Michezo
Dakika 360 za kibabe kwa Simba, Yanga
DAKIKA 360 za Ligi Kuu Soka ya NBC PL 2026/27 zimetimia kwa kila klabu kucheza michezo minne, huku maji na mafuta vikianza kujitenga katika safari ya kuwania ubingwa wa Tanzanzia Bara msimu huu.

Klabu za Simba na Yanga zimeanza kwa kishindo kizito msimu huu, kwa kila timu kupata ushindi wa asilimia miamoja za michezo hiyo minne, na kuwasha taa ya kijani ya kuwania taji, umande ukiwa haujakauka.
Wananchi Yanga ambao ni mabingwa watetezi, wamevuna pointi 12 katika dakika 360, dhidi ya Namungo FC, Coastal Union, JKT Tanzania na Pamba Jiji FC, wakifunga mabao 13 na kuruhusu mabao 2, na kuwa nafasi ya kwanza kwenye msimamo.
Wakati huo Mnyama Simba akivuna pointi 12 kwenye michezo minne sawa na watani zao ambapo, amewapepeta Kagera Sugar, Pamba Jiji FC, Singida Black Stars na Coastal Union, mabao 7 ya kufunga huku wakiruhusu mabao mawili, nafasi ya pili kwenye msimamo kwa tofauti ya mabao ya kufunga.
Kwa namna miamba hiyo ilivyoanza ligi ni wazi vita ndio vimeanza upya licha ya Wananchi kutamba katika misimu mitano mtawalia, huu ukiwa wa sita ambapo Mnyama ana kazi ya kujiuliza kama atarejesha ufalme wake msimbazi kwa kunyanyua taji hilo.
Swali ni je, ni Simba ama Yanga atakayedondosha alama msimu huu kwa kupata, suluhu, sare ama kupoteza? Wakati tunasubiri majibu katika mahakama ya muda, Azam FC wao wamerejea kwenye maisha yao ya kawaida ya kushindwa kutamba ugenini.
Ni kama mzimu wao hauna furaha kabisa wakiwa katika viwanja vya mikoani, Azam, wamecheza dakika 360, dakika 180 sawa na michezo miwili ya ugenini dhidi ya Polisi Tanzania na Geita Gold zote wameambulia sare.
Katika alama 12 tayari wameangusha alama 4, sawa na asilimia 33.33 za pointi walizopoteza, wakishika nafasi ya nne nyuma ya Mbeya City wenye pointi tisa, wakishinda michezo mitatu na kupoteza mmoja.
- Simba
- Yanga
- NBC PL
- Azam FC