Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Uchumi & Biashara

Fitch yaipa Tanzania mtazamo chanya kiuchumi

KAMPUNI ya kimataifa ya Fitch Rating inayojihusisha kufanya tathmini ya uwezo wa nchi kukopesheka katika masoko ya fedha ya kimataifa, imetoa alama ya B+ kwa Tanzania katika tathmini yake ya hivi karibuni.

Jumatatu, 31 Agosti 2026 · 06:00Dakika 4 kusomaToleo 180, uk. 18
Muonekano wa Jiji la Dar es Salaam, ambalo ni kitovu cha kukuza uchumi wa Tanzania.
Muonekano wa Jiji la Dar es Salaam, ambalo ni kitovu cha kukuza uchumi wa Tanzania. — Kutoka Maktaba ya Pambazuko

Taarifa iliyotolewa na Wizara ya Fedha wiki iliyopita inasema kuwa hatua hiyo ya Fitch inadhihirisha kuimarika kwa misingi ya uchumi na uimara wa sera za uchumi jumla nchini.

Kwa mujibu wa ripoti ya kampuni hiyo iliyochapishwa katika tovuti yake rasmi, Fitch imesema mabadiliko hayo yanatokana na kuimarika kwa akiba ya fedha za kigeni, kuwepo kwa nakisi ya bajeti inayodhibitika na kuendelea kwa ukuaji wa uchumi.

Fitch inaeleza kuwa kwa pamoja mambo haya yanatarajiwa kuongeza mapato kusaidia kuhudumia bajeti ya nchi pamoja na kupunguza mzigo wa deni la serikali. Aidha, Fitch imesema akiba ya fedha za kigeni nchini inatarajiwa kuongezeka kutoka dola za Marekani bilioni 6.3 mwishoni mwa mwaka 2025 hadi kufikia dola bilioni 7.9 mwaka 2028, sawa na uwezo wa kugharamia malipo ya nje kwa takribani miezi 3.3.

Fitch imeeleza kuwa kupungua kwa changamoto katika soko la fedha za kigeni na kuongezeka kwa unyumbufu wa kiwango cha ubadilishaji wa fedha, kumechangia kupunguza baadhi ya hatari za muda mfupi, huku akiba ya dhahabu iliyoko Benki Kuu, inayokadiriwa kufikia dola za Marekani bilioni 2.4, inaweza kuongeza zaidi kinga ya nchi dhidi ya mishtuko ya nje katika nyanja za uchumi.

Katika upande wa bajeti na usimamizi wa deni, Fitch imekadiria kuwa nakisi ya bajeti kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 2026 ilikuwa asilimia 2.8 ya Pato la Taifa, ikichangiwa na ongezeko la ukusanyaji wa mapato na athari ndogo za ruzuku za mafuta katika utekelezaji wa bajeti na inatarajiwa nakisi hiyo kubaki karibu asilimia 3 ya Pato la Taifa hadi mwaka wa fedha 2028.

Katika ripoti yake Fitch imebainisha pia kuwa mapato ya kodi yaliongezeka kutoka asilimia 14.6 hadi asilimia 15.6 ya Pato la Taifa kati ya 2023 na 2025.

Fitch pia imetabiri kuwa uwiano wa deni la serikali kwa Pato la Taifa utapungua kutoka asilimia 48.9 mwaka 2025 hadi asilimia 46.2 mwaka 2028, kiwango ambacho kitakuwa chini ya wastani wa asilimia 55 unaokadiriwa kwa nchi zilizo katika kundi la ukadiriaji wa B.

Imeeleza kuwa kupungua kwa deni kutachangiwa na ukuaji mkubwa wa Pato la Taifa kwa thamani ya sasa pamoja na kuwezesha kuwa na nakisi ndogo ya msingi ya bajeti.

Kwa upande mwingine Fitch imepongeza hatua zinazochukuliwa kuboresha usimamizi wa fedha za umma, ikibainisha kuwa hadi Machi 2026, kiasi cha madeni ya serikali yaliyothibitishwa kwa wazabuni na marejesho ya kodi kilikuwa kimepungua hadi asilimia 0.2 ya Pato la Taifa kutoka asilimia 1.2 ya Desemba 2022.

Kwa upande wa ukuaji wa uchumi, Fitch inatarajia Tanzania kuendelea kufanya vizuri ikilinganishwa na wastani wa nchi zilizo katika kundi la B, ikitabiri ukuaji wa Pato la Taifa kwa asilimia 5.8 mwaka 2026, dhidi ya wastani wa asilimia 3.7 kwa kundi hilo.

Fitch inakadiria kuwa uchumi utakua kwa wastani wa asilimia 6.1 katika kipindi cha 2027–2028, ukichochewa na uwekezaji wa umma, utalii, nafasi ya Tanzania kama kitovu cha usafirishaji na biashara kikanda pamoja na ukuaji wa sekta ya madini.

Wakati huohuo, Fitch inatarajia mfumuko wa bei wa wastani wa asilimia 4.2 mwaka 2026, kutoka asilimia 3.3 mwaka 2025, lakini bado ukiwa chini ya wastani wa asilimia 5.6 unaotarajiwa kwa nchi za kundi la B.

Fitch imeeleza pia kuwa Tanzania imepiga hatua katika kuboresha mfumo wa sera za uchumi jumla tangu mwaka 2023, kupitia maboresho ya kitaasisi na kiutendaji yaliyoimarisha uhuru wa benki kuu, mfumo wa uendeshaji wa kiwango cha ubadilishaji wa fedha na usimamizi wa soko la fedha za kigeni.

Aidha, wameongeza kuwa maboresho hayo yanaweza kuongeza uwezo wa Tanzania kukabiliana na mishtuko ya kiuchumi, ingawa baadhi yake bado yanahitaji kuthibitishwa kupitia utekelezaji wake kwa muda.

Pia wasiwasi wa awali kuhusu uwezo wa takwimu za kitaifa kuakisi mabadiliko ya ukuaji wa uchumi umepungua baada ya kukamilika kwa zoezi la kubadili mwaka wa msingi wa Pato la Taifa Juni 2026.

Fitch inatazamia pia kuendelea kuimarika kwa akiba ya fedha za kigeni, kuongezeka kwa ufanisi katika ukusanyaji wa mapato, udhibiti wa matumizi ya serikali na kushuka kwa uwiano wa deni kwa Pato la Taifa ni miongoni mwa mambo yatakayoweza kuchangia hatua zaidi ya kuboresha ukadiriaji wa Tanzania.

Shirika hilo limeeleza kuwa kuongezeka kwa imani kwamba maboresho ya mfumo wa sera za uchumi jumla yataendelea kuimarisha uwezo wa nchi kukabiliana na mishtuko ya nje na kudumisha utulivu wa uchumi kutakuwa msingi muhimu wa hatua hiyo.

Kwa ujumla, Fitch imeona mwenendo wa uchumi wa Tanzania ukiwa na msingi chanya, huku ikiweka mkazo katika kuendelezwa kwa nidhamu ya fedha, kuimarishwa kwa mapato ya ndani na utekelezaji endelevu wa maboresho ya sera ili kujenga mazingira imara zaidi ya uchumi.

  • Fitch Ratings
  • Uchumi
  • Deni la taifa
  • Wizara ya Fedha

Soma Pia