Uchumi & Biashara
CRDB yapata mkopo wa bil. 800/-
Mafanikio ya Benki ya CRDB yametokana na ufaninisi wa majukumu yake na imani kutoka kwa wateja wake, hivyo, kuwa na nafasi ya kuongeza mtaji wake kupitia taasisi za fedha ndani na nje ya Tanzania.

BENKI ya CRDB imefanikiwa kupata mkopo wa pamoja wa dola milioni 300 za Marekani (karibu sawa na bilioni 800/-) kutoka kwa taasisi za kimataifa, hatua inayoongeza uwezo wake kuwawezesha wateja na kuchochea ukuaji wa uchumi katika masoko ya Tanzania, Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC).
Mafanikio haya yamekuja baada ya CRDB kuweka lengo la awali la kukusanya dola milioni 150, lakini ikaweza kuvutia ahadi za uwekezaji zenye thamani ya dola milioni 744 kutoka kwa taasisi mbalimbali za kimataifa, katika mpango ulioratibiwa na Investec na Intesa Sanpaolo.
Hii ni mara ya tano mfululizo kwa CRDB Bank kushirikiana na Investec na Intesa Sanpaolo katika mpango wake wa ufadhili wa pamoja, huku mwaka huu ukiashiria pia kuanzishwa kwa awamu mpya ya mkopo wa miaka mitatu.
Akizungumza kuhusu hatua hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa CRDB Bank, Dkt. Abdulmajid Nsekela, amesema mafanikio haya yanaakisi imani inayoendelea kujengwa katika masoko ya kimataifa kuhusu uwezo, uthabiti na mwelekeo wa ukuaji wa CRDB Bank.
Fedha hizi zitaongeza uwezo wa Benki kutoa suluhisho za kifedha kwa wateja wake, kusaidia upanuzi wa biashara, na kuchangia katika maendeleo ya uchumi katika masoko ambayo CRDB Bank inayahudumia.
Dkt. Nsekela amewashukuru Investec, Intesa Sanpaolo na washirika wote wa kifedha kwa kuendelea kuiamini na kuiunga mkono CRDB Bank katika safari yake ya kuimarisha nafasi yake kama mshirika wa maendeleo na biashara katika Afrika Mashariki na Kati.
- Crdb
- Uchumi
- Mkopo
- Biashara