Habari Kuu
Nchimbi asubiri ‘vumbi litue,’ yuko salama
Tangu kutangaza kujiuzulu nafasi ya Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt. Emmanuel Nchimbi, mwanasiasa huyo amekuwa kimya na wala haonekani, hali inayoleta wasiwasi. Pambazuko limepata taarifa za wapi alipo.

NI siku 22 sasa tangu aliyekuwa Makamu wa Rais, Balozi Dkt. Emmanuel Nchimbi ajiuzulu wadhifa wake Agosti 25, 2026, huku wasiwasi ukitanda kuhusu alipo.
Ukimya wake na kutoonekana popote, kumezua maswali lukuki ambayo hayakuwa yamepata majibu, lakini sasa Pambazuko, pasinashaka, linaweza kueleza kwamba “Dkt. Emmanuel John Nchimbi, yuko salama.”
Gazeti la Pambazuko kutoka vyanzo vinavyomfikia na kuzungumza na Dkt. Nchimbi vimehakikisha kwamba mwanasiasa huyo aliyepata kuwa kiongozi wa juu kabisa, baada ya Rais Samia Suluhu Hassan yuko Dar es Salaam.
“Nchimbi yuko nyumbani kwake hapahapa Dar es Salaam, anapata muda wa kupumzika kwa sasa, anajipa muda pia wa kutafakari zaidi wakati akisubiri vumbi la sasa lipoe kidogo na mtamsikia na kumuona,” kilieleza chanzo hicho.
Watanzania waliingiwa wasiwasi baada ya kuwepo taarifa zilizoshindwa kuthibitisha aliko kiongozi huyo baada ya kujiuzulu.
Kupitia mitandao ya kijamii, mazungumzo ya wazi, mijadala ya wasomi, wana harakati na hata vijiweni, swali kuhusu alipo Dkt. Nchimbi halikuweza kupata majibu.
Hali hiyo pia ilikolezwa na kutopatikana kwa mwanasiasa huyo na balozi baada ya simu yake ya mkononi kutopatikana pia.
Pambazuko, kwa wiki tatu sasa limekuwa katika msako wa ukweli wa wapi alipo Dkt. Nchimbi, anafanya nini, kwa nini haonekani maeneo ya wazi hata kwenye nyumba za ibada, jambo ambalo siyo la kawaida kwake.
Kupitia vyanzo vyake ambavyo vinahifadhiwa kwa sababu maalum – angalau kwa sasa, Pambazuko limebaini kuwa kiongozi huyo amejipa muda kujipumzisha.
“Nawahakikishia kiongozi (Dkt. Nchimbi) ni mzima, yupo sehemu salama, amepumzika anasubiri ‘vumbi’ litulie, atakuja mtamuona tu. Watanzania wasiwe na hofu juu ya kiongozi wao, yuko salama...”
Dkt. Nchimbi amekaa madarakani chini ya miezi kumi, baada ya kuteuliwa kuwa mgombea mwenza wa Rais Samia Suluhu Hassan, Agosti 27, 2025, na kuapishwa Novemba 3, 2025, akichukua nafasi ya Dkt. Philip Mpango.
Mara ya mwisho Dkt. Nchimbi kuonekana hadharani ilikuwa Agosti 22, 2026 kwenye ufunguzi wa mradi wa kufua umeme wa maji wa Julius Nyerere (JNHP) wilayani Rufiji, Pwani.
Hata hivyo, kwenye shughuli hiyo, kiongozi huyo alifanyakazi ya kumkaribisha rais tu, licha kwamba alipewa dakika 10 za kuzungumza. Badala yake alitumia chini ya dakika moja, akimkaribisha Rais Samia akiwa ndiye mgeni rasmi wa shughuli hiyo.
Mawasiliano mengine ya Dkt. Nchimbi na Watanzania ni Agosti 25,2026 kupitia akaunti yake ya Instagram ambako alipitisha barua yake fupi ya kutangaza kujiuzulu kwake nafasi ya makamu wa rais na siku iliyofuata Agosti 26, 2026, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikamfutia uanachama wake.
- nchimbi
- kujiuzulu
- tanzania
- ccm