Habari Kuu
Jaji Warioba, Prof Tibaijuka wakalia kuti kavu CCM
Makada wa siku nyingi wa CCM; Jaji Warioba na Prof. Tibaijuka, huenda wakapewa "kadi nyekundu" ya kuwafurusha ndani ya chama hicho tawala, Pambazuko laeleza.

KUNA dalili kwamba Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinajiandaa kuchukua hatua za kinidhamu dhidi ya makada wake wawili wastaafu, Jaji Joseph Sinde Warioba na Profesa Anna Kajumulo Tibaijuka, ikiwamo uwezekano wa kuwavua uanachama.
Taarifa zilizofikishwa katika chumba cha habari cha Pambazuko zinaeleza kuwa viongozi hao wameandikiwa barua za wito wa kufika mbele ya vikao vya chama kujibu tuhuma zinazowakabili.
Hata hivyo, Pambazuko halijapata uthibitisho huru kwamba barua hizo zimewafikia wahusika na endapo wamekubali kuhudhuria vikao hivyo.
Vyanzo vinadai kuwa hatua hiyo inahusishwa na kauli zao za hadharani kuhusu mwenendo wa CCM na serikali yake, ambazo baadhi ya viongozi ndani ya chama wanazitafsiri kuwa zimekwenda kinyume na utamaduni, nidhamu na taratibu za chama.
Kwa nyakati tofauti, Warioba ambaye amewahi kuwa Makamu wa Kwanza wa Tanzania na pia waziri mkuu wan chi hiyo, amesisitiza umuhimu wa katiba inayokidhi matakwa ya wananchi, uchaguzi wenye haki, maridhiano na kujengwa kwa taasisi zinazoheshimu utawala wa sheria.
Amekuwa pia akikosoa siasa za ubaguzi na kuonya kwamba vyama vinapaswa kutanguliza maslahi ya taifa.
Profesa Tibaijuka – ambaye alipata kuwa waziri, naye amewahi kutoa misimamo mikali kuhusu uwajibikaji, haki, uongozi na umuhimu wa CCM kurejea misingi yake badala ya kuwanyamazisha wanaotoa mawazo tofauti.
Kwa mujibu wa taarifa hizo, hoja inayotajwa kuwa nzito ni madai kwamba wamekuwa wakisema chama kimeondoka katika misingi yake ya usawa, haki na kuheshimu sauti za wananchi. Wakosoaji wa hatua hiyo wanaona adhabu inaweza kutafsiriwa kama kufunga milango ya mjadala wa ndani kabisa sasa.
Iwapo hatua ya kuwafukuza itatekelezwa, inaweza kuibua mjadala mkubwa kuhusu nafasi ya kukosoana ndani ya chama hicho.
Baadhi ya viongozi wa juu wa CCM wameweka hadharani misimamo yao kwamba Warioba na Tibaijuka wanapaswa kuhojiwa na ikiwezekana “wapishe” ili kutokera viongozi wa chama hicho tawala.
Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana wa CCM (UVCCM), Mohammed Ali Kawaida ameelezwa kusema kwamba “Jaji Warioba na Prof. Tibaijuka wanapaswa kupumzika na kufunga midomo yao ili CCM ifanye kazi ya kuwaletea wananchi maendeleo.”
Katibu wa Umoja wa Wazazi wa CCM, Ally Hapi naye amekuwa akipenda “kuwaponda” wastaafu wanaotoa maoni yao kwa kukosoa chama hicho na viongozi wake akisema kuwa “waache chokochoko."
Viongozi wengine hasa wa jumuia za chama hicho, wameita waandishi wa habari na kuwakemea Jaji Warioba na Prof. Tibaijuka kwa madai kwamba "wanakivuruga chama chao," hivyo dawa pekee ya kuwanyamazisha ni kuwafukuza uanachama.
Tayari Prof. Tibaijuka amesema kwamba amesikia kuwepo kwa njama za kumfukuza chama na kwamba yuko tayari kwa lolote, lakini hatakaa kimya wakati kuna mambo "yanavurugika." Jaji Warioba hajasikika kuzungumzia tishio hili.
- Jaji Warioba
- Prof. Tibaijuka
- CCM
- kufukuzwa uanachama