Barua za Wasomaji
Barua za Wasomaji — Toleo 178
Kero, ushauri na maoni kutoka kwa wasomaji wa Pambazuko.

Mamlaka ishughulikie kero ya ombaomba Dar
JIJI la Dar es Salaam limejaa watu wanaoomba msaada mitaani, hasa kwenye taa za barabarani na vituo vya mabasi.
Wengi wao ni watoto na wazee waliolazwa na umaskini, hali inayoleta usumbufu kwa madereva na abiria kwani wengine huingia barabarani na kuzuia magari.
Ombaomba hao pia hasa watoto wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya uhalifu wanavyovifanya kwa kivuli cha uombaji.
Tunaomba mamlaka kwa kushirikiana na wadau vishughulikie jambo hili ili kuondoa kero hizo.
Lakini pia Jeshi la Polisi lifanye doria ili kudhibiti uwepo wao na wananchi waache kutoa msaada mtaani bali tuwafikishie vituoni. Hii itasaidia kupunguza kero na kulinda heshima ya jiji letu.
Habiba Hamidu, Dar es Salaam

Serikali iokoe Stendi ya Mtoni Kijichi
NATOA wito kwa serikali kupitia Wizara ya Ujenzi na Mamlaka ya Dar es Salaam kuja kuangalia kilio chetu sisi wakazi wa Mtoni Kijichi.
Miaka michache iliyopita serikali ilitumia fedha nyingi kujenga stendi ya mabasi ya kwenda mikoa ya kusini iliyopo Mtoni Kijichi.
Lengo lilikuwa kupunguza msongamano jijini, kuwapunguzia abiria usumbufu na kutoa huduma bora.
Leo stendi hiyo imetelekezwa na kubaki bila kazi yoyote na kusababisha uwekezaji wa mamilioni kupotea bila tija yoyote.
Abiria wanaokwenda mikoa ya kusini hivi sasa wamerejea tena katika eneo la Mbagala na Temeke, ndio wanateseka kusubiri mabasi ya kwenda kusini wakipigwa na jua au kunyeshewa mvua kwa sababu stendi hizo hazina miundombinu yoyote.
Swali langu ni kwa nini kujenga mradi mkubwa kisha kuutelekeza? Hii ni kupoteza fedha za walipakodi.
Naiomba serikali ifanye ukaguzi, irekebishe stendi hiyo na ianze kuitumia mara moja na ikiwa inaona haifai kwa kazi hiyo wawekeze. Pia iwajibishe waliotelekeza mradi huu.
Watanzania tunataka kuona matunda ya miradi mbalimbali kwa manufaa ya wananchi.
Abiria Mkereketwa, Dar es Salaam
Wapiga debe wadhibitiwe
NAANDIKA barua hii kwa kulaani uwepo wa wapigadebe katika vituo vya daladala kwa sababu wamekuwa kero kubwa kwa abiria.
Wengi wao hupiga kelele na kutoa matusi ili kuvuta abiria, hasa kwenye vituo na masoko.
Wengine hupanda mabasi hata wakati basi likiwa limejaa na kusababisha msongamano na ajali ndogo ndogo. Tabia hii imepunguza heshima ya usafiri wa umma na kuwafanya watalii kuhisi kutokuwa salama.
Tunaomba Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) kwa kushirikiana na halmashauri na mamlaka za serikali za mitaa kuweka mifumo ya kupokea abiria iliyo na nidhamu.
Pia Jeshi la Polisi lifanye doria ili kuwadhibiti wapiga debe hawa.
Ikiwa watadhibitiwa watasaidia jiji kuwa tulivu na lenye utaratibu na heshima hasa katika maeneo ya vituoni.
Jackson Peter, Makongo, Dar es Salaam
- Barua
- Wasomaji