Habari Kuu
Chivayo na gharama, uhuru wa kuingia Ikulu za Afrika apendavyo
Bilionea Chivayo wa Zimbabwe alikuwa akiingia Ikulu za baadhi ya viongozi wa Afrika na kujiachia kama yuko mgahawani. Ukaribu wake na marais wa nchi hizo sasa umethibitika ulikuwa ukiwezekana kwa gharama kubwa, Pambazuko linaweza kueleza zaidi.

MFANYABIASHARA tajiri wa Zimbabwe, Wicknell Chivayo, amekuwa akivuta hisia za wengi kutokana na ukaribu wake na marais wa Afrika, huku vyanzo vya Pambazuko Digital vikidai kwamba alitumia fedha nyingi kurahisisha ukaribu huo.
Chivayo, ambaye alifariki kwenye ajali ya helikopta iliyotokea Jumatano – Septemba 30, 2026, anaelezwa kuwa moja ya “starehe” zake ni kukutana na wakubwa, hasa viongozi wan chi kwa “gharama yoyote ile.”
Taarifa zilizowasilishwa kwa gazeti hili zinadai kuwa baadhi ya safari zake zilihusisha matumizi yanayofikia hadi dola za Marekani 200,000 (zaidi ya Shilingi milioni 500) kuingia Ikulu na kukutana na rais.
Vyanzo vinadai kwamba baadhi ya wasaidizi wa karibu wa viongozi hao na hata wanafamilia walirahisisha kufanyika kwa “vikao” hivyo.
Wanufaika wakubwa wa safari za Chivayo kumfikia rais ni pamoja na wasaidizi wa rais, wasiri wake, watoto na wakuu wa safu ya usalama wa kiongozi huyo.
Hata hivyo, kiasi hicho, waliopokea fedha na madhumuni ya malipo havijapata uthibitisho wa moja kwa moja wa nyaraka kwa kuwa hufanyika kwa njia isiyokuwa wazi.
Kilichothibitishwa hadharani ni kwamba Chivayo alikutana mara kadhaa na viongozi wa kikanda, akiwamo Rais William Ruto wa Kenya.
Agosti 2026, bilionea huyo alichapisha video kwenye mitandao yake ya kijamii akiwa ndani ya gari lililoendeshwa na Ruto kuelekea eneo la kutua helikopta katika makazi ya rais huyo, Kilgoris. Alikuwa amehudhuria hafla ya uchumba wa Charlene Ruto, binti wa rais.
Akizungumza na Gazeti la The Times la Zambia, Chivayo alisema uhusiano wake na Ruto ulikuwa wa binafsi, uliotokana na imani, heshima na ushauri na kukanusha kutumia ukaribu huo kupata zabuni na upendeleo katika biashara ama uwekezaji.
Huko Afrika Kusini, Rais Cyril Ramaphosa aliripotiwa kusema hamfahamu Chivayo baada ya kuonekana naye wakati wa ziara katika shamba la Rais wa Zimbabwe, Emmerson Mnangagwa, Mei 3, 2026.
Aidha, Rais Mnangagwa alikanusha madai kwamba alikuwa akimfadhili Chivayo kusambaza magari na fedha kama zawadi, hasa wakati wa kukaribia uchaguzi wa nchi hiyo.
Chivayo amewahi kukabiliwa na mashitaka kuhusu mradi wa umeme wa jua huko Gwanda. Machi 13, 2023, na Mahakama ya Zimbabwe ilimwachia huru yeye na kampuni yake, Intratrek, katika mashitaka manne, yakiwamo udanganyifu na utakatishaji fedha, kutokana na ukosefu wa Ushahidi.
Kutoka maisha magumu hadi utajiri
Wicknell Chivayo alizaliwa mwaka 1982 na kukulia Gandami, eneo la Chivhu katika Mkoa wa Mashonaland East, Zimbabwe. Alipokuwa na takribani miaka 10, baba yake, Isaac Mathias Chivayo, alifariki katika ajali ya gari, na jukumu la kumlea likabaki kwa mama yake.
Alisoma Dudley Hall Primary School, kisha akaingia Churchill Boys High School. Changamoto za kifedha zilimkatisha masomo mwaka 1996.
Mwaka uliofuata, 1997, aliamua kuajiriwa kwenye kampuni ndogo na kupewa kazi ya kuwa “mtu wa hesabu” ikiwamo kushughulikia malipo ya mishahara kwa kuwa alikuwa akijua hesabu.
Baadaye, alianzisha Intratrek Zimbabwe, kampuni iliyopata mikataba katika sekta za nishati na miundombinu.
Biashara hizo zilipanua jina lake, lakini pia zikamwingiza katika migogoro ya kisheria, hasa kuhusu utekelezaji wa miradi ya umma.
Miongoni mwa mashauri yaliyovuta hisia ni lile la mradi wa umeme wa jua wa megawati 100 wa Gwanda. Chivayo na Intratrek walikabiliwa na mashitaka yanayohusiana na matumizi mabaya ya fedha za mradi huo, lakini Machi 2023 wakaachiwa katika mashitaka manne, yakiwamo udanganyifu na utakatishaji fedha, kutokana na ukosefu wa ushahidi.
Kando ya kesi hiyo ya jinai, Intratrek na Kampuni ya Umeme ya Zimbabwe (ZPC) walikuwa na mgogoro kuhusu uhalali na utekelezaji wa mkataba na Januari 11, 2023, Mahakama Kuu iliamua kwamba mkataba uliendelea kuwa halali na kuziagiza kampuni hizo kuutekeleza.
Desemba 1 mwaka huo, Mahakama ya Juu ilitupilia mbali rufaa ya ZPC na kuamuru Chivayo na kampuni yake kulipwa kiasi kikubwa cha fedha.
- chivayo
- ikulu
- utajiri
- bilionea