Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Michezo

Dabi Kariakoo joto lapanda, lashuka!

HOMA ya dabi ya Kariakoo inazidi kupanda huku timu zote mbili; Simba na Yanga zikiendelea kujinoa kwa mazoezi makali kwa ajili ya maandalizi ya mchezo huo mkubwa utakaochezwa Oktoba 10, 2026.

Jumatatu, 28 Septemba 2026 · 06:00Dakika 1 kusomaToleo 184, uk. 44

Mnyama ambaye ameweka kambi ya siku 10 nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kuhakikisha anafuta uteja wa kupigwa mara ya sita mfululizo katika kipindi cha misimu mitatu kwenye Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.

Yanga nayo siyo kinyonge, inazidi kujinoa kuhakikisha inaendeleza ubabe wake kwa Mnyama, ikiwa imesalia Dar es Salaam, huko katika kambi ya Avic Town, Kigamboni.

Tayari mashabiki wa watani hao wa jadi wanazidi kunogesha tambo kwa kila mmoja kutamba kwamba atachukua pointi tatu kutoka kwenye mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa.

“Safari hii hatukubali kufungwa na Yanga maana imeshaanza kuwa mazoea kila siku sisi, hatukubali kwani tuna timu nzuri, winga zetu nzuri Libasse na Oura wote wanafanya vizuri siku hiyo Yanga atalia lazima,” amesikika shabiki wa Simba, Shukuru Ramadhani, mkazi wa Kijitonyama, Dar es Salaam.

Kwa upande wa mashabiki wa Yanga, wao wanadai kwamba hawana wasiwasi, wanasubiri tu kuchukua pointi tatu kwa “mteja wao.”.

“Yanga hatuna wasiwasi kabisa, tunasubiri tu kuchukua pointi tatu zetu kama kawaida, hao Simba wajiandae kulia kama wanavyofanya siku zote,”.

amesema Hanifa Said, mkazi wa Tabata Matumbi.

Ikumbukwe timu zote zimeshinda katika michezo yake sita ya mwanzo mwa msimu huu 2026/27, huku Yanga wakifunga mabao 16 na kuruhusu mabao 2 tu katika michezo sita ya Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara Simba pia imeshinda mechi zote sita na kufunga jumla ya mabao 11 na kuruhusu mabao 2 tu katika michezo yote sita ya Ligi Kuu ya NBC Tanzania Bara.

Je, nani atashinda mechi hiyo inayobeba hisia za mashabiki wengi wa kabumbu la Tanzania, je ni Simba au Yanga? Muda ndiye na kipyenga cha mwisho ndiyo waamuzi.

  • Simba
  • Yanga
  • Dabi
  • Kariakoo
  • Soka

Soma Pia