Rukia maudhui makuu
Pambazuko
Ukweli Hauna Kutu

Michezo

Mnyama hachekeshi Afrika, Wananchi poa tu

WAWAKILISHI bora wa muda mrefu katika mashindano ya kimataifa kutoka ardhi ya Julius Kambarage Nyerere, Klabu ya Simba, hawachekeshi hata kidogo linapokuja suala la mechi za kimataifa Afrika.

Jumatatu, 14 Septemba 2026 · 03:00Dakika 1 kusomaToleo 182, uk. 38

WAWAKILISHI bora wa muda mrefu katika mashindano ya kimataifa kutoka ardhi ya Julius Kambarage Nyerere, Klabu ya Simba, hawachekeshi hata kidogo linapokuja suala la mechi za kimataifa Afrika.

Hilo limedhihirika tena jana baada ya kuwasasambua Mighty Wonderes ya Malawi kwa mabao 6-1.

Simba walirejea katika mitaa ya Temeke kuendeleza ubabe wao msimu huu kwa kuwakaribisha Mighty Wonderes kwenye Dimba la Uhuru, mchezo wa mkondo wa pili wa hatua za awali ambapo wametinga kwa kishindo hatua ya mtoano kutinga makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika (CAF CL).

Jana -Septemba 13, Mnyama aliunguruma kwenye mbuga anayotamba sana kwa kutoa burudani ya kabumbu na sanaa ya kucheza na nyavu chini ya watumbuizaji bora, Clatous Chota Chama na Libasse Gueye.

Mabao ya Simba yaliwekwa kambani na Chama aliyefunga mara mbili, Libase mara mbili, huku Morice Abraham na Keletso wakifunga bao moja moja na kuwafurusha Wamalawi hao kwa jumla ya mabao 7-1.

Sasa kazi inafuata salamu zinawaendea wapinzani ambao watakuwa na kibarua kizito kuja Dar es Salaam kukabiliana na joto la Jiji na pumzi ya moto ya Mnyama katika jioni za Ligi ya Mabingwa.

Wakati Simba akicheka, Wananchi, Timu ya Yanga nao walikenua Septemba 12 katika Uwanja wa Azam Complex, Chamazi kwa kuwatupa nje Gaborone United ya Botswana kwa jumla ya mabao 3-2. Ni baada ya kushinda mabao 2-1 kwenye mtanange huo.

Ikumbukwe Simba na Yanga msimu huu zimebeba bendera ya Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika, huku Azam FC na Singida Black Stars wakiwakilisha kwenye kombe la Shirikisho CAF CC.

Umebakiwa na makala 2 za bure mwezi huu. Jiunge ili kusoma bila kikomo.

  • Simba
  • Yanga
  • CAF Champions League
  • Mpira wa miguu

Soma Pia