Jicho la Tai
Chacha, hata kutongozwa unaogopa?
Ama kweli dunia ina mambo mengi sana na haipoi hata siku moja. Ona jambo hili la kufikirisha; kwamba kiongozi mkubwa anaamua kutumia vyombo vya maguvu kudhibiti mtu anayemhusudu. Msome Mzee Tai ujue mengi.
PAUL Matiko Chacha, Katibu wa NEC, Oganaizesheni wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), ametuachia mjadala ambao hata vikao vya chama vinaweza kuuhitaji; je, kutongozwa ni kosa la jinai, sifa ya kisiasa au dharura inayohitaji kituo cha polisi?
Kwa simulizi yake, mwanamke aliyemtaja kwa jina la Sophia alifikishwa polisi baada ya kumtumia ujumbe wa simu eti unaompongeza na zaidi sana kubeba maono kwamba “anamkubali sana.”
Chacha akadai kwamba mwanamama huyo alikuwa pia anampa ujumbe wa kumtaka kimapenzi.
Sasa hapo ndipo mimi, kwa uzee wangu, nikajiuliza; Chacha ana shida gani? Au alitaka “attention” kidogo, jina lake lipite kwenye vichwa vya habari na watu wajue kuwa Katibu wa Oganaizesheni ana mvuto unaovuka mipaka ya matawi ya CCM?
Nilipokuwa CCM, tena nikiwa kiongozi, nilitongozwa mara nyingi. Sikuwahi kuomba gari la polisi, kuandaa jalada wala kuita waandishi wa habari. Nilijua jibu fupi linatosha: “Asante kwa kunikubali, lakini nimeoa na sina nafasi.”
Chacha angeweza kufanya vivyo hivyo, ikiwa kweli ujumbe ulikuwa ombi la mapenzi tu. Kumkataa mtu hakuhitaji pingu; kunahitaji sentensi iliyo wazi.
Mwanamke kumweleza mwanaume kuwa anampenda siyo uhalifu moja kwa moja, kama ambavyo mwanaume kumtongoza mwanamke siyo tiketi ya moja kwa moja kwenda kituoni.
Kinacholeta tatizo ni kulazimisha, kutishia, kutukana, kufuatilia au kuendelea kutuma ujumbe baada ya kukataliwa.
Hapo ndipo tunapaswa kuwa waangalifu.
Hatujaonyeshwa ujumbe wote, idadi yake wala mazingira yake. Ikiwa kulikuwa na vitisho, ulaghai, lugha chafu au usumbufu wa kudumu, Chacha alikuwa na haki ya kutafuta msaada wa polisi.
Lakini kama ilikuwa meseji ya “nakukubali”
au “ninakupenda,” basi kutumia polisi ni sawa na kuita zimamoto kwa sababu mshumaa umewaka mezani.
Huenda Sophia hakuvutiwa na sura pekee, labda aliona utendaji wa Chacha alipokuwa Mkuu wa Mkoa wa Tabora, akamkubali, kama CCM ilivyomuona na kumvuta makao makuu.
Mimi hapo nashangaa, badala ya Chacha kusoma pongezi iliyopitiliza, kiongozi wetu akaona vyema afungue jalada la uchunguzi.
Tena, cheo chake kinahusu oganaizesheni, kazi ya kuunganisha watu, kusikiliza hisia zao na kutatua mikwaruzano kwa hekima.
Kama kila anayezidisha sifa au kutuma moyo kwenye simu atapelekwa polisi, basi vituo vitahitaji dawati maalumu la viongozi kuzongwa kimapenzi.
Somo hapa ni kubwa kuliko utani. Viongozi wana mamlaka, mitandao na vyombo vya dola vinavyowatii, wanapaswa kujizuia kuvigeuza kuwa kinga dhidi ya kila usumbufu mdogo wa maisha. Polisi wana majukumu mazito; hawapaswi kuwa kamati ya kuchuja watu wanaowapenda viongozi.
Na pia, mipaka iheshimiwe. Kukubali utendaji wa kiongozi hakumpi mtu ruhusa ya kumsumbua bila mwisho, jibu la “hapana” linapaswa kutosha, lakini pia “hapana” isipotolewa, tukio la kawaida linaweza kuvikwa sare, likapandishwa kwenye gari la polisi na hata kuhukumu.
Kwa kumpeleka Sophia polisi kwa kutongoza tu, Chacha amefeli pakubwa katika kipimo cha busara.
Uongozi haupimwi kwa uwezo wa kuamuru, bali kwa kujua jambo gani linahitaji dola na lipi linahitaji ujumbe mmoja wa heshima.
- chacha
- tabora
- ccm
- rc
- katibu