Habari Kuu
Chivayo, mkewe kuzikwa bila vichwa
Hakika ajali yoyote inaweza kuleta chochote kibaya na wakati mwingine kisichofikirfika mapema. Ona sasa, miili ya Chivayo na mkewe, imepatikana bada ya ajali ya helikopta, Pambazuko linaeleza kuhusu kadhia hiyo.

FAMILIA za mfanyabiashara wa Zimbabwe, Wicknell Chivayo, na mkewe, Lucy Muteke zimekubaliana kuwazika pamoja katika Makaburi ya Glen Forest, Harare, Alhamisi, Oktoba 8, 2026.
Hatua hiyo inafuatia kukamilika kwa taratibu za kitaalamu za kutambua vinasaba vya mabaki ya miili yao.
Miili ya wawili hao itazikwa bila kuwa na vichwa, baada ya jitihada ya kuvipata kushindikana kutokana na kuungua.
Taarifa ya mazishi kutoka kwa familia, shughuli ya kuwapumzisha wanandoa hao imepangwa kuanza saa nane mchana. Walifariki Septemba 30 katika ajali ya helikopta kwenye shamba la Kudenga, eneo la Marondera.
Uamuzi wa kuwazika Harare umeelezwa kuwa njia ya kuwawezesha ndugu, marafiki, washirika wa biashara kupata wasaa wa kuzuru kaburi la watu hao
Msemaji wa familia, Herbert Chivayo, amesema familia zimezingatia kwamba watu wengi waliowafahamu wanandoa hao wanaishi katika mji mkuu huo.
Imeelezwa kuwa waombolezaji hawatapewa nafasi ya kuona miili na kwamba uamuzi huo umetokana na hali ya mabaki baada ya helikopta kuanguka na kuwaka moto.
Katika ufafanuzi mwingine, Herbert, ambaye ni mjomba wa Chivayo, amekanusha madai yaliyosambaa mitandaoni kwamba vichwa vya wanandoa hao vilipatikana kwenye eneo la ajali.
Gazeti la The Guardian limemnukuu akieleza kuwa baadhi ya mabaki yalidhaniwa awali kuwa sehemu za vichwa, lakini uchunguzi wa wataalamu haukuthibitisha dhana hiyo. Kwa maelezo yake, vichwa havikuwa vimepatikana wakati alipotoa taarifa hiyo.
Herbert amesema moto uliharibu miili ya waliokuwa ndani ya helikopta, kiasi kwamba utambuzi wa kawaida haukuwezekana.
Ilibidi kutumika kwa utaalamu wa kutambua vinasaba kulikofanywa na wajuzi wa uchunguzi wa mabaki pamoja na vipimo.
Ajali hiyo pia iliwaua rubani, Calvin Tafirei Soda, rubani msaidizi, Courage Mutavirwa na msaidizi wa ulinzi wa Chivayo, Senelisiwe Magagula.
Chanzo cha kuanguka kwa helikopta bado kinachunguzwa, ingawa taarifa za awali zinadokeza kuwa mabadiliko ya hali ya hewa huenda yalikuwa chanzo kikubwa cha kutokea kwa ajali hiyo.
Chivayo alikuwa mfanyabiashara mwenye umaarufu mkubwa Zimbabwe na nje ya nchi hiyo, akijulikana kwa kugawa zawadi za magari na fedha pamoja na ukaribu wake na viongozi mbalimbali wa Afrika.
Katika taarifa yao ya pamoja, familia za Chivayo na Muteke zimewashukuru wananchi kwa kuwafariji wakati huu wa majonzi.
Zimesema zinaendelea kushikamana katika huzuni, huku zikikamilisha maandalizi ya mazishi yatakayowakutanisha waliowafahamu wanandoa hao kwa ajili ya kuwaaga pamoja.
- chivayo
- kuzikwa
- Lucy