko la Tandika

NAOMBA kutoa kilio changu kuhusu uchafu katika Soko la Tandika, Dar es Salaam.

Mitaro ya soko hilo inatiririsha maji machafu kiasi cha kuhatarisha afya za watu wanaokwenda sokoni hapo.

Napaza sauti hii kupitia chombo chako cha habari ili wahusika walifanyie kazi jambo hili.

Imekuwa kawaida kwa wafanyabiashara, hasa wa samaki kumwaga uchafu ambao hutiririka katika mitaro na kusababisba adha kwa wanaoingia sokoni.

Tunaomba mamlaka husika iliangilie hili kwa uzito ili kuepuka madhara makubwa zaidi.

Halima Said, Tandika, Dar es Salaam

Sheria ya silaha irekebishwe sasa

SERIKALI ni vyema ikapitia upya sheria ya umiliki wa silaha, hasa kwa wasanii, kwa sababu baadhi yao wamekuwa wakitumia silaha kutishia watu pasipokuwa na sababu za msingi.

Ninatoa ushauri huu kwa sababu hivi karibuni, msanii mmoja anadaiwa kumfyatulia risasi mtu aliyedaiwa kuwa mwizi.

Matukio ya aina hii yamekuwa yakijirudia sana kwa wasanii wetu kutumia silaha hovyo na wengine wamekuwa wakizionesha silaha zao kupitia mitandao yao ya kijamii, jambo ambalo linakatazwa kisheria.

Ombi langu jingine kwa mamlaka husika ni kuwapatia elimu hawa wasanii na watu wengine wote ambao wanamiliki silaha, kwa sababu wanazitumia ‘ndivyo sivyo’ kwa kutisha raia mitaani.

Abdul Juma, Ngaramtoni, Arusha

Nini tatizo Barabara Mailimoja – Baobab

HII ni mara ya nne naleta tena kero kuhusu barabara inayotoka Mailimoja hadi Baobab kuelekea Bagamoyo kupitia Kata ya Pangani, Halmashauri ya Kibaha Mji.

Barabara hii ni mbovu kupindukia.

Ahadi zimekuwa nyingi kuwa tungejengewa kwa kiwango cha lami tangu mwaka juzi lakini hakuna kinachoendelea.

Tunaomba kwa mara nyingine mamlaka itutatulie kero hii.

Anna Rweyemamu, Kibaha

  • Barua
  • Wasomaji

Soma Pia