Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Biashara

Dhahabu bado kinara pato la kigeni

Uchumi wa Tanzania sasa unabebwa zaidi na fedha za kigeni zinazotokana na mauzo ya dhahabu, Gazeti la Pambazuko linaeleza.

Alhamisi, 17 Septemba 2026 · 12:27Dakika 2 kusoma
Shehena ya dhahabu
Shehena ya dhahabu — Picha kutoka Maktaba ya Pambazuko

DHAHABU imeendelea kuwa mhimili wa pato la kigeni kwani mauzo yake ndiyo yanaongoza kuiingizia nchi fedha za kigeni, Benki Kuu Tanzania (BoT), imeeleza.

Ripoti ya hali ya uchumi kwa mwezi Julai (MER) iliyotolewa na BoT hivi karibuni inaonyesha kuwa kwa jumla sekta ya mauzo ya nje imeendelea kuonyesha ustahimilivu na ukuaji mzuri kwa mwaka unaoishia Julai 2026.

Katika kipindi hicho, BoT inaeleza, jumla ya mauzo ya bidhaa na huduma nje ya nchi iliongezeka kwa asilimia 16.5 na kufikia dola za Marekani milioni 19,985.8 ikilinganishwa na kipindi kama hicho mwaka 2025.

Kwa mujibu wa ripoti hiyo, dhahabu imeendelea kuwa bidhaa nambari moja na nguzo kuu nchini kwa kuingiza fedha nyingi zaidi za kigeni.

Katika mwaka unaoishia Julai 2026, mauzo ya dhahabu nje ya nchi yalipanda kwa asilimia 37.4 na kufikia dola za Marekani milioni 5,670.7 (kutoka dola milioni 4,127.1 mwaka uliopita).

Mchango wa dhahabu pekee unawakilisha asilimia 47.4 ya mapato yote ya mauzo ya bidhaa nje ya nchi.

Kwa mujibu wa BoT, dhahabu imeendelea kuwa kinara wa kuingiza fedha za kigeni kutokana na bei nzuri ya madini hayo katika soko la kimataifa.

Huduma nyingine Mapato ya Tanzania kutoka kwenye masoko ya kimataifa yanaonyesha taswira nzuri ya ukuaji wa uchumi, ikichangiwa na mchanganyiko wa sekta za huduma, uzalishaji wa viwandani, na kilimo.

Mbali na dhahabu, mapato ya fedha za kigeni yamechangiwa pia na bidhaa na huduma nyingine kadhaa ikiwemo utalii na mazao ya kilimo.

Katika sekta ya huduma, utalii unaendelea kufanya vizuri kama mhimili mkuu wa kuingiza fedha za kigeni. Kuimarika kwa sekta hii kuliiwezesha kuingiza kiasi cha dola za Marekani milioni 4,292.8, kwa mujibu wa ripoti hiyo ya BoT.

Wakati huohuo, sekta ya usafirishaji nayo ilirekodi ukuaji wa asilimia 29.7 na kufikisha mapato ya dola za Marekani milioni 3,221.5, mafanikio yaliyotokana na kuongezeka kwa shehena ya mizigo inayopitishwa kuelekea nchi jirani (transit goods), hasa kupitia Bandari ya Dar es Salaam.

Kwa upande wa bidhaa za viwandani, nchi imepiga hatua kubwa kwa kushuhudia ukuaji wa uzalishaji kwa asilimia 46 na kuliingizia taifa dola za Marekani milioni 2,215.5.

“Ongezeko hili lilichochewa zaidi na mauzo ya bidhaa za chuma na nondo, vito vya kioo, pamoja na nguo,” inasema BoT katika ripoti hiyo.

Sekta ya kilimo pia haikubaki nyuma, ambapo uzalishaji wa mazao ya asili uliongezeka kwa asilimia 14.9 na kufikia thamani ya dola za Marekani milioni 1,628.8.

Ndani ya kundi hili la mazao ya asili, tumbaku ilikuwa kinara kwa kuingiza dola za Marekani milioni 588.6, ikifuatiwa na korosho zikiingiza dola za Marekani milioni 479.3, huku kahawa ikisaidiwa na bei nzuri katika soko la dunia na kuingiza dola za Marekani milioni 396.0.

  • uchumi
  • tanzania
  • dhahabu
  • mauzo

Soma Pia