Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Uchumi & Biashara

Madhara kupanda mfumko wa bei ‘yatokota’

WACHUMI wanaonya kuwa ingawa takwimu zinaonyesha kuwa mfumko wa bei haujafika kwenye hali mbaya sana, lakini mwenendo wake katika miaka ya hivi karibuni ni suala linalopaswa kuanza kufikiriwa kwa kina na hatua kuchukuliwa.

Jumatatu, 14 Septemba 2026 · 03:00Dakika 2 kusomaToleo 182, uk. 18

WACHUMI wanaonya kuwa ingawa takwimu zinaonyesha kuwa mfumko wa bei haujafika kwenye hali mbaya sana, lakini mwenendo wake katika miaka ya hivi karibuni ni suala linalopaswa kuanza kufikiriwa kwa kina na hatua kuchukuliwa.

Takwimu zinazotolewa na Benki Kuu (BoT) zinaonyesha kuwa mfumko wa bei nchini Tanzania umeendelea kubaki ndani ya lengo la kitaifa na vigezo vya kikanda vya Jumuia ya Afrika Mashariki (EAC) na SADC.

Lakini kiwango cha mfumko wa bei kimekuwa kikipanda kila takwimu mpya zinapotolewa.

Mathalan, ripoti ya hali ya uchumi (MER) iliyotolewa hivi karibuni na BoT inaonyesha kuwa mfumko wa bei wa mwaka hadi mwaka ulifikia asilimia 4.2 mwezi Julai 2026, ikilinganishwa na asilimia 4.0 mwezi Juni 2026 na asilimia 3.3 mwezi Julai 2025.

“Pamoja na kwamba kiwango hiki hakijafikia viwango vya juu vya kurekodiwa au vile vya ukomo wa kikanda, mwenendo huu wa kupanda kwa mfumko wa bei kwa miezi ya hivi karibuni unaonyesha wazi presha inaongezeka katika uchumi wa watu binafsi,” anabainisha mchumi mmoja aliyezungumza na Pambazuko.

Taasisi za uchumi ikiwemo BoT zinataja athari za gharama za mafuta ambazo zimesababisha kupanda kwa gharama za usafirishaji kuwa ndio kisababishi kikubwa kwa ongezeko hili la mfumko wa bei.

Kwa mujibu wa MER hiyo, mfumko wa bei wa msingi (core inflation) - ambao hauhusishi chakula na nishati, ulipanda hadi asilimia 3.9 mwezi Julai 2026 kutoka asilimia 3.7 mwezi Juni na asilimia 1.9 mwezi Julai 2025.

Vilevile, mfumko wa bei za nishati, mafuta, na huduma uliongezeka hadi asilimia 6.9 mwezi Julai 2026.

Hata hivyo, BoT inabainisha katika ripoti hiyo kuwa utulivu wa bei za vyakula (ambazo zilibaki asilimia 4.1 mwezi Julai) kutokana na mavuno na akiba ya chakula nchini, umesaidia kwa kiasi kikubwa kuzuia mfumko wa bei usipande kwa kasi zaidi.

Athari kwa mwananchi

Kupanda huku kwa mfumko wa bei kunaamanisha kuwa mwananchi hivi sasa analazimika kutumia kiasi kikubwa zaidi cha fedha kupata bidhaa au huduma ile ile aliyokuwa anaipata mwaka jana.

Wachumi wanabainisha kuwa hii inaamaanisha kuwa gharama za maisha zinazidi kuongezeka.

Wachumi hao wanasema pia kuwa kwa mujibu wa misingi ya kiuchumi, kupanda huku kwa mfumko wa bei kunamaanisha kupanda kwa gharama za usafiri na huduma.

“Inaamanisha kuwa kiasi kile kile cha fedha anachopata mwananchi sasa hivi kinamnunulia bidhaa na huduma chache zaidi ikilinganishwa na mwaka uliopita,” anafafanua mchumi huyo.

Kwa kuwa gharama za usafirishaji zimepanda na athari zake zinasambaa kwenye bidhaa nyingine, kaya nyingi zitalazimika kutumia sehemu kubwa ya kipato chao kwenye mahitaji ya msingi ya kila siku, hivyo kupunguza fedha za kuweka akiba au kuwekeza.

Hata hivyo, mchumi huyo ametoa msisitiza kwa serikali kuendelea kuimarisha Wakala wa Hifadhi ya Chakula ya Taifa (NFRA) kwani takwimu zinaonesha kuwa utulivu wa bei za vyakula ndio umeshikilia mfumko wa bei kwa sasa.

Umebakiwa na makala 2 za bure mwezi huu. Jiunge ili kusoma bila kikomo.

  • Mfumko wa bei
  • BoT
  • Uchumi
  • Gharama za maisha

Soma Pia