Biashara
Rwanda yavuruga wauza pombe kali
SERIKALI ya Rwanda imeibua sintofahamu miongoni mwa wazalishaji, wasambazaji na wauzaji wa pombe kali katika nchi za Afrika Mashariki.
Nchi hiyo imepiga marufuku aina 52 za vinywaji vinavyozalishwa katika nchi sita na kuingizwa nchini humo.
Marufuku hiyo inatokana na kile ambacho kimeelezwa kuwa pombe hizo kutokidhi viwango na kwamba ni hatari kwa afya za watumiaji.
Katika marufuku hiyo, kwa Tanzania inahusisha aina 14 za vinywaji vikali vikiwemo maarufu vya Konyagi, K-Vant na Tzee, ambavyo vimetawala katika masoko ya ndani ya nchi hiyo.
Katika taarifa yake ya Jumatano Agosti 5, 2026, Mamlaka ya Chakula na Dawa Rwanda (Rwanda FDA) ilitangaza kupiga marufuku uagizaji, usambazaji, na uuzaji vinywaji hivyo 52 na kufunga viwanda vinane vya ndani vinavyozalisha pombe kali.
Mamlaka hiyo ya Rwanda ilieleza kuwa hatua hiyo ilitokana na kutokea kwa vifo vya watu zaidi ya 50 vilivyoripotiwa kati ya Januari na Juni 2026 na wengine zaidi ya 100 kupoteza uwezo wa kuona baada ya kunywa pombe zisizo salama.
Wazalishaji watikiswa
Akizungumzia suala hilo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Shirikisho la Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Deogratius Massawe alisema hatua hiyo ya Serikali ya Rwanda siyo ya kuchukuliwa kwa wepesi kwa kuwa zuio hilo halihusishi bidhaa za Tanzania pekee, bali pia za ndani ya nchi hiyo, nchi nyingine za Afrika Mashariki za nje ya Afrika.
Massawe alilieleza Pambazuko kuwa katika ufuatiliaji wa awali, ameona agizo hilo likitolewa kama mkakati wa ndani wa taifa hilo kuzuia unywaji pombe uliopitiliza, baada ya Rais Paul Kagame kuhutubia moja ya mkutano wa vijana ambapo alieleza namna ambavyo nguvu kazi imekuwa ikitatizwa na unywaji pombe holela wa vijana, hasa pombe kali.
“Kwa Rawanda, wale wako tofauti kidogo na hizi nchi zetu nyingine. Inaonekana kama hilo tayari lilikuwa agizo kutoka kwa Rais Kagame na huenda muda siyo mrefu ikipitishwa sheria rasmi...”
“Lakini kwa muda huu bado tunaendelea na juhudi za kujua uhalisia wa agizo hilo na kuangalia iwapo kweli zuio hilo linaheshimu makubaliano ya kibiashara baina ya nchi zetu...”
“Mara zote tunapokutana tunanadi soko la nchi zetu za Afrika Mashariki, na hapa ninaona ubaya unaoweza kujitokeza ni kwa nchi nyingine ambazo Rwanda inapeleka bidhaa zake, nazo zinaweza kuchukua tahadhari kali dhidi ya baadhi ya bidhaa zao.
Lakini hadi sasa bado tunatoa nafasi kwao ili waeleze kwa kina sababu za hatua hiyo, huenda zikawa zenye mashiko, tutajua namna ya kwenda nao,” alisema.
Alieleza kuwa katika juhudi za awali, TPSF imefanya mawasiliano na Balozi wa Rwanda nchini Tanzania ambaye tayari amekubali kukutana nao siku chache zijazo kuzungumzia suala hilo, ambapo watataka kujua kwa undani sababu za hatua hiyo.
Amesema kwa sasa maswali ambayo wengi wanaendelea kujiuliza mambo kadhaa iwapo hatua ya kuzuia na kutaka mzigo wote uliokuwepo wakati wa agizo hilo urejeshwe kwa wenyewe ni sahihi.
Wazalishaji washituka
Pambazuko lilifanikiwa kuwafikia baadhi ya wazalishaji wa ndani, ambapo mmoja wa watendaji ndani ya Kampuni ya Tanzania Breweries Limited (TBL) ambayo kinywaji kilichoko chini yao cha Konyagi kimeguswa, alieleza kuwa kwa sasa hawawezi kusema lolote kwa kuwa ndiyo wamelipokea na ni jambo ambalo hawakulitarajia.
“Kwa upande wetu, tunaendelea kufanya mawasiliano na tunaliona liko katika upeo wa kiserikali zaidi...”
“Sisi tunaendelea kufuatilia kwa mamlaka zinazohusika na tutatoa taarifa yetu rasmi tutakapojiridhisha kuhusu athari na hasara halisi tutakayokuwa tumeipata kupitia agizo hilo,” alieleza huku akikataa jina lake kutajwa gazetini.
Serengeti Breweries Limited (SBL) ambayo baadhi ya vinywaji vyake navyo vimeguswa, msemaji wa kampuni hiyo, Timoth Msoffe alilieleza Pambazuko kuwa wamepata taarifa hiyo na wanaifanyia kazi hasa kwa ajili ya kuangalia athari wanazoweza kuzipata kama wazalishaji na hata kwa wasambazaji wao.
“Kwa sasa athari za moja kwa moja zinakwenda kwa wasambazaji tunaofanya nao biashara, ambao ndio wanaochukua mzigo kwetu na kupeleka nje hasa huko Rwanda...”
“Tumepata taarifa hizo na tunaendelea kufanya juhudi za kuwasiliana na ubalozi wa Rwanda nchini na taasisi zinazosimamia biashara kati ya Tanzania na nchi za nje ili kujua hatua tunazoweza kuchukua kwa sasa,” alisema.
Ubalozi wakaa kimya
Mmoja wa maofisa wa ubalozi wa Rwanda nchini aliyefikiwa na Pambazuko alisema hawezi kuzungumza lolote kwa kuwa yeye siyo msemaji wa ubalozi, hivyo balozi atakuwa katika nafasi nzuri ya kuzungumzia suala hilo baada ya kumalizika kwa mapumziko ya mwishoni mwa wiki.
Wizara yavuta pumzi
Mkurugenzi Mawasiliano katika Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Mindi Kassiga alisema kwa sasa suala hilo linahusika zaidi na mamlaka za Rwanda na jumuiya za wafanyabiashara kwa kuwa limetolewa na Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Rwanda (Rwanda FDA) na inahusiana na suala la ubora.
Alisema kwa hatua hii, wanaohusika moja kwa moja na suala hilo ni mamlaka ya viwango nchini, ubalozi wa Rwanda na mamlaka nyingine zinazohusiana moja kwa moja na wazalishaji wa ndani wanaouza bidhaa zao huko.
Balozi huyo alisema kabla ya kufika katika hatua ya wizara kuingilia, kuna mamlaka nyingi ambazo zinatakiwa kulishughulikia katika hatua za awali na iwapo zikikwama ndipo Wizara itakapochukua hatua, hasa kwa kuzingatia matokeo ya ukaguzi na uthibitisho wa ubora kama ambavyo nchi husika inahitaji kulingana na viwango vyake.
Taarifa ya Rwanda FDA
Mamlaka ya Chakula na Dawa ya Rwanda, ikitumia sheria na nchini humo na kwa maslahi ya afya ya umma, iliwaeleza waagizaji, wasambazaji, wauzaji rejareja na umma kwa ujumla kwamba uingizaji wa vinywaji vyenye pombe vilivyoorodheshwa katika kiambatisho umesimamishwa kwa muda na kuwa agizo hilo limeanza kutumika mara moja.
FDA ya Rwanda iliwaagiza waagizaji wa bidhaa hizo kuanza mara moja kurudisha bidhaa hizo, kuwaagiza wasambazaji wa bidhaa za kigeni kurejesha bidhaa zilizoorodheshwa kutoka kwa wateja wao.
Kurudisha hisa za sasa na bidhaa zilizorejeshwa kwa waagizaji na waagizaji kuwasilisha ripoti za kurejeshwa kwa bidhaa ndani ya siku tatu za kazi tangu kuchapishwa kwa tangazo hilo, yaani kufikia leo, Jumatatu Agosti 10, 2026.
Pia FDA ya Rwanda iliwaagiza wasambazaji na wauzaji rejareja wote wa bidhaa zilizoorodheshwa kuacha mara moja usambazaji na uuzaji wao, na kuwarejeshea waagizaji wao kiasi kilichobaki mara moja na watumiaji wa vileo vilivyoorodheshwa kuacha mara moja matumizi yao na marufuku ya matangazo yote na nyenzo za utangazaji wa vileo zilizoorodheshwa lazima ziondolewe mara moja kutoka popote zinapoonyeshwa.
Kati ya bidhaa zilizopigwa marufuku nyingi zinatokea nchini India yenye bidhaa 20 ikifuatiwa na Tanzania (bidhaa 14), Uganda (11), Kenya (5), Burundi (1) na Poland (1).
- Rwanda
- Pombe
- Afrika Mashariki
- Biashara