Habari Kuu
CDF, IGP, DCI wagoma kushahidi, Lissu afunga utetezi
Mshitakiwa wa kesi ya uhaini nchini Tanzania, Tundu Antiphas Lissu amekamilisha utetezi wake wa kujinasua, baada ya wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama kugoma kuwa mashaidi wake, Pambazuko linaeleza.

MWENYEKITI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, amefunga rasmi ushahidi wake katika kesi ya uhaini inayomkabili baada ya mashahidi watatu; wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama aliowahitaji upande wa utetezi, kukataa kufika mahakamani.
Akizungumza leo, Septemba 18, 2026, mbele ya jopo la majaji wa Mahakama Kuu, Masjala - Ndogo ya Dar es Salaam, Lissu amesema Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Ramadhani Kingai, alikuwa akitarajiwa kuwa shahidi wake wa sita, lakini hakufika kutoa ushahidi.
Lissu, ambaye anajitetea mwenyewe, ameieleza mahakama kuwa alikutana na kuzungumza na Kingai, ambaye alimweleza kwamba hayuko tayari kuwa shahidi wa upande wa utetezi.
Kwa mujibu wa maelezo ya Lissu mahakamani, Kingai pia alimwambia kuwa Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini (IGP), Camilius Wambura, na Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi (CDF), Jenerali Jacob Mkunda, hawatakuwa tayari kutoa ushahidi watakaporejea nchini. Ilielezwa kuwa wapo nje ya Tanzania.
Lissu amedai zaidi kwamba Kingai alimweleza kuwa viongozi hao watatu “watashangilia” iwapo atatiwa hatiani.
Hata hivyo, kauli hiyo iliwasilishwa mahakamani na Lissu, na hakuna majibu ya moja kwa moja yaliyotolewa na Kingai, Wambura au Mkunda kuhusu madai hayo, wakati Pambazuko likiendelea kuwatafuta.
Kabla ya hatua hiyo, mahakama ilikuwa imekubali ombi la Lissu la kuwaita viongozi hao kuwa mashahidi wa utetezi.
Kutofika kwao kulikuwa kumechelewesha mwenendo wa kesi, huku Lissu akiomba muda wa kuwasiliana nao ili kujua kama wangetii wito wa mahakama.
Lissu ameeleza kuwa mazungumzo yake na Kingai, yameshindwa kufikia muafaka kwa wakuu hao wa vyombo vya usalama kufika mahakamani kutoa Ushahidi wao. Hatua ambayo imemlazimisha kumaliza ushahidi bila kuwasikiliza viongozi aliowaona muhimu zaidi kwenye utetezi kwake.
Kutokana na kutopatikana kwa mashahidi hao, Lissu ameieleza mahakama kwamba hana ushahidi mwingine wa kuwasilisha, hivyo kufunga rasmi sehemu yake ya utetezi.
Hatua hiyo inafungua ukurasa mwingine katika kesi hiyo yenye mvuto mkubwa wa kisiasa na kisheria.
Mahakama sasa inatarajiwa kuelekeza hatua zitakazofuata baada ya kukamilika kwa ushahidi wa utetezi, ikiwamo uwasilishaji wa hoja za mwisho kabla ya uamuzi.
Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini, ambalo alikutwa na kesi ya kujibu na endapo atakutwa na hatia, adhabu yake ni kunyongwa hadi kufa.
- Mkunda
- Wambura
- Kingai
- Polisi
- JWTZ
- Uhaini
- Tanzania